2017-10-19 15:00:00

Majadiliano ya kidini yanapania kudumisha: haki, amani na maridhiano


Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali ni nyenzo msingi ya kupambana na tabia ya ubinafsi, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na maridhiano kati ya watu, kila mtu akipewa nafasi ya kushuhudia imani yake! Kumbe, katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Wakristo wanapaswa kumuungama Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chanzo cha imani, furaha na matumaini ya waja wake. Mwenyezi Mungu ni kiini cha majadiliano na watu wake na kamwe hajaacha kuzungumza na wanawadamu katika safari ya maisha yao hapa duniani, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale hata leo hii, Mwenyezi Mungu anazungumza na binadamu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele, aliyetumwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Haya ni mafundisho makuu yaliyotolewa na Kardinali Jean Louis Tauran, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini wakati wa kufungua Mwaka wa Masomo 2017-2018 kwenye Taasisi ya Taalimungu ya Assisi, iliyoko Umbria, nchini Italia. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, neno majadiliano lilianza kutumiwa na Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka wake wa kicgungaji “Ecclesiam suam” yaani “Kanisa la Kristo” kwa kuonesha kwamba, kazi ya ukombozi inayotekelezwa na Mwenyezi Mungu kadiri ya mpango wake wa daima inafumbatwa katika majadiliano, changamoto kwa Mama Kanisa kujikita katika majadiliano na watu wa Mungu.

Mwenyezi Mungu ameamua kujifunua kwa watu wake kwa njia ya majadiliano. Kumbe, huu ni utume unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kujikita katika ufunuo wa huruma ya Mungu unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kristo Yesu, utimilifu wa ufunuo wa Mungu kadiri ya Mafundisho ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alikazia umuhimu wa majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali duniani kama njia ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Kunako mwaka 1986 akizungumza na wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican alikazia: umoja, udugu na mshikamano wa familia ya Mungu, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wote hawa wamekombolewa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Pili, alifafanua tofauti zinazojitokeza kati ya watu wa Mungu mintarafu: historia, tamaduni na mahali wanapotoka watu hawa, mwaliko kwa wakristo kuheshimu ile mbegu ya Neno la Mungu iliyopandwa na kukita mizizi yake katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Ndiyo maana, Mama Kanisa bado anahamasishwa kujizatiti kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, ili wote waweze kupata wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Huu ndio utume wa Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo wa kuhakikisha kwamba, anashuhudia kwamba, tofauti zinazojitokeza kati ya watu ni utajiri unaomwelekea Mwenyezi Mungu na kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wa Mataifa, kiungo muhimu cha umoja kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu. Katika muktadha huu, majadiliano ya kidini inakuwa ni fursa makini kwa waamini wa dini mbali mbali kutangaza na kushuhudia imani yao.

Leo hii, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, waamini wa dini mbali mbali wanakabiliwa na changamoto kuu tatu: Mosi, Utambulisho wa dini yao; nani ni Mungu wao na ushuhuda wa maisha mintarafu kile wanacho kiamini katika maisha. Pili ni changamoto pia ya kuheshimu watu wenye imani tofauti kwa kutambua kwamba, hawa si adui bali ni wanandani wa hija ya maisha kuelekea katika ukweli. Tatu ni changamoto ya ukweli katika imani wanayoungama na kuishuhudia. Yote haya yakizingatiwa kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini, hakuna sababu ya vita vya kidini, nyanyaso na dhuluma kwa misingi ya kiimani kama inavyoshuhudiwa kwa sasa sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Jean Louis Tauran anasema, Mapinduzi ya Ufaransa ya Mwaka 1789 yaliunda Jamii inayosimikwa katika dhana ya ukanimungu na matokeo yake, mifumo ya kisiasa iliyoibuka wakati huo na kuendelea ikajijenga katika mchakato wa kumwondoa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu. Dini inaokena kuwa ni jambo binafsi ambalo halihitaji ushuhuda wa hadhara. Haya ndiyo mahangaiko ambayo yanaendelea kuwakumba watu wanaoishi Barani Ulaya, kwani dhana ya ukanimungu imeingia kwa nguvu sana. Changamoto ya kutaka Mwenyezi Mungu apewe heshima katika maisha ya hadhara ni dhana iliyoibuliwa na waamini wa dini ya Kiislam, waliotaka wapewe mahali pa kujenga Misikiti ili kumwabudu Mwenyezi Mungu; kwa kuheshimu Ibada zao pamoja na kushuhudia uwepo wa Mungu kati yao. Baadhi ya waamini wakatumia fursa hii kujenga dhana ya kulipiza kisasi na hapo dini ikaanza kutumiwa si kwa ajili ya kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu, bali vita na utengano kati ya waamini na “kafiri”.

Kumbe, majadiliano ya kidini ni fursa ya kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani inayoheshimu tofauti-msingi kama utajiri na changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu kati ya watu wa Mungu. Majadiliano ya kidini hayana budi kusimikwa katika ukweli na uwazi; kwa kutambua na kuthamini utambulisho wa maisha ya kiroho sanjari na kudumisha katekesi makini ya kila mwamini katika dini yake bila ya kutaka kufanya wongofu shuruti. Majadiliano ya kidini ni fursa muhimu sana kwa waamini kuweza kutangaza na kushuhudia imani yao; kwa kuheshimu na kuthamini uwepo wa dini za watu wengine ndani ya jamii na kuwaelekeza katika hija inayowapeleka kwa Mwenyezi Mungu asili ya wema na utakatifu wote.

Majadiliano ya kidini ni sehemu muhimu sana inayoweza kuwasaidia waamini kufahamu imani yao kwa dhati, ili kuweza kuitangaza na kuishuhudia, vinginevyo hapa ni shughuli pevu kabisa, kwani badala ya amani na utulivu, watu watakuwa na woga, mashaka na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wasiwe na woga wa kutangaza na kushuhudia imani kwa watu wa Mataifa, huu ni utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho anahitimisha hotuba yake Kardinali Jean Louis Tauran, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini wakati wa kufungua Mwaka wa Masomo 2017-2018 kwenye Taasisi ya Taalimungu ya Assisi, iliyoko Umbria, nchini Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.