2017-10-10 13:30:00

Umoja wa Mataifa: Watoto 800 wameuwawa kikatili kwa mwaka 2016


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Gutterres anasikitishwa sana na taarifa ya mauaji ya watoto zaidi ya elfu 800 waliouwawa au kupata vilema vya kudumu kutokana na vita, ghasia na machafuko, sehemu mbali mbali za dunia. Lakini, watoto kutoka Yemen wameathirika vibaya zaidi, kwani takwimu zinaonesha kwamba, watoto zaidi ya 683 waliuwawa katika kipindi cha Mwaka 2016. Inasikitisha kuona kwamba, watoto hawa wametumiwa kama chambo wakati wa mapigano na wakati mwingine, wamefungiwa mabomu ya kujitosa mhanga kwa ajili ya kufanya mashambulizi katika maeneo mbali mbali yenye msongamano mkubwa wa watu; shuleni, hospitalini. Umoja wa Mataifa unawataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za mtoto kimataifa.

Kutokana na vita, ghasia na machafuko ya kisiasa na kidini, zaidi ya asilimia 11.5% ya watoto wapatao milioni 123 wanakabiliwa na umaskini mkubwa na hawana nafasi ya kwenda shule, kiasi cha kukwamisha juhudi za Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kupambana na baa la ujinga duniani. Nchini Siria na Iraq, watoto milioni 3.4 wamejikuta hawana tena fursa ya kuendelea na masomo. Takwimu zinaonesha kwamba, Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati, idadi ya watoto wasiokwenda shule imefikia milioni 16.

Umoja wa Mataifa unasikitika kusema, kwamba, katika kipindi cha miaka kumi mfululizo, idadi ya watu wanaoishi katika umaskini wa hali na kipato; wanateseka kutokana na magonjwa na ukosefu wa maji safi na salama pamoja na uhakika wa usalama wa chakula inazidi kuongezeka maradufu na kwamba, waathirika wakuu ni watoto na wanawake. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna vita, ghasia na machafuko katika baadhi ya nchi za Kiafrika yamesahauliwa na kuonekana kuwa ni sehemu ya maisha ya kwaida!

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Gutterres anasema,  ukosefu wa maji safi na salama; ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula; machafuko kati ya wakulima na wafugaji sehemu mbali mbali za dunia; ni kati ya mambo yanayohatarisha usalama, ustawi na maisha ya watoto duniani. Hali hii inachangiwa pia na athari za mabadiliko ya tabianchi: ukame wa muda mrefu pamoja na mafuriko. Hali hii pia inachangiwa na uchafuzi wa vyanzo vya maji, hali inayohatarisha afya ya watu. Kumbe, utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuhakikisha kwamba, watoto wanalelewa na kukua katika mazingira salama na yenye amani; kwa kupata fursa ya masomo, afya, ustawi na maendeleo yao kama yanavyobainishwa kwenye Haki ya Mtoto ya Umoja wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.