2017-11-02 16:58:00

Watawa na Jamii za Maisha ya Kitume zitoe ushuhuda yakinifu katika nyanja zote


Katika wito wa kitawa wa kisekolari, ni maisha ya kila siku yanayomlea mtawa. Watawa kati ya watu, ni ushuhuda wa kuvutia na unabii wa maisha kwa ajili ya Mungu na ulimwengu. Hii ni sehemu ya Hotuba ya Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maisha ya Wakfu na Jamii za Maisha ya Kitume, siku ya Jumapili tarehe 29 Octoba 2017, wakati wa kufunga warsha kwa ajili ya watawa wa Jamii za Maisha ya Kitume nchini Italia.

Warsha kwa ajili ya watawa wa Jamii za Maisha ya Kitume nchini Italia, imefanyika kuanzia tarehe 28 – 29 Octoba 2017, jijini Roma, katika Taasisi ya Mafundisho ya Mababa wa Kanisa, Augustinianum. Maandalizi ya warsha hii yalifanyika kwa ushirikiano madhubuti kati ya Baraza la Maaskofu nchini Italia na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maihsa ya Wakfu na Jamii za Maisha ya Kitume.

Askofu mkuu Carballo anasema, kwa kuwa maisha ni sehemu ya uwepo wa Bwana, maisha hayo hayo yanapaswa kuwa ni nyenzo ya kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, ambapo maisha ya mwanadamu yanakuwa Neno wa Mungu anayeendelea kufanyika Mwili na kukaa kati ya watu. Mwenyezi Mungu ni Mungu wa historia, na hivyo imani ya mkristo ni imani ya kihistoria. Kwa misingi hiyo, maisha ya mwanadamu yanapata uthamani wake mkubwa, sio kwa sababu za kijamii, bali kwa sababu za kitaalimungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu anaishi katika maisha hayo ya mwanadamu na amekuwa akitenda kazi kati yake tangu awali, na anaendelea kufanya hivyo.

Maisha ya mkristo ni maisha ya imani katika hija isiyokoma kamwe, bali yanasonga mbele kadiri ya mpango na mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, amekuwa akionya mara kadhaa hatari ya utengano au mpasuko kati ya imani na maisha ya kila siku. Mgawanyiko huu umepelekea ugonjwa wa schizofrenia wa imani kati ya watu, sababu ya kuabudu vitu na kupoteza nafasi ya Injili ya Kristo kati ya watu. Hivyo kuna umuhimu  mkubwa wa kusimika malezi ya kiroho, kiutu, kiakili na kijamii ili kutengeneza umoja wa ndani wa mwanadamu, na kuepuka mpasuko kati ya maisha yake ya kila siku na imani anayotegemewa kuikiri na kuiishi.

Ubinafsi na mpasuko anaoutengeneza mwanadamu leo, unamfanya aitazame imani kana kwamba ni tunu binafsi tu na kuiishi katika upweke, badala ya kuishuhudia na kuiadhimisha katika jumuiya, kati ya watu. Imani inatazamwa kana kwamba ni kutafuta furaha na amani binafsi, kuhangaikia miujiza, uponyaji na mafanikio. Hizi ni tabia za wapenda vya kunyonga, sasa vya kuchinja ni kama hawaviwezi. Kwa namna hii mwanadamu anatafuta kila namna ya kukwepa mateso, mahangaiko na uchovu badala ya kujifunza namna ya kuyapokea yote kwa imani, kwani ni sehemu msingi ya maisha ya mwanadamu, katika hija yake hapa duniani.  

Watawa wa Jamii za Maisha ya Kitume wanapaswa kutolea ushuhuda yakinifu katika kila nyanja za maisha kisiasa, kijamii na kiuchumi, anasema Askofu mkuu Rodriguez Carballo. Maisha ya utawa katika udugu na jumuiya, hayapingani na maisha ya kumshuhudia Kristo katika mzunguko wa kukurukakara na purukushani zingine za maisha ya kila siku, iwapo watawa hawa wanabaki waaminifu katika Karisma yao na wito wa maisha na utume wao kwa ujumla.

Kwa sababu hiyo, ni muhimu wachungaji mapadri na watawa kwa ujumla, waweke mazingira ambapo waamini watajisikia kukaribishwa na kueleweka. Hii itakuwa ni namna ya kuwawezesha wachungaji mapadri na watawa kugundua utajiri uliopo katika makanisa mahalia na mahitaji ya watu kiroho na kimwili, na hivyo utume wao kuzaa kweli matunda yenye kudumu.

Kwa upande wake Kardinali João Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maisha ya Wakfu na Jamii za Maisha ya Kitume, wakati wa mahubiri kwenye Misa Takatiku ya kufunga warsha hiyo amesema, ni muhimu kila mmoja kuishi kwa furaha na kuuvumbua Uso wa Huruma ya Mungu, kwa kujiweka kila wakati katika shule ya Neno la Mungu. Neno la Mungu lina nguvu ya pekee na litaweza kuboresha mahusiano kati ya watu na kubadili mtazamo wa maisha. Hivyo ni muhimu kuiishi furaha katika umoja, katika jumuiya, kwani furaha ya Mungu ndani ya mwanadamu ni ushuhuda kwa wengine ya kwamba, Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kumbadili mtu na kuboresha maisha yake.

Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.