2017-10-25 16:29:00

Ask.Galantino:Ubora wa elimu unaotolewa na Kanisa unapendwa na wazazi


Husikika ikisemekana kwamba uwepo wa shule za binafsi, yaani zisizomilikiwa na kuendeshwa na serikali, husaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za serikali katika bajeti za kila mwaka. Maneno haya yameutikisa ukumbi wa Cenacolo katika bunge la Italia, yalipotamkwa na Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini Italia, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya 19 ya Elimu Katoliki nchini humo. 

Askofu Galantino anasema, umuhimu wa uwepo wa shule zisizo za serikali, unaonekana zaidi katika thamani na ubora wa elimu ndani ya taifa husika kuliko kufikiria unafuu wa gharama kwa serikali; na kwa hakika litakuwa ni jambo la kusikitisha sana iwapo serikali itaruhusu shule zisizo za serikali kwa sababu tu ya kukwepa gharama katika bajeti yake, kwa sababu kuna tunu za msingi na muhimu zaidi ya gharama.

Kwanza kabisa kuna haki na uhuru wa wazazi kuchagua shule wanayoona wao kuwa inafaa zaidi kwa kuwalea na kuwaelimisha watoto wao. Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake ya Kitume, Amoris laetitia, yaani Furaha ya Upendo ndani ya Familia anasisitiza jambo la haki na uhuru huu kwamba: ni wajibu mkubwa wa wazazi kuwalea watoto wao, na wakati huo huo ni haki yao. Hivyo wazazi wasiutazame wajibu huu kana kwamba ni mzigo, bali ni haki msingi ambayo wanapaswa kuitetea siku zote isijekuondolewa kwao na mtu yeyote, hata ikiwa ni serikali. Serikali na taasisi zingine za elimu, hushiriki katika malezi na elimu ya watoto na wanapaswa kuheshimu uhuru wa wazazi katika kuchagua shule ambazo wazazi wanapendelea kulea na kuelimisha watoto wao. Hivyo wazazi wasiwekewe masharti magumu kisiasa, kiuchumi au kisheria kiasi cha kushindwa kufaidi haki yao hiyo msingi.

Shule na hata taasisi za elimu ya juu zisizo za serikali zisionekane kana kwamba ni maadui au washindani kwa zile ambazo ni za serikali, anasema Askofu Galantino. Ikumbukwe kwamba elimu shuleni au katika taasisi za elimu na ufundi, ni washiriki wa huduma katika kulea na kukuza watoto na vijana wa familia mbali mbali ambao ndio haswa wajenzi wa taifa la kesho. Hivyo serikali inapaswa kuzingatia Katiba ya nchi na kuweka sheria kanuni zinazowezesha mashule na taasisi kutekeleza huduma ya elimu kwa uhuru, katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na ufundishaji, mbinu, mipango na tunu msingi. Serikali iweke utaratibu wa kiwango fulani cha kawaida ambacho shule na taasisi zote za elimu na ufundi zitapaswa kuzingatia, lakini zisiwe taratibu ambazo zinawabana sana au kuwa mzigo kwa wamiliki na waendeshaji, au hata kwa wanafunzi na wana vyuo.


Kamati ya Elimu Katoliki nchini Italia imetoa waraka unaoonesha jinsi gani mabadiliko ya utaratibu wa umiliki na uendeshaji wa shule na taasisi za elimu nchini humo zimekuwa za maneno zaidi bila utekelezaji madhubuti, na hivyo kukwamisha malengo ya mafanikio makubwa zaidi ambayo yangeweza kufikiwa na shule zisizo za serikali. Mfano uhuru wa shule na taasisi hizo ni mdogo sana, usawa wa elimu kisheria bila usawa kiuchumi, uhuru wa kuchagua mfumo wa elimu, namna ya kuwahangaikia watoto walio katika mazingira magumu na maandalizi mazuri ya waalimu na wakufunzi. Hata hivyo, Kamati ya Elimu Katoliki nchini Italia, inatambua bidii zilizowekwa na Kanisa kuhakikisha elimu inayotolewa katika shule na taasisi za Kanisa inakuwa bora.

Askofu Galantino anasema kwamba, anajisikia fahali kwa niaba ya Kanisa, kwa kuwa shule na taasisi za Kanisa hazibagui vijana wa kuelimisha. Kanisa linaelimisha wote bila kujali sura, kabila, dini wala rangi. Lengo la Kanisa ni kutoa huduma ya elimu iliyo na ubora mkubwa, kiasi kwamba vijana hao wanapomaliza kipindi cha maandalizi kielimu na kuingia katika uwanja wa huduma kitaifa na kimataifa, waweze kuwa kweli wenye mchango mkubwa katika maendeleo ya binadamu, kimwili na kiroho. 

Ubora wa elimu unaotolewa na Kanisa, unadhihilishwa wazi na wingi wa wazazi wanaopenda kupeleka vijana wao katika shule na taasisi za Kanisa, hata inapowalazimu wazazi kujibana sana kiuchumi ili kufanikisha nia yao hiyo. Kwa sababu hiyo, anasisitiza Askofu Galantino, haki na uhuru wa wazazi kuchagua mfumo wa elimu, vinapaswa kupewa kipaumbele na kutetewa kikatiba na katika utendaji, siyo kwa maneno matupu yasiyovunja mfupa.

Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.