2017-10-16 12:10:00

Yaliyojiri: Watakatifu, Sinodi ya Maaskofu wa Amazoni & Umaskini!


Maisha ya Kikristo ni historia inayofumbatwa na huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, changamoto kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanaitikia mwaliko wa Bwana harusi ili kuweza kushiriki karamu yake, kama walivyofanya watakatifu wapya 35 waliotangazwa na Mama Kanisa, tarehe 15 Oktoba 2017, Jumapili ya XXVIII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Amerika ya Kusini yatafanyika mwezi Oktoba, 2019 hapa mjini Roma, ili kuibua mbinu mkakati mpya wa uinjilishaji kwa ajili ya sehemu hii ya watu wa Mungu, hasa zaidi, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa watu mahalia, ambao wakati mwingine wanasahaulika katika vipaumbele vya maendeleo endelevu ya binadamu.

Lengo jingine ni kuendeleza utunzaji bora wa mazingira kwenye misitu ya Amazoni, ambayo ina umuhimu wa pekee sana duniani, ili kwa pamoja, watu wote wa Mungu waweze kumwimbia utenzi wa sifa na shukrani kwa kuwaangazia njia ya haki na amani! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu kusimama kidete ili kutambua, kupambana na kung’oa vyanzo vyote vya umaskini duniani, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha Siku ya Kupambana na Umaskini Duniani kwa Mwaka 2017. Watakatifu wapya waliotangazwa na Mama Kanisa, ni mashuhuda wa imani 30 kutoka nchini Brazil, 3 kutoka Mexico na mapadre wawili kutoka Barani Ulaya. Wote hawa Mwenyezi Mungu anapenda kuadhimisha karamu ya upendo pamoja nao, daima wakiwa makini katika kutekeleza amri na utashi wake, kwani bila upendo, maisha na utume wa Kikristo unakuwa ni tasa hauna mashiko wala mvuto! 

Haya ni kati ya mambo msingi yaliyohimizwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwatangaza watakatifu wapya, ambao wanalipamba Kanisa kutokana na ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni watu ambao hawakujishikamanisha kwa kutaka usalama wa maisha yao, kwa kujitafuta wenyewe au raha ya maisha kwa kujifungia katika ubinafsi wao! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujishikamanisha na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani! Waamini na watu wenye mapenzi mema, wawe tayari kujibu ukatili wa walimwengu na ukosefu wa haki msingi kwa njia upendo mkuu. Mwamini anaweza kushinda ubaya kwa kutenda wema.

Ni wajibu na dhamana ya waamini kuhakikisha kwamba, wanalitunza vazi la harusi walilovikwa siku ile walipokuwa wanapokea Sakramenti ya Ubatizo, ndiyo neema ya utakaso inayopaswa kuendelea kupyaishwa kila siku ya maisha. Hii ni changamoto kwa waamini kumwilisha upendo wa Mungu ili uweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao ya kila siku. Watakatifu waliotangazwa na Mama Kanisa ni mfano bora wa kuigwa kwani wameonesha upendo mkuu kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao. Vazi lao la harusi lilipambwa kwa huruma na upendo wa Mungu! Waamini wakimbilie kwenye kiti cha huruma ya Mungu mara wanapogundua kwamba, vazi la harusi linaanza kuchafuka, ili kuonja tena huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.