2017-10-20 09:14:00

Katika yote, Mwenyezi Mungu apewe: sifa, utukufu, heshima na ukuu!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, katika Zaburi tunaimba “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake (Zab 24:1)”. Ni utambulisho wa nafasi ya Mungu katika kazi yake ya uumbaji. Yeye ni muumba wa vyote na anaviweka vyote katika mwongozo wake. Ulimwengu wote na vyote vilivyomo haviwezi kuukimbia mkono wa Mungu au kujificha mbele za uso wake. Yeye anajua njia zetu zote na anao uwezo wa kutuelekeza wote kadiri ya mapenzi yake. Hii inamaanisha kuwa watu wote bila kujali kwamba wanamjua Mungu au wanamkiri wanajulikana mbele za Mungu na wanayo chapa ya Mungu. Wakati wa uumbaji Mungu alisema: “Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu” (Mw 1:26).

Somo la kwanza la Dominika hii linatufunulia hilo na kuonesha urefu wa mkono wa Mungu. Mungu anamuinua Koreshi kutoka katika taifa ambalo katika mazingira na wakati wake walionekana kutomjua Mungu wa kweli, Mungu aliyeabudiwa katika Israeli. Mtu huyu mpagani anawekwa kama masiha wake kwa ajili ya kuwakomboa watu wake: “Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake.” Mungu anaweka wazi kabisa kwamba Koreshi hakumjua akisema: “Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua”.

Ukuu huu wa Mungu kwa Koreshi machoni pa mataifa ni uthibitisho wa utendaji wake kwa yeyote anayemtaka kwani ana hakika watu wote wamewekewa chapa ya sura yake. Huu ni ufunuo kwa hadhi ya mwanadamu ambayo inampambanua kati ya viumbe vyote. Yeye amepewa akili na utashi ili kuuratibisha na kuufanya ulimwengu kuendelea kuwa mzuri. Kazi yake inaufunua utukufu kwa Mungu pale inaporandana na mipango ya mwenyezi Mungu. Inatosha tu kwa mwanadamu kuitikia na kumpatia Mungu nafasi yake inayostahili. Yeye ni “Bwana wala hapana mwingine”. Ni wito kwetu kutojisumbua na kuanza kutafuta miungu wengine na kumwacha Yeye aliyetuumba na ambaye ametuwekea chapa yake nafsini mwetu.

Dunia mamboleo inayojipambanua katika usekulari inaupora ukuu wa Mungu. Mwanadamu anageuzwa kuwa bwana na mmiliki wa ulimwengu. Chapa ya utu inaondolewa katika mwanadamu na hivyo kinachotukuzwa ni pesa na mali za kidunia. Ni jamii ambayo haiuoni tena utu wa mtu kwa sababu imepoteza ladha ya Mungu. Hadhi ya mtu inahesabika katika yale ambaye anayamiliki. Wasio na mali wanabaki kutumika kama bidhaa na vyombo vya kuendelea kuwaneemesha wachache. Jamii hii inajipambanua katika sera na taratibu zake ambazo haziulindi utu wa mtu bali ni kulinda mali na utajiri wa wachache. Hivyo shughuli zote za kijamii na kisiasa zinaongozwa na mungu-mali.

Taratibu na mienendo hii yote inamwelekeza mwanadamu katika kuutii ukweli bandia, ukweli ambao unaondoa hadhi na asili ya mwanadamu na kwa dhahiri inatupeleka katika anguko la mwanadamu. Angalia leo hii jinsi jamii ilivyoigaragaza tunu ya familia. Mwanadamu amejivika upendo bandia na kujikinai kuunda familia katika uhuru bila kujali Amri na maongozi ya Mungu. Matokeo ya familia hizi zinazoundwa na upendo bandia ni maovu mbalimbali za kibinadamu, maovu ambayo yanaiondoa kabisa hadhi yake. Leo hii tunashuhudia mauaji ndani ya familia, tunaona talaka nyingi zinatolewa kwa sababu tu mwanadamu anaukosa upendo wa Mungu ambao ni upendo unaodumu milele. Kwa njia ya upendo huo mwanadamu anajifunza uvumilivu, msamaha, huruma, kushirikiana na tunu nyingi za kikristo ambazo ni msingi kwa familia bora.

Leo tunakumbushwa kuihusha hiyo sura ya Mungu na kumrudishia mwanadamu hadhi yake. Huu ndiyo utume wa Kanisa ambao Kristo ametuachia, yaani kumkomboa mwanadamu. Mwenyezi Mungu anakuita wewe kila wakati na kila mahali hata kama unaziba masikio yako kusudi uende ukawe sababu ya kuwa wokovu kwa wanadamu. “Nimekuweka uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia” (Mdo 13:47). Koreshi aliitikia wito wa Mungu na akawa sababu ya wokovu kwa wana wa Israeli kutoka utumwani Babeli. Sisi nasi katika ubatizo wetu tunarudishiwa hadhi yetu na kuwa na nuru ndani mwetu, nuru ambayo inapaswa kutuongoza ili kumkomboa mwanadamu. Ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kuiweka hai nuru hiyo ambayo ni Kristo Yesu katika shughuli zetu mbalimbali na hivyo kuwa sababu ya mapinduzi katika utendaji wetu, mapinduzi kutoka sura bandia ya utu wetu na kuelekea katika sura halisi ya utu wetu.

Katika somo la Injili, Kristo Yesu anatusisitizia kumpatia Mungu yaliyo yake na Kaisari yaliyo yake. “Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu” (Mt 22:21). Hapa ni kutukumbusha kwamba tunapaswa kuzitii mamlaka za kibinadamu na kama anavyotukumbusha tena Mtakatifu Paulo akisema: “kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu” (Rum 13:1). Mamlaka zote zinapata kibali toka kwa Mungu pale tu zinapotenda kadiri ya ukweli wa Injili. Hii inamaanisha kwamba, asili yake toka kwa Mungu inamsukuma aliye katika madaraka kumpatia Mungu nafasi inayostahili. Ndiyo maana Kristo anakazia katika jibu lake kwamba pamoja na kumpatia heshima yake huyu aliye katika madaraka usisahau kumpatia Mungu aliye Bwana wa wote, yaani wewe na huyo anayekuongoza nafasi yake. Mwenyezi Mungu anapatiwa nafasi yake katika ukweli.

Mwaliko wa Kristo ni kumpatia kila mmoja kile ambacho kimeweka chapa yake katika sarafu. Hivyo kwa Kaisari mpatie sarafu yake kwani ina chapa yake ambayo inaonesha mamlaka yake na anaweza kuidai jinsi atakavyo. Mwenyezi Mungu anataka umpatie ukweli ambao umejificha katika nafsi ya mwanadamu aliumbwa kwa sura na mfano wake. Taratibu na mienendo inajaribu kuifuta na kuindoa sura ya Mungu katika mwanadamu na matokeo yake hatumpatii Mungu nafsi zetu bali tunawapatia wanadamu. Tunastuliwa katika Dominika hii kuenenda katika ukweli. Mamlaka za kidunia zipo kwa ajili ya kuweka utaratibu na uelewano katika jamii lakini kamwe taratibu hizo au mamlaka hizo zisiipuuzie nafasi ya Mungu.

Mtume Paulo anatukumbusha ukweli huo kwa kutuambia kwamba sisi tu wateule wa Mungu. Hakuna mwanadamu anayejileta bali wote tunakuja kwa uchaguzi na makusudi ya Mungu. “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yer 1:5). Hivyo Paulo anatuhasa  kutousahau ukweli huo na kutambua kwamba “Injili haikutufikia kwa maneno tu, bali katika Nguvu, na katika Roho Mtakatifu”. Ni wajibu wetu kujitarisha na uwepo wa Roho Mtakatifu ili kutembea daima katika kweli na kuutangaza ukweli. Hii inafanyika kwa njia ya sala na tafakari za kiroho. Daima tujijaze elimu za kimungu ili kujiwekea hakika ya kutembea katika njia ya ukweli na kuuthibitisha ukuu wa Mungu kwa watu wote. Leo tunaalikwa kumpatia Mungu yaliyo yake, yaani kuondokana na kumtukuza mwanadamu na miungu yake katika ulimwengu ulio mali ya Mungu na kuuweka uwepo wa Mungu Bwana wetu aliye asili ya mema yote.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.