2017-10-19 09:00:00

Mfuko wa Joseph Ratzinger-Benedikto XVI katika kukuza tafiti duniani


Padre Federico Lombardi, SJ., Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, hivi karibuni amewasilisha matukio makuu yanayotarajiwa kutekelezwa na Mfuko huu kwa siku za hivi karibuni, yakiwa na mwelekeo wa kiekumene kama sehemu ya mchakato wa Kanisa kukuza na kudumisha majadiliano na Makanisa ya Kikristo katika uwanja wa taalimungu. Mkazo pia umewekwa katika tafiti za muziki kama njia ya mawasiliano.

Akitangaza washindi wa Tuzo ya awamu ya VIII ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni amesema, tuzo hii itatolewa rasmi kwa washindi hapo tarehe 18 Novemba 2017. Washindi wa mwaka huu ni Theodor Dieter, mwanataalimungu kutoka Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani na Mkurugenzi mkuu wa kituo cha tafiti za kiekumene cha Strasburg; Karl Heinz Menke, mwanataalimungu wa Kikatoliki, mwanachama wa Tume ya Kitaalimungu kimataifa pamoja na Arvo Pàrt, mtunzi wa muziki mtakatifu kutoka katika Kanisa la Kiorthodox.

Kardinali Gianfranco Ravasi anasema, lengo la Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI ni kuendeleza mawazo ya kitaalimungu yaliyofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake, mambo ambayo kwa hakika ni amana na utajiri mkubwa kwa ajili ya utume wa Kanisa ulimwenguni. Watafiti hawa wanawasaidia watu kuzama na hatimaye, kufahamu utajiri unaofumbatwa katika mawazo ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, katika uhalisia wa maisha ya watu. Tuzo ya mwaka huu inatoa mwelekeo mpana zaidi kwa kutaka kufahamu mawazo ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika ulimwengu wa sanaa unaowahamasisha watu kuzama zaidi kwa kujikita katika maswali msingi!

Hili ni kama dirisha wazi linalowaelekeza watu kuwa na upeo mpana zaidi katika maisha! Arvo Pàrt, mtunzi wa muziki mtakatifu kutoka katika Kanisa la Kiorthodox ni kati ya magwiji waliojielekeza zaidi katika tafiti za muziki mtakatifu, kwa kuunganisha utajiri kutoka katika Mapokeo ya Muziki wa Kilatini, mambo msingi ya kuzingatia na umuhimu wa muziki unaowashirikisha waimbaji wengi, ikilinganishwa na muziki unaoimbwa na mtu mmoja. Hii ni njia mbadala katika masuala ya kitaalimungu, ingawa bado tafiti za kitaalimungu zinapewa kipaumbele cha kwanza na Mfuko huu.

Kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI na Chuo Kikuu Cha Francisco di Vittoria, hasa katika masuala ya tafiti ya “mawazo wazi”. Washindi wamepewa tuzo yao, hapo tarehe 27 Septemba 2017 kwenye Makao makuu ya Taasisi ya Kipapa ya Sayansi. Kwa upande wa tafiti za kisayansi, tuzo imetolewa kwa Darcia Narvaez, kutoka Chuo Kikuu cha Notre Dame, kilichoko nchini Marekani, kwa kujikita katika maendeleo ya kanuni maadili na utu wema katika tafiti. Wengine ni Claudia na Juan Franck kutoka Chuo Kikuu cha Austral, Buenos Aires, Argentina. Katika masuala ya kifalsafa, tuzo imetolewa kwa majaalimu wa falsafa kutoka Chuo kikuu cha Loyola, kilichoko Chicago, nchini Marekani, kwa kujikita katika malezi na majiundo makini ya utunzaji wa ekolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu. Sr. Sarolta Laura Baritx, anayefundisha huko Budapest, Hungaria, amejielekeza zaidi katika ufundishaji wa uchumi mintarafu kanuni za Kikristo katika masuala ya kiuchumi kama zinavyofafanuliwa kwenye Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI unatarajiwa kuhitimisha shughuli zake kuu kwa mwaka 2017 kwa kuadhimisha Kongamano la VII ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Costa Rica, kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama unavyochambuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Huu ni mradi unaopania kuchambua kwa kina na mapana changamoto ya utunzaji bora wa mazingira na maendeleo yake katika medani za kimataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.