2017-10-16 08:10:00

Ulinzi, usalama na haki msingi za wakimbizi zipewe kipaumbele!


Kanisa katika maisha na utume wake, linapenda kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu hususan wakimbizi na wahamiaji wanaokabiliwa na changamoto kubwa kwa wakati huu. Hawa ni watu wanaokimbia vita; dhuluma na nyanyaso za kidini na kisiasa; majanga asilia pamoja na umaskini. Ni matumaini ya Vatican kwamba, Mkataba wa Kimataifa juu ya ulinzi na usalama wa wakimbizi utatekelezwa kwa dhati kama sehemu ya mchakato wa kulinda utu na heshima yao kama binadamu.

Ni vyema ikiwa kama Itifaki ya Kimataifa iliyotiwa sahihi kunako mwaka 1951 itazingatiwa ili kupambana na biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo pamoja na mifumo yake yote! Wakimbizi wanaoomba hifadhi ya kisiasa wanapaswa kuhudumiwa kikamilifu kwa kuzingatia sheria za nchi na mikataba ya Jumuiya ya Kimataifa. Kulinda uhuru wa wakimbizi, utu na heshima yao ni wajibu wa kimaadili unaopaswa kutekelezwa na watu wote, lakini zaidi na Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni hoja iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss katika mkutano wa Kamati kuu tendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani ni changamoto inayogusa na kutikisa mielekeo na tunu msingi za maisha ya mwanadamu na kwamba, dhamana ya kuwahudumia na kuwapatia watu hawa hifadhi ni sehemu muhimu sana ya amana ya binadamu katika kukuza na kudumisha udugu na mshikamano wa dhati. Katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia mambo makuu yafuatayo: kukaribisha, kulinda, kuhamasisha na kushirikisha; mambo yanayofumbatwa katika mchakato wa maendeleo endelevu! Ili kutekeleza mambo haya kuna umuhimu pia wa watoto kuhakikishia uraia katika nchi wanakozaliwa; kuheshimu umoja na mafungamano ya kifamilia na kijamii, bila kusahau haki zao msingi katika huduma ya elimu na afya badala ya kuwekwa vizuizini.

Askofu mkuu Ivan Jurkovič, anasema, Mpango Mkakati wa Huduma kwa Wakimbizi, CRRF,  ni changamoto kubwa na “donda ndugu” la nyakati hizi linalohitaji kushughulikiwa kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanahudumiwa kikamilifu, bila kuathiri huduma msingi za wananchi wanaotoa hifadhi kwa watu hawa. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba, Mpango Mkakati wa Huduma kwa Wakimbizi umeanza kutekelezwa sehemu mbali mbali za dunia. Ushuhuda na mang’amuzi kutoka katika nchi hizi unaweza kuwa ni chombo madhubuti katika mchakato wa kutengeza Mkataba wa Kimataifa juu ya ulinzi na usalama wa wakimbizi unaofumbatwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwamba, Mkakati huu utasaidia pia kupunguzu majonzi na masikitiko kutoka kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi ughaibuni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.