2017-10-27 16:14:00

Tutambue ya kuwa,Upendo kwa Mungu unajifunua katika upendo kwa jirani


Mwanadamu katika asili yake ni mjamii. Mwanadamu anajifunua na kujitambua asili yake sawasawa katikati ya jamii ya mwanadamu. Katika muktadha huu ndipo tunaweza kuidhihirisha dini ya kweli. Dini ni mahusiano yetu wanadamu na Mungu wetu aliye mkuu sana. Mahusiano haya yanapata mashiko katika muunganiko wetu sisi kwa sisi na pamoja na viumbe vyote. Vitabu vitakatifu na hata mawazo ya wanafalsafa wa kale yanaudadavua uumbaji kama ufunuo wa Mungu. Upendo wetu kwa Mungu unajieleza vizuri katika upendo kwa jirani zetu na vyote vinavyotuzunguka. Leo tunawekewa mbele yetu Amri kuu ya Mpendo ambayo inajikita katika Upendo kwa Mungu na kwa jirani.

Injili ya Dominika hii inatupatia wajibu huo wa upendo ili kuidhihirisha dini ya kweli, yaani kumpenda Mungu “kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote” na katika namna iliyo sawa ni kumpenda jirani yako. Kristo anatuambia kwamba “katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii”. Hapa tunaoneshwa wazi kuwa kujishikamanisha na Mungu si jambo la kinadharia bali ni tendo halisi ambalo linapaswa kudhihirika katika maisha ya kila siku. Mungu wangu yu hai na anaishi katika nafsi ya jirani yangu. Uhai wa uhusiano wangu na Yeye unajifunua katika mahusiano chanya na mwenzangu.

Mafarisayo walifanya sehemu ya jamii ya kiyahudi ambayo ilijikinai kushika dini vizuri. Wakati wa Kristo kundi hili lilizabuliwa kibao na kukumbushwa ukweli na kumwabudu Mungu umejikita katika nini. Walikumbushwa kwamba dini ya kweli si ile ambayo ilijenga kiburi na majivuno ya kujiona upo bora kuliko wengine bali ni kujiweka katika upendo wa Mungu na kuueneza kwa watu wote ambao wanauhitaji. Hapa wanaoneshwa mantiki ya upendo wa kimungu ambao unamfanya mmoja kuikana nafsi yake na kujitoa kwa wengine na katika hatua hiyo huipata nafsi yake kwa wengine. Huo ndio mfumo mpya wa kimapinduzi ambao unautawaza ufalme wa Kristo katika jamii ya mwanadamu.

Upendo wetu kwa Mungu na kujitoa kwetu kwake kunapata mashiko katika kujitoa nafsi zetu kwa upendo mkubwa ajili ya wengine. Ni ukumbusho kwetu wa kufunua mioyo yetu na kuwajali wengine kwa kuwatakia mema kwani sote kama wanadamu tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mtume Yohana anatuasa akituambia: “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu” (1Yoh 4:12). Kabla ya kuteswa kwake Kristo alitufundisha kwa mfano upendo huu kwa jirani zetu baada ya kuwaosha miguu mitume wake na kutuagiza akisema: “Ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi (Yoh 13:14).

Upendo wetu kwa jirani unawekwa kama sharti mahsusi la kuufunua upendo wa Mungu kwetu. Mwenyezi Mungu anatupenda sote na anataka kumpatia mema kila mmoja wetu. Lakini Yeye anatutumia sisi kama mawakala wake ili kwa kwa njia ya huduma zetu kwa wenzetu wote wanauonja upendo wake. Haya yanatimilika katika kuitikia vema miito yetu mbalimbali ambayo tumekabidhiwa. Ibada yetu kwa Mungu yaani ibada ya kweli ni sadaka ya nafsi yetu ambayo tunaitoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hatuwezi kujidai kuwa tunamtumikia Mungu ili hali tunashindwa kutimiza nyajibu zetu za kawaida iwe katika familia zetu, katika jamii yetu na sehemu zetu za kazi. Mwitiko wetu chanya katika nafasi mbalimbali unaufunua upendo wa Mungu kwa wengine na kwa njia hiyo unatupatia sote matunda ya pendo lake yaani Roho Mtakatifu, ambayo ni “upendo, furaha, Amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi” (Gal 5:22 – 23).

Upendo wetu kwa jirani zetu unahitajika zaidi kwa walio dhaifu na wanyonge. Hili ndilo linafafanuliwa na maagizo wanayopewa wana wa Israeli katika somo la kwanza. Makundi haya yanatajwa kama wageni, wajane, yatima na maskini. Neno la Mungu linatuambia kwamba “ukiwatesa watu hao katika neno lolote, nao wakinililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao”. Waisraeli walionywa katika hili kwani hatari iliwanyemelea baada ya kutoka utumwani na kufika nchi ya ahadi kuingia katika jamii yenye msigano kati ya makundi ya wenye mamlaka na matajiri dhidi ya wanyonge na maskini. Makundi haya ni makundi ya wale ambao wamekwisha dhoofika kwa sababu ya ubabe na unyonyaji uliokithiri wa kijamii. Watu wa namna hii wamepoteza matumaini yao katika macho ya wanadamu na hivyo tumaini lao limebaki katika Mungu.

Jamii mamboleo ya kibinadamu inaonekana kupoteza usikivu katika neno hili. Ni jamii ambayo imetengeneza matabaka na kubariki mifumo ya “mwenye kupata apate na mwenye kukosa akose”. Ni mifumo ambayo imejikita katika ubinafsi na hivyo kuutupilia mbali ubinadamu. Tujinyooshee vidole sisi tulio katika imani ya kikristo. Pengine tunaweza kuwashutumu Mafarisayo kwa wakati wao lakini tukajisahau kujishutumu na sisi wakati huu. Kama nasi tunaoonekana kumpenda Mungu na kuiishi dini yetu tupo katikati ya jamii hii hii ambayo inapambwa na sura ya mwanadamu anayehangaika upo wapi ushuhuda wa imani yetu? Hii ni ngumu kumeza lakini ndiyo ukweli wa mambo kwamba mahali fulani mambo si shwari na tunakurupusha imani yetu.
Mimi na wewe tunaweza kuwa ni washiriki katika kuibariki mifumo hii ya kinyonyaji. Pengine hii na kwa kupitia uvivu na uzembe wetu na kutokujali kwetu kutimiza vema nyajibu zetu. Wajane, yatima, wageni na maskini wa wakati wetu wanalia kwa kukosa haki na sisi ama tumeziba masikio na macho yetu tusisikilize ama kuona au tunashiriki katika kuwapora haki yao kwa kutotenda haki katika tasnia mbalimbali zitoazo haki. Dini yetu na upendo wetu kwa Mungu upo wapi? Ni nafasi ya kugutuka na kutoka katika giza hilo. Ni wakati wa kujifunua na kuishi ukweli wa dini yetu ili kwa mifano yetu ya maisha mwanadamu aweze kuuonja upendo wa Mungu.

Tuige mfano wa Wakristo wa Thesalonike ambao waliishi Injili kwa matendo yao kiasi cha kuwa mfano kwa watu wengine. Mtume Paulo anawasifu akisema: “Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu, hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya. Maana kutoka kwenu Neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea” (1Thes 1:6 – 8). Ushuhuda wa imani yao na mapendo yao umeeneza upendo wa Mungu kiasi kwamba Mtume Paulo hakuona haja ya kuhubiri tena. Hilo ndilo ambalo tunapaswa kulionesha kwa kuishi upendo wa Mungu tunaoutangaza kwa mfano wa matendo yetu mema ili matendo hayo yamtangaze Mungu zaidi kwani “Actions speak louder than words”.

Tujivike upendo wa Mungu ambao utatupatia furaha ya milele kwa maana upendo wake mkuu wadumu milele. Tuueneze upendo huo tunaouonja ili kwa mfano wa maisha yetu ya upendo kwa jirani zetu wanadamu wote waushuhudie na kuuonja upendo wa Mungu. Mwenyeheri Maria Cocifissa Curcio daima aliwasisitizia watawa wenzake kwamba “upendo mnaouchota katika Ekaristi muueneze ulimwenguni kote”. Huo ndiyo wajibu wa kimisionari tunaopatiwa leo hii. Daima tukumbuke kwamba upendo wa Mungu si mali binafsi bali unajidhihirisha katika upendo wetu kwa jirani zetu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.