2017-10-16 08:34:00

Utume wa Bahari na changamoto ya maboresho ya maisha ya wavuvi!


Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, chini ya uongozi wa Kardinali Peter Turkson, kuanzia tarehe 1 hadi 7 Oktoba 2017, limeendesha Kongamano la XXIV la Kimataifa la Utume wa Bahari, huko Kaohsiung, nchini Taiwan, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Nimenaswa katika mtego”. Kongamano hili limejielekeza kwa namna ya pekee katika mahitaji msingi: kiroho na kimwili kwa wafanyakazi katika sekta ya uvuvi pamoja na changamoto zinazotishia: usalama, utu na heshima yao.

Wajumbe wameitaka Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kupambana na biashara haramu ya binadamu; changamoto ya wahamiaji na wakimbizi; kazi za suluba pamoja na uvuvi haramu. Askofu mkuu Marcelo Sanchez Sorondo, Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi pamoja na Sayansi Jamii anasema, utumwa mamboleo na mifumo yake yote, bado iko hai na madhara yake yanaonekana sehemu mbali mbali za dunia! Kumbe, hapa kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Kardinali Peter Turkson kwa upande wake anasema, Utume wa Bahari unaowahusisha wafanyakazi zaidi ya milioni 38, ambao wanakabiliwa na changamoto kubwa sana katika sekta ya uvuvi kutokana na vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa huko baharini. Wavuvi ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kazi za suluba na utumwa mamboleo wanaofanyiwa wavuvi, madhara yake yanajionesha katika familia zao.

Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo la Yangon nchini Myanmar anasema, utandawazi na utamaduni usioguswa na mahangaiko ya watu wengine, umewapofusha watu kiasi hata cha kushindwa kuona nyanyaso dhidi ya wafanyakazi katika sekta ya uvuvi ambao, leo hii wamegeuzwa kuwa ni watumwa: kwa kufanyishwa kazi za suluba, kwa kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na kunyanyaswa, kwa kuishi na kufanya kazi katika mazingira duni sana, ingawa wanachangia katika ukuaji wa uchumi kitaifa na kimataifa.

Wataalam kutoka katika sekta ya uvuvi wamekiri kwamba, wavuvi wadogo wadogo wanafanya kazi ya “kijungu meko”, ambayo kamwe haitawasaidia kujikwamua kutoka katika umaskini wa hali na kipato. Kuna haja ya kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi katika sekta ya uvuvi sanjari na maeneo yao ya kazi, kwani hata leo hii anasema Kardinali Maung Bo, Kristo Yesu anaendelea kusulubishwa miongoni mwa wavuvi kutokana na maisha yao kuwa duni sana. Ni matumaini ya Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Itifaki ya maisha ya wavuvi iliyopitishwa hivi karibuni, inayoanza kutumika mwezi Novemba, itakuwa ni chachu katika maboresho ya ustawi na maendeleo ya wavuvi duniani; kwa kujikita katika sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia utu wao kama binadamu.

Kardinali Charles Maung Bo anakaza kusema, kuna haja ya kuendelea kuragibisha umuhimu wa Utume wa Bahari katika maisha na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Mama Kanisa. Waamini waelimishwe kuhusu mchango wa wavuvi, matatizo, changamoto na fursa mbali mbali wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao: kijamii na kiuchumi. Wafanyakazi na watu wanaojitolea katika Utume wa Bahari wamepongezwa sana na wajumbe wa mkutano huu kwa kazi na majitoleo yao. 

Wahudumu wa maisha ya kiroho wajengewe uwezo wa kukutana na kuzungumza na mabaharia pamoja na wavuvi, ili kuwasaidia katika mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili. Watu wafahamishwe nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa wavuvi sehemu mbali mbali za dunia hata kama wanachangia kwa kiasi kikubwa, ukuaji wa uchumi: kitaifa na kimataifa. Kumbe, hapa kuna haja ya kushikamana ili kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wavuvi pamoja na familia zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.