2017-10-13 15:13:00

Vatican: watu wana haki ya kupata maji safi na salama


Maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa sanjari na kuhakikisha kwamba, watu wanapata tiba muafaka kwa magonjwa yanayowasibu. Maji ni sehemu muhimu sana katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, lakini takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna watu zaidi ya bilioni 2 hawana uhakika wa maji safi wala salama, hali ambayo inatishia afya ya watu hawa sehemu mbali mbali za dunia. Maji safi na salama ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha Injili ya uhai, afya ya umma, utu na heshima ya binadamu!

Bado kuna watu milioni 884 hawana maji safi wala salama; watu takribani bilioni 2.5 hawana fursa za huduma bora ya afya ya jamii duniani. Umoja wa Mataifa kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa huduma ya maji safi na salama katika maisha ya watu, ndiyo maana ukaanzisha kampeni ya kimataifa “Maji ni uhai” kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2015. Tangu wakati huo, Jumuiya ya Kimataifa, Serikali pamoja na wadau mbali mbali wa maendeleo endelevu ya watu wameibua sera na mikakati ya maboresho ya huduma makini ya maji safi na salama kama sehemu ya haki msingi za binadamu.

Itakumbukwa kwamba, tangu mwaka 2003, dhana ya maji safi na salama imekuwa ikipewa kipaumbele cha pekee kwenye ajenda za Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, kwa sasa inaeleweka kimsingi kuwa, maji ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya binadamu, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki zake msingi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema maji ni kito cha thamani katika maisha ya binadamu na kamwe hayawezi kugeuzwa kuwa kama bidhaa ya kiuchumi, kwani pasi na maji safi na salama, maisha ya binadamu yako mashakani. Kutokana na mantiki hii, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu!

Hii ni sehemu ya upembuzi yakinifu uliofanywa na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye makao yake makuu mjini Geneva, nchini Uswiss kwa kushirikiana na wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa huko Geneva pamoja na “Mfuko wa Caritas in Veritate”. Wadau wote hawa wamegusia kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu ya binadamu ifikapo mwaka 2030 kwa kuzingatia changamoto za maendeleo mintarafu athari za mabadiliko ya tabia nchi. Wajumbe wamekazia umuhimu wa huduma ya maji kama sehemu ya uti wa mgongo wa maendeleo endelevu ya binadamu na kwamba, kuna uhusiano wa karibu kati ya utumiaji wa maji safi na salama kama nguzo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Haki ya maji safi na salama inadumisha Injili ya uhai na hivyo kuwa ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ikilinganishwa na watu wanaoteseka kutokana na magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyokuwa safi wala salama! Mchango wa sekta binafsi katika huduma ya maji safi na salama; maji na wakimbizi na wahamiaji; biashara ya maji na athari zake pamoja na utunzaji bora wa maji kwa ajili ya matumizi ya wote! Maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu inafumbatwa katika msingi wa uwepo wa maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu; uwezekano wa kupata maji haya katika umbali unaokubalika na Umoja wa Mataifa; uhakika wa upatikanaji wa maji kwa gharama nafuu kwa wote pasi na ubaguzi. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga ili kuhakikisha kwamba, haki ya maji inatekelezeka kwa wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, watu wote wanayo dhamana ya kutunza na kulinda vyanzo vya maji kwani hii ni haki msingi na sehemu muhimu sana ya uhai wa binadamu. Matumizi ya maji safi na salama kwa nidhamu na uwajibikaji ni muhimu sana, kwani maji yasipolindwa na kutunzwa vyema, yanaweza kuwa ni chanzo cha vita na migogoro ya Jumuiya ya Kimataifa kwa siku za usoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.