2017-11-26 11:32:00

Ni kipindi cha Majilio: Fumbo la Umwilisho na Hukumu ya Mwisho!


Ndugu msikilizaji wa "Vatican News" Katika Rum. 13;11 – tunasoma hivi – mvaeni Bwana Yesu Kristu – naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini. Tunaanza kipindi cha majilio – ikiwa na maana ya matayarisho ya ujio wa Bwana, Bwana ambaye ni mwongozo na dira ya maisha yetu sisi tunaomwamini.  Mtu mmoja anaelezea maisha ya mwanadamu kama mawimbi ya bahari, ambayo hujaa na kupwa, huongezeka na kupungua. Tunapoanza tena kipindi cha majilio - Kanisa latupatia nafasi ya kuangalia safari yetu katika bahari (dunia) ili tufike katika bandari ya salama (mbingu).

Majilio ni mwanzo wa mwaka mpya wa liturijia ya kanisa. Leo tunaanza mwaka mpya wa kanisa. Tunapoanza mwaka mpya, tunatafakari ujio na kuzaliwa wa Kristo pale Betlehemu na tunaangalia yajayo – yaani Kristo atakapokuja tena. Katikati ya mihimili hii miwili – tunakuta maana ya maisha yetu kama wakristo. Kipindi cha majilio kinatupa mwanga au kioo cha kutazama tulikotoka na haja ya kutazamia kwa matumaini kule tuendako - maisha na matumaini yajayo tuliyopewa na Kristo. Huunganisha kumbukumbu zetu – tunakumbuka kuwa Mungu amekuja kwetu akakaa nasi na tunahuisha matumaini yetu – kwamba, Kristo atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu.

Kumbukumbu: tunakumbuka nini? Tunamkumbuka Yesu Kristo aliyejifanya mtu – tunatakafakari uwepo wake na maisha yake hapa duniani kama Mungu na mwanadamu –akaupa umaana uwepo wetu sisi – hadhi ya kimungu – akatuonesha maana ya maisha – Eti Mungu akawa mwanadamu. Tumshukuru Mungu. Matumaini: tunatumaini nini? Tunatumaini ujio mtakatifu aliotuahidia, jumuiya kamilifu na utu uliofungamanishwa na upendo wa Mungu. See Pope Benedict XVI ( Joseph Card. Ratzinger) ‘Seek that what is Above’ 1986 …Memory Awakens Hope. Huu muunganiko ni jambo kubwa sana; kumbukumbu na matumaini. Hii ni kumbukumbu inayoponya, inayoleta matumaini. Lengo la kanisa ni kuamsha muunganiko huu – kumbukumbu na matumaini. Katika majilio tunakumbuka matendo makuu ya Mungu na tunatumaini upendo mkuu wa Mungu.

Tendo hili linatupa nafasi ya kuingia ndani ya maisha ya fumbo hili. Katika Efe. 1:3-10 – tunasoma habari juu ya wingi wa neema isiyopimika – Mungu alituteua tuwe wake. Ni zawadi na zawadi hii inatugeuza kuwa viumbe vyake na mali yake Mungu. Maisha yetu ni safari kama ndani ya bahari. Ukitembelea mahali mara moja, mara mbili, mara tatu n.k kila mara utagundua vitu vizuri zaidi mahali hapo ambapo mara zilizotangulia hukuviona. Leo hii tunaalikwa tutumie kipindi hiki na muda huu kumtembelea Bwana tena na tena. Babati mbaya wengi wetu tunamtembelea Mungu mara chache sana na hatukai au hatubaki naye kwa muda mrefu na wa kutosha. Kwa maana hiyo hatupati nafasi ya kumfahamu vizuri na hivyo hatutaweza kuthamini huo uwepo wake. Majilio yatupa nafasi ya kukaa na kubaki na Bwana.

Tunaalikwa tuishi na kutafakari daima hekima ya Mungu – katika 1 Kor. 2,6-10 tunasoma hivi juu ya hekima ya Mungu; walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika; bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu, ambayo wenye kutawala dunia hii hawaijui hata mmoja, maana kama wangaliijua, wasingalimsulubisa Bwana wa utukufu, lakini kama ilivyoandikwa; mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.

Kukesha huku kwahitaji matumizi ya hekima ya Mungu na si ya mwanadamu ili tuongozwe daima na Roho wa Mungu. Tabia mojawapo kubwa na ya pekee ya dini ya bibilia ni mkazo wake kwenye matumaini yajayo. Tema ya matumaini ipo wazi kwenye Agano La Kale na Jipya. Ndiyo maana tunasherehekea majilio – matumaini yaliyopo na yajayo ya ufalme wa Mungu. Yeye ni tumaini letu – hii ipo wazi katika Agano Jipya. Ni nini chanzo cha matumaini haya? Ni matendo makuu ya Mungu ambayo tangu zamani za kale mwenyezi Mungu ameonesha kwetu. Kama ameshafanya haya tayari je ni kwa kiasi gani ataendelea kufanya? Kwa maana hii basi katika Majilio: matumaini na imani yanakutana tena kwa sababu sisi tunaamini.

Katika somo la kwanza – mwanzoni yaonekana ni kilio zaidi ya matumaini. Kitabu kiliandikwa wakati wa maangamizi ya Yerusalemu na matumaini ya watu yalibaki kwa Mungu tu. Mungu lakini anaonekana kuwa mbali sana na pia ahadi zake za ukombozi zaonekana kuwa mbali pia. Isaya hata hivyo anaungana na wadhambi na anaomba kwa ajili yao kwa Mungu. Isaya anamwomba Mungu hata kama wao waliona kuwa yeye ameondoa ahadi yake ya ukombozi. Hivyo kinachonekana ni kama kilio, lakini ndani yake ni maombi ya matumaini. Isaya asingekuwa na matumaini bado hakika asingeomba.

Wanateseka katika matumaini. Wewe Mungu ni Baba yetu. Sala kama hii isingeombwa kama wasingekuwa wanatambua kuwa Mungu ni Baba yao. Hata katika shida bado Mungu yupo. Mfano wa Eliya 1 Fal: 19;12 – ututafakarishe pia – Eliya anamtafuta Mungu katika kelele nyingi – kumbe Mungu anaonekana katika utulivu. La msingi hapa ni ule ufahamu wa Eliya juu ya Mungu anayeokoa na anadhamiria kumtafuta kwa hali yo yote ile. Pengine hata sisi tuko katika mazingira ya mawimbi na fujo nyingi hapa duniani. Lakini Mungu anakuja kwetu katika utukufu wake. Tumpokee.

Somo la pili linatumika leo sababu ya hali iliyopo ya kungoja, kutumaini – ufunuo wa Kristo Bwana siku za mwisho. Yeye atatuokoa na dhambi zetu na laumu zote mbele ya Baba yake. Kanisa la Korintho lilikuwa pia katika shida – hakuna amani na uelewano kati yao. Paulo anawakumbusha uwepo wa Kristo ambaye ameshatukomboa sisi. Paulo anawaambia kuwa shida yao waiweke chini ya Kristo mkombozi wao. Matumaini yao yapo kwa Kristo – atakayekuja kwetu

Katika injili – ujio huu wa Kristo uko wazi kabisa. Hapa tunaona na kuambiwa kuwa huko kungoja kwetu ni lazima kuendane na maandalizi ya kumtambua Roho mtakatifu na utayari wetu pia.  Mtakatifu Ireneo katika maandishi yake karne ya 3 ‘Dhidi ya Uzushi – Against Heresies’  anaandika hivi: akielezea kazi ya Kristo – imani ya Kikristo, inatambua kuwa Mungu ni mmoja na Yesu Kristo mwanae, Bwana wetu, ambaye vitu vyote viko chini yake. Kati ya vitu hiyo yupo mwanadmu, ambaye ni sura na mfano wake Mungu. Hivyo naye mwanadamu ni mali yake, naye Mungu asiyeonekana, akaonekana kwetu, tukamfahamu. 3,16,6;Gia’ E Ancora’ (Already and Not Yet), CCCXX, Milan, 1979, p. 268. Mwinjili Marko kama Paulo, aliandika wakati wa mahangaiko. Kanisa la Roma lilikuwa katika shida. Haikuwa ni shida iliyotoka ndani ya kanisa bali nje. Kubaki imara katika imani kulihitajika sana. Matumaini katika imani thabiti ndiyo kinga pekee iliyobaki.

Ndiyo maana mtume Marko anasisitiza maneno ya Yesu ya kukesha. Muwe macho, kesheni. Hamjui siku wala saa – walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba Mk. 13,32. Maneno hayo ni muhimu na mazito. Ndiyo yanayotufanya kweli tukeshe, tufungue macho, tutazame vizuri. Mwandishi mmoja anatukumbusha tutoke katika ulimwengu wa ndoto na tuingie katika ulimwengu wa ukweli. Katika Injili Yesu anatualika tufungue macho ya roho zetu, tuwe macho kiroho ili akija atukute tunakesha, tuko hai na si hoi. Ndiyo maana pia tunakumbushwa kufahamu vizuri hicho kinachotokea.

Katika Injili tumeona pia picha ya mtu anayechungulia mlangoni, ili amfungulie Bwana na kumkaribisha ndani. Ndivyo tunavyotakiwa nasi kufanya kipindi hiki cha majilio. Mlinda mlango anatakiwa kuwa macho na mwangalifu, mwenye subira ili amwone Bwana akija. Ni lazima kuchungulia. Mhubiri mmoja anatukumbusha – haja ya kuinua macho na kuona upeo. Tumezoea kuona mpaka mwisho wa upeo wetu. Kipindi cha majilio kinatupa nafasi ya kuinua macho juu ili kuona zaidi ya upeo wetu. Tuchungulie mbali. Bwana anakuja.

Ufahamu wa jambo linalotokea ni muhimu sana, vingenevyo hatutakesha, hatutasubiri, kwa ajili ya nini? Upo msemo kuwa mbwa pamoja na kuwa na uwezo wa kunusa mbali, lakini pia asipoona kitu chenyewe kwa kawaida habweki. Sisi tumeshamwona Bwana. Bado tunakuwa baridi? Kama kweli tunaamini alichofanya Yesu Kristo, na kama kweli tuna matumaini kwa ujio wake, ni lazima kukesha. Hivyo majilio kinakuwa ni kipindi kinachounganisha kumbukumbu na matumaini yetu. Huunganisha kumbukumbu zetu – tunakumbuka kuwa Mungu amekuja kwetu akakaa nasi na tunahuisha matumaini yetu – kwamba Kristo atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu. Uelewa huu unatusaidia kuishi kwa ushuhuda uwepo wa Mungu hapa duniani. Tusingoje mpaka siku ya mwisho. Tumshuhudie hivi sasa. Kwa kawaida katika kipindi cha majilio tunakumbuka na tunatafakari mambo makuu ambayo Mwenyezi Mungu ametutendea. Fumbo la Mungu kuja kwetu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.