2017-12-01 14:00:00

Tujiandae kwa kukesha:Kudumu katika matendo mema kwa ndugu na jirani!


Mama Kanisa Mtakatifu sana anatualika kuingia katika Mwaka mpya, Mwaka B wa Kanisa. Hii ni ishara ya upyaishaji wa daima wa maisha ya Kanisa na hivyo kulifanya kuonekana daima jipya na linalopendeza. Mwaka mpya wa Kanisa uanza kwa kipindi cha Majilio. Neno “Majilio” linajieleza lenyewe kuwa ni tenda la kufika au kuingia kwa kitu au jambo fulani na kunapokuwa na ujio bila shaka kunakuwa na wanaongojea. Kwa upande wa wangojeao hujikita katika maandalizi ili kumpokea huyo ajaye! 

Kristo amekwishakuja ulimenguni; sasa tutajiuliza tunangojea nini au ni ujio gani huo? Hili linaelezeka kwa kukiangalia kipindi hichi ambacho kinagawanywa katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza inatutafakarisha juu ya ujio wa pili wa Kristo. Ujio wake huu wa pili ni wa hakika kwani Mwenyewe aliahidi akisema: “Nakwenda kwa Baba kuwaandalia mahali… nitakuja tena kuwakaribisha kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo” (Yoh 14:2b, 3b). Hivyo maandalizi yetu yanajikita katika kuungojea huo ujio wake wa pili. Sehemu ya pili ambayo inaanza tarehe 17 Desemba inajikita katika maandalizi ya Sherehe ya Noeli ambayo inakusudia kulifanya hai tendo la Kristo kuzaliwa kati yetu zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Adhimisho hilo linamwingiza Kristo katika nyua za mioyo yetu na hivyo anakuwa kweli kielelezo na kitovu cha safari yetu ya Mwaka huu mpya wa Kanisa tunaouanza.

Somo la kwanza linatuwekea taswira ya mmoja ambaye yupo katika hali ya toba kwa Bwana. Huyu anaonesha kuwa anamfahamu vema Mungu ila katika maisha yake ameingia katika ukengemfu. Sehemu hii ya Neno la Mungu inadokeza tabia tatu za kipindi hiki cha Majilio. Kwanza ni kipindi cha toba na kuanza upya. Mwenyezi Mungu amewatendea mambo makubwa na kuwakomboa lakini anakiri akisema: “tazama ulikuwa na hasira, nasi tulitenda dhambi; tumekuwa katika mambo haya muda mwingi; nasi, je! Tutaokolewa?” Taifa la Israeli linarejea na kukumbuka uovu waliotenda kwa kumuasi Mungu pamoja na kwamba aliwapenda sana. Sasa wanajaribu kuona kama Mungu atawarudisha tena. Wanapokuwa katika hali ya uasi kungoja kwao kunakuwa bure. Wanapaswa kufanya toba na kumgeukia Mungu. Pili, majira haya yanatuelekeza kuutambua tena ukuu wa Mungu na nafasi yake kwetu. “Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u Baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi tu kazi ya mikono yako”. Hivi majira haya yanaturudisha tena katika njia ya reli na kutembea katika namna iliyo sahihi.

Tatu, kipindi cha Majilio kinatukumbusha kukesha daima katika uaminifu wetu kwa Mungu. “Wewe wamlaki yeye afurahiaye yaliyo haki na kuyatenda, watu wale wakukumbukao katika njia zako”.  Tendo la kukesha linasisitiziwa vizuri katika somo la Injili. Kristo anasema: “Angalieni, kesheni, ombeni, kwa kuwa hamjui wakati ule utakaokuwapo”. Kristo anatumia mifano inayoeleweka. Mlinzi anayeachiwa kulinda nyumba wakati Bwana wake kasafiri atabaki macho na kuwa makini ili asikose malipo yake wakati atakaporudi Bwana wake. Huyu hawezi kulala kwanza kwa kuogopa mali aliyoachiwa isipotee na pili atakaporejea Bwana wake kwa saa asiyoijua hamkute yupo macho. Huu ni mfano wa maisha yetu katika imani. Imani hii tumepewa wakati wa Ubatizo na katika liturujia yake tulipewa mchumaa uwakao ishara ya Kristo ambao tunapaswa kuulinda wakati wote.

Maisha ya mwanadamu wa leo ambayo yamegubikwa na mahangaiko mengi ya kidunia yanatoa nafasi finyu kwa mmoja kuwa hai katika imani yetu. Mahitaji na matarijio ya kimwili na ya kidunia yanatusonga na kutufanya kuipa kisogo imani yetu. Tunatafuta masuluhisho ya kuuridhisha mwili na matamanio ya kidunia. Neno la kuambiwa kutenda katika hali ya kukesha kiroho linakosa ladha. Ndivyo wengi tunavyofanya maandalizi yetu na kwa bahati mbaya hata katika matukio ya kiimani. Mfano halisi ni kipindi hiki tulichopo. Pamoja na kwamba tunafahamu kuwa tunayemngojea ni mgeni wetu katika muktadha wa kiroho akili na mawazo yetu tunayaelekeza katika maandalizi ya kimwili tu: tutavaaje, tutatoka na kwenda wapi, tutakula nini nk. Ndiyo maana Sherehe kubwa kama Noeli zinaishia kuwa ni matukio kama matukio mengine ya kijamii na kukosa ladha ya kiroho.

Tunapoalikwa na Kristo kukesha inamaanisha kuanzisha mwenendo wa kiroho ambao utakufanya kukumbuka daima kwamba katika kila ulitendalo maishani mwako macho na moyo wako uelekezwe daima na kuwa tayari kukaribisha mwangaza wa kiroho kutoka kwa Mungu tunaopewa na Bwana wetu Yesu Kristo. Hii ndiyo kumweka Kristo kuwa kielelezo na kisima ambacho kwacho unachota hekima yote ya kimungu. Kurasa za Injili Takatifu zinatupatia utajiri mkubwa wa matendo ya Kristo ambaye kwa utume wake alituonesha njia ya kweli ya kuturudishia uzima na kujazwa na uwepo wa Mungu ndani mwetu. Tunapoanza safari hii ya kiroho katika Mwaka mpya wa Kanisa ni budi kujazwa na tunu za kimbingu na kuwa hai katika Kristo.

Majilio ni kipindi cha kujikumbusha tena uhai huo wa kiimani. Pengine tulichoka na mwanga wetu kufifia. Basi tusimame imara na kuzitengeneza taa zetu ili ziendelee kuangaza. Tungojee kwa matumaini kurudi kwake Bwana wetu Yesu Kristo ili atakapokuja atukute tunakesha katika sala, sadaka, na matendo yetu ya huruma. Uendelevu na uimara wa imani yetu unaonekana katika kujazwa na utajiri wa Kristo ndani mwetu. Mtume Paulo anatuambia kwamba “katika kila jambo mlitajirika katika Yeye, katika maneno yote, na maarifa yote… hata hamkupungukiwa na karama yo yote, mkikutazamia sana kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye atawathibitisha hata mwisho ili msilaumiwe siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo”. Siku hii inaitwa “parousia” yaani ujio au uwepo wa Mungu.

Kujazwa kwa neema za Kristo ndilo jambo tunalosisitiziwa katika kipindi hiki cha Majilio. Mantiki yake inajikita katika wazo lile lile la kumfanya Kristo kuwa kiini na kitovu cha maisha yetu katika safari nzima ya Mwaka huu wa kiluturujia tunaouanza leo. Ni wazi kwamba uwezo wa kungojea na tunu tunayopewa na Kristo kadiri ya Mtume Paulo. Yeye tunayemngoja ndiye anayetupatia uvumilivu na uwezo wa kukesha. Neema hizo tunazipata kwa njia ya Neno lake na katika Sakramenti hasa Sakramenti ya kitubio ambayo inatupatia neema ya utakaso na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ambamo tunampokea Kristo mzima katika maumbo ya mkate na divai na katika Sakramenti hizi tunapata utimilifu wa ahadi za mbinguni.

Kristo anakaa ndani mwetu nasi tunaungana naye. Yeye anakuwa ndiye injini ya maisha yetu. Mwaliko wa kukesha kwa ajili ya ujio wa Kristo kwetu sisi wangojeaji unatudai kujiunganisha naye. Tuianze tena safari yetu kwa furaha huku tukiutazamia ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tukeshe tukiwa hai ndani mwetu katika Yeye, kwani hatujui siku wala saa atakapokuja. Tugeuze matendo yetu na kufanya toba pale tulipoiasi imani yetu na kumsukumizia Mungu pembeni. Daima tumfanye Mungu kuwa Bwana na Kiongozi wa maisha yetu. Nawatakieni mwanzo mwema wa Mwaka mpya wa Kanisa.

Na Padre Joseph Peter Mosha.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.