2017-10-17 09:53:00

Jengeni utamaduni wa kuvumiliana, kuheshimiana na kuthaminiana!


Wahindu na Wakristo wanahamasishwa kwenda mbali zaidi na dhana ya uvumilivu: ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku kuu ya Deepavali kwa waamini wa dini ya Kihindu duniani, inayoadhimishwa hapo tarehe 19 Oktoba 2017. Hii ni siku kuu ya mwanga inayopaswa kuangaza akili na maisha ya waamini, ili kuwaletea furaha mioyoni na majumbani mwao, ili kuimarisha familia na jamii katika ujumla wake na kushukuru kwa mema yote yanayotendeka kuwazunguka. Changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo ni ukosefu wa maridhiano hali inayopelekea vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Wahindu na Wakristo wanaweza kukuza na kudumisha heshima kati yao na kwenda mbali na dhana ya uvumilivu, ili kufurahia amani na utulivu kwa kila jamii.

Uvumilivu unawawezesha waamini kujenga moyo wa uwazi na maridhiano kwa kutambua uwepo wa watu wengine kati yao! Lakini, ikiwa kama waamini wanataka kujenga na kudumisha amani na utulivu, uvumilivu peke yake hautoshi kabisa. Kumbe, kuna haja kuheshimiana na kutambua utofauti wa tamaduni, mila na desturi za watu katika jamii zao, ili kujenga na kuimarisha umoja katika jamii. Heshima kwa watu wengine ni jambo muhimu sana katika kukuza mchakato wa uvumilivu, kwani, husaidia kuthamini utu wa binadamu, dhana inayopaswa kuvaliwa njuga na jamii, ili kuheshimu tofauti zinazojitokeza kijamii, kitamaduni na kidini mintarafu mapokeo na utekelezaji wake kwa vitendo. Heshima hii inajielekeza zaidi katika kutambua na kuthamini haki ya uhai wa binadamu na uhuru wa kuabudu dini ambayo mtu anaitaka mwenyewe!

Njia inayohimizwa hapa ni kwa waamini wa dini hizi mbili kuhakikisha kwamba, wanaheshimiana na kulindana ili kudumisha amani na utulivu. Tabia ya kuheshimiana inatoa mwanya kwa watu wote, kiasi cha watu kujisikia wako nyumbani, badala ya watu kugawanyika na kutengana. Uvumilivu huwawezesha watu kuona tofauti zao kama alama ya utajiri unaofumbatwa katika familia moja ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, utofauti si tishio, bali ni chanzo cha kutajirisha. Viongozi wa kidini wanapaswa kuonesha ujasiri wa kupokea tofauti mbali mbali zinazojitokeza katika maisha yao: kidini na kitamaduni na kwamba, wale waliotofauti na wao, kamwe wasionekane kuwa kama adui, bali wawakaribishe na kuwaona kuwa ni mwaandani wa safari na kwamba, kila mmoja wao anao wema ambao pia ni kwa ajili ya wote.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linawaalika waamini wa dini hizi mbili kujikita katika uvumilivu kwa kuheshimu watu binafsi na jumuiya katika ujumla wake, kwani kila binadamu anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Kwa njia hii, waamini wote wanahamasishwa kujenga utamaduni wa kuheshimiana, kwa kutafuta suluhu ya amani katika vita na kinzani ili kujenga maisha yenye utulivu. Kwa kuzingatia mapokeo ya maisha ya kiroho na umuhimu wa kujenga na kudumisha amani na ustawi kwa wote; Wakristo na Wahindu kwa kushirikiana na waamini wa dini mbali mbali duniani pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kujenga utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana.

Dhana hii inaweza kukuzwa na kudumishwa kwa njia ya za mawasiliano ya kijamii, ili kwenda mbali zaidi na dhana ya uvumilivu, ili hatimaye, kujenga jamii inayosimikwa katika amani na utulivu; kwa kuheshimiana na kuthaminiana na kwamba, watu wote wanahimizwa kuchangia mchakato wa ujenzi wa umoja wa familia, kwa kila mtu kushiriki kadiri ya uwezo wake. Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini na Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, MCCJ wanawatakia waamini wote wa Kihindu Siku kuu Njema Deepavali, yaani Siku kuu ya Mwanga.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.