2017-11-25 14:19:00

Ukarimu wetu kwa wenzetu ni kibali cha kushiriki karamu ya Ufalme wa Kristo!


Leo ni Dominika ya 34 ya Mwaka A wa Kanisa, Dominika ya mwisho katika Mwaka wa Kanisa ambapo tunapata fursa ya kumshangilia Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme. Liturujia ya Mwaka wa Kanisa imefumbatwa na utimilifu wa fumbo la Kristo ambaye ni tumilifu wa Ukombozi wetu wanadamu. Baada ya kusafiri pamoja kwa kipindi cha Mwaka mzima kuitafakari kazi hiyo ya ukombozi ya Kristo tunapata fursa ya kushangilia pamoja naye na kumpokea kama Mfalme, yaani mtawala wamaisha yetu. Ufalme wake ambao ameusimika duniani ni ufalme wa wote na kila mmoja anaalikwa kusafiri pamoja na Kristo ili kuusimika utawala wake katika maisha yake. Hapo ndipo Mungu anakuwa yote katika yote.

Sala ya utangulizi ya Sherehe ya leo inaupambanua vema ufalme wa Kristo ikisema: “Ufalme wake ni wa ukweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, upendo na amani”. Masomo yetu ya leo yanatuonesha namna ambavyo Kristo ameudhihirisha ufalme wake huo na namna gani ataudhihirisha katika siku zijazo. Kristo ameufunua ufalme wake kwa kuwa karibu nasi na kwa ukarimu wake. Yeye ni Mchungaji ambaye Nabii Ezekieli anamuelezea katika somo la kwanza. Sehemu hiyo ya maandiko matakatifu inamfunua Kristo Mfalme kama Mchungaji mwema ambaye anaonekana katika umakini wake na upendo wake kwa kondoo wake. Hivyo ufalme wake umenuia kutumiminia neema za Mungu na kuonja faraja na ukarimu wake.

Utawala huu wa Kristo unatofautiana na utawala unaonekana katika jamii ya mwanadamu leo. Viongozi wa kijamii wanakuwa ni watawala na mabwana na sio wachungaji ambao wanajitoa kwa ajili ya mema ya jamii nzima. Kuwa Kiongozi kunadai kuelekeza kundi na kufikia fanaka. Wengi wa viongozi wa kijamii wanashindwa kujivika sifa na Kristo Mfalme. Badala ya kuwa wakweli wao utawaliwa na ahadi za uongo ambazo zinalenga kujitanua matamvua yao na kuondelea kutawala: Badala ya kupalilia uzima wao wanaendelea kuwakandamiza watu wao kwa huduma duni na kuziua dhamiri zao kutokuangalia ukweli: Badala ya kuwaongoza watu katika utakatifu, yaani kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu wao wanamwondoa Mungu katikati ya jamii na kuyatukuza mawazo ya kibinadamu. Watawala hawa ambao wanapingana na Ufalme wa Kristo wanaonekana katika kuchezea haki na amani na kuusadaka upendo.

Zamani za Nabii Ezekieli Mwenyezi Mungu aliamua kuchukua jukumu la kuwachunga Kondoo yeye mwenyewe kwa sababu wale waliopewa jukumu hilo walimsaliti. Mwenyezi Mungu alisema: “Ole weo wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe…mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo” (Ezek 34:2 – 3). Watawala wabovu ni maangamizi kwa ubinadamu. Leo hii tunaona maovu mbalimbali dhidi ya ubinadamu. Utu wa mtu umegaragazwa ukiashiria watawala wamebaki katika kujinufaisha wenyewe. Kila mmoja anatafuta uongozi si manufaa ya jamii nzima ya mwanadamu bali kwa faida yake binafsi au kwa maneno mengine kwa ajili ya kuchumia tumboni kwake. Ndiyo maana tunaona jinsi ambavyo kuna matendo ya rushwa na udanganyifu mwingi nyakati za Uchaguzi, makusudi ni kuiwekea bima nafasi ya uongozi na hivyo kugeuka watala na kuwanyonya wengine badala ya kuwahudunia.

Historia ya ukombozi wa Mwanadamu inafumbatwa katika fumbo la ukombozi la Kristo. Ufalme wake unadhihirika katika mwanadamu aliyekombolewa. Hivyo mimi na wewe tunaalikwa kushiriki katika karamu ya ufalme huo kwa njia ya matendo yetu ya ukarimu kwa jirani zetu, matendo ambayo yataufunua uso wa Kristo Mfufuka kwa maskini, wanyonge na wahitaji. Mtakatifu Vincent wa Paulo, Mtume wa ukarimu kwa maskini aliongozwa na taswira hiyo, yaani kuuona uso wa Mungu katika maskini, wanyonge na wanaoteseka. Injili ya Dominika hii inatuelezea kwa uwazi kabisa kwamba Upendo wetu kwa wenzetu ndicho kigezo cha ushiriki wetu katika Ufalme wa Kristo. Kristo anawaaita hawa kuwa wamebarikiwa na Mungu kwani walilisha wenye njaa, waliwanywesha wenye kiu, waliwakaribisha wageni, waliwavisha walio uchi, waliwatunza wagonjwa na waliwatembelea waliokuwa kifungoni. Kwa wale ambao walitenda kinyume cha hawa Kristo anawaambia wazi: “Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari ibilisi na malaika zake”.

Upendo wa kushirikishana ndiyo kadi ya mwaliko kuishiriki karamu hii. Karamu ya Kristo inatutaka kila mmoja wetu kuwa tayari kufungua macho yake na kutazama nje na kuwaona wanadamu wenzake walio wahitaji na kuwakunjulia mikono yake na kuwainua, kufungua moyo wake na kuwamiminia upendo. Dominika iliyopita tumeiona hiyo haiba katika sifa ya umama. Mama katika familia ana jicho pana, moyo mkubwa na mikono isiyochoka kuhudumia. Kristo Mchungaji mwema ambaye ndiye Mfalme wetu anatualika mimi na wewe kuundeleza ufalme wake ili kwa njia ya huduma zetu za upendo kwa wenzetu tuweze kuutawaza ufalme wake katikati ya jamii ya wanadamu. Pengine tuonapo mwanadamu anateseka ni shutuma kwetu kushindwa kuwa vyombo vya kuustawisha ufalme wa Kristo.

Kristo aliouonesha upendo wake kama Mchungaji mwema na ndiyo kielelezo kwetu cha kuonesha huo upendo wa kushirikishana. Yeye ameuonesha kwa ukaribu wake kwetu na kwa ukarimu wake. Amekuja duniani kukaa pamoja nasi, ameichukua namna yetu na kuwa Emmanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Hiyo ndiyo namna tunaypoaswa kuifanya. Wokovu wetu haujikiti katika kuukiri ufalme wake kwa maneno tu bali katika kurandana na kazi zake za kumkomboa mwanadamu. Yule anayekuwa kweli mjumbe wa huruma ya Mungu ndiye anayeonesha kuukaribisha Ufalme wa Kristo kwa sababu ametoa nafasi katika nafsi yake kueneza upendo wa Mungu. Kwa ushindi wake wa kifo cha msalabani Kristo ametufunulia njia ya kushiriki katika ufalme wake. Kazi ni kwetu sisi kuukumbati msalaba na kuuishi ili kutoa harufu nzuri ya huruma ya Mungu kwa wote wanaoihitaji.

Mtume Paulo analielezea Fumbo la Pasaka kama utimilifu wa ufalme wa Kristo. Ufalme huo unajifunua pale Mungu anapokuwa yote katika wote. Kumbe Ufalme wake unanuia kuyatimiza mapenzi ya Baba yake ambaye ndiye aliyemtuma kuja kumkomboa mwanadamu. “Basi, vitu vyote vikisha kutiishwa chini yake, ndipo Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake Yeye aliye mtiishia vitu vyote”. Huyu ndiye Baba anayepaswa kubakia kuwa ni kitovu cha yote katika maisha ya mwanadamu. Mungu Baba anapofanywa kuwa kitovu cha yote sote tutatenda katika ukweli yaani kadiri ya kusudi la uumbaji na hapo ndipo inapolenga kazi nzima ya ukombozi. Hii ni kwa sababu Ukombozi unatujia baada ya anguko la mwanadamu, anguko ambalo chanzo chake ni tendo la mwanadamu kumwondoa Mungu katika maisha yake. Mwanadamu alitaka kuwa kama Mungu.

Kwa maneno mengine mwanadamu bila Mungu hawezi kufurahia uwepo wa Ufalme wa Kristo kwani kila mmoja anajitengenezea ufalme wake mwenyewe na matokeo yake ni anguko na maovu dhidi ya mwanadamu. Lakini mwanadamu anapokuwa na Mungu kama yote katika yote hapo ufalme wa Kristo unastawi na hivyo upendo, undugu, msamaha haki na amani ambavyo ni sifa mahsusi za ufalme wa Kristo vitatawala. Tuukaribishe utawala wa Kristo ili kwa nafasi zetu mbalimbali tumkomboe mwanadamu. Tawala Ee Kristo Mfalme, Tawala kwetu!!

Padre Joseph Peter Mosha.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.