2017-10-18 08:16:00

Maaskofu: Upendo na ukarimu kwa mahujaji wanaoelekea katika hija!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, hivi karibuni yamechapisha Waraka wa kichungaji kuhusu: Hifadhi na Ukarimu kuelekea Njia ya Santiago de Compostela kama kielelezo makini cha ukarimu wa Kikristo. Hii ni njia ambayo mahujaji wengi wanaitumia kwenda Hispania, lakini kwa kupitia nchini Ufaransa. Maaskofu wanapenda kuwahamisha waamimi pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa upendo, ukarimu na utu wema kwa mahujaji wanaoelekea katika Njia ya Compostela.

Maaskofu kwanza kabisa wanakazia umuhimu wa kujenga na kudumisha ukarimu, kwa kuwapokea na kuwahudumia wageni na mahujaji katika hija yao. Kama waamini wanapaswa kutoa na kuonesha ukarimu bila kudai malipo; kwa chakula, kikombe cha maji baridi na mahali safi pa kulaza kichwa! Pale inapowezekana, waoneshe fadhila kwa kuwasaidia waamini wenye kipato kidogo kuweza kutekeleza ndoto ya kufanya hija kwenye Madhabahu ya Santiago de Compostela. Wawafariji na kuwatia shime kwa maneno ya Injili.

Maaskofu wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutangaza na kushuhudia Injili ya Ukarimu, kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Lengo ni kuwasaidia waamini wanaoishi katika Njia ya Santiago de Compostela ambayo mahujaji wengi wanaitumia kwa miguu kama njia ya kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kujitakasa na dhambi zao, tayari kuomba na kuambata neema na baraka za Mwenyezi Mungu, kutekeleza dhamana hii kama sehemu ya maisha na utume wao wa Kikristo. Waamini hawa wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya imani kwa Kristo na Kanisa lake; alama wazi ya ukarimu na upendo wa Kikristo.

Nyumba zao ziwe na alama ya Msalaba, kielelezo cha hekima, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Waweke katika makazi yao, picha au sanamu ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, Biblia Takatifu na pale panapowezekana waweke pia Nyaraka mbali mbali za Khalifa wa Mtakatifu Petro, zilizotolewa hivi karibuni! Wawaoneshe mahujaji maeneo wanayoweza kutembelea wanapokuwa katika safari yao, ili kuboresha maisha yao ya kiroho wanapokuwa njiani kuelekea Santiago de Compostela. Wawasaidie mahujaji kuweza kupata habari kuhusu maadhimisho ya matukio mbali mbali ya Kikanisa pamoja muda wa Ibada, ili kweli hija yao iweze kurutubishwa kwa mambo msingi ya maisha ya kiroho!.

Maaskofu wanakaza kusema, Ukarimu wa Kikristo unapaswa kuoneshwa hata katika nyumba za mashirika ya kitawa na kazi za kitume, kwa kutenga watawa maalum wanaoweza kusaidia kuwapokea na kuwahudumia mahujaji katika safari yao. Watawa hawa watengwe kwa kazi hii malum, ili waweze kuwa tayari kuwapokea wageni wakati wowote wanapobisha hodi malangoni pao, kama alama ya kumpokea Kristo Yesu anayepita kati yao, akitaka kujipumzisha kama ilivyokuwa kwenye Familia ya Maria, Martha na Lazaro.

Maaskofu wanaendelea kufafanua kwamba, maeneo ya ukarimu wa Kikristo ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa! Hapa ni mahali panapowawezesha waamini kukutana na Mwenyezi Mungu katika safari ya maisha yao, ili kuweza kujipatia mambo msingi katika maisha. Maaskofu Katoliki kutoka Ufaransa na Hispania wamekuwa wakikutana mara kwa mara ili kuimarisha mwono na mwelekeo wa maisha ya kiroho kwa ajili ya mahujaji wanaotaka kufanya hija ya maisha ya kiroho na kiimani kwenye Madhabahu ya Santiago de Compostela, huko Hispania. Huu ni mkakati wa shughuli za kichungaji unaotekelezwa na Maaskofu kutoka Ufaransa na Hispania kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaofanywa kwa njia ya hija za maisha ya kiroho na kiimani kwa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.