2017-10-27 17:51:00

Ziara ya Kard.F.Filoni nchini Uganda tangu tarehe 26-30 Oktoba 2017


Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Kardinali Fernando Filoni, yupo Uganda kuhitimisha maadhimisho ya miaka 50 ya Jimbo kuu la Kampala. Ni ziara yake ya kichungaji nchini humo kuanzia tarehe 26 hadi 30 Oktoba. Ijumaa tarehe 27 Oktoba atakutana na watoto na vijana wa Seminari kuu ya Ggaba, Mapadre, watawa wanawake na wakiume. Mchana atafanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri, na baadae, katika kanisa kuu la Mtakatifu Maria, atakutana na wana ndoa na kubariki makumbusho yaliyopewa jina la Papa Francis.

Jumamosi tarehe 28 Oktoba atakutana na makatekista na walimu kwenye madhabahu ya Munyonyo, mkutano ambao utafuatiwa na Misa takatifu. Mchana Kardinali Filoni atatembelea makazi ya maskini huko Kisenyi. Jumapili, Oktoba 29 kardinali Filoni ataongoza Misa takatifu kuhitimisha maadhimisho ya Jubilee ya Jimbo Kuu la Kampala katika madhabahu ya Mashahidi wa Uganda na Jumatatu tarehe 30 atarejea Roma.

Watakatifu mashahidi wa Uganda ni kundi la Watumishi 22 wa mfalme wa Buganda (sasa Uganda), waongofu wa ukatoliki kutoka kwa Wamisionari wa Afrika (White Fathers), ambao waliuawa kwa kuiungama dini ya kikristo chini ya utawala wa Mfalme Mwanga II (1884-1903) kati ya Novemba 15, 1885 na 27 Januari 1887 baada ya kukataa kubadili msimamo  wa imani yao. Walifanywa kuwa wenye heri na Papa Benedikti XV mwaka 1920 na walitawazwa kuwa watakatifu  na Papa Paulo wa sita mnamo tarehe 8 Oktoba 1964 mjini Vatican. Katika ziara yake ya kitume Afrika mwaka 1969, Papa Paulo VI aliwasimika katika madhabahu ya Namugongo.

Tarehe 7 Februari 1993, Papa Yohani Paolo II aliongoza Misa katika madhabahu ya Namugongo, wakati wa ziara yake ya kichungaji katika nchi za Benin, Uganda na Sudani. Papa Francis alipoitembelea Uganda alitambua ukuu wa mashahidi wa Uganda alipoadhimisha misa katika madhabahu ya  Namugongo tarehe 28 Novemba 2015.

Jimbo Kuu la Kampala lilianzishwa rasmi tarehe 5 Agosti, 1966. Jimbo kuu hili lina idadi ya watu 4,242,000, ambapo 1,740,000 ni wakatoliki; Parokia 63; Mapadre 288 wa jimbo na Mapadre 72 wa mashirika; waseminari 160;  Watawa wa kiume 285 na watawa wa kike 666. Jimbo linasimamia taasisi 398 za elimu na vituo 69 vya misaada.

Fr Tito Kimario 
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 
All the contents on this site are copyrighted ©.