2017-10-10 14:26:00

Rais Uhuru Kenyatta na Bwana Odinga wahimizwa kudumisha majadiliano


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaendelea kuwahimiza Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Bwana Raila Odinga kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa hasa katika kipindi hiki tete che kuelekea katika marudio ya uchaguzi mkuu nchini humo. Maaskofu wanasema, lengo na majadiliano haya ni kudumisha amani, demokrasia na utawala wa sheria. Hayo yamesemwa na Askofu Philip Arnold Subira Anyolo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, Jumamosi, tarehe 7 Oktoba 2017 wakati wa sala ya kitaifa ya kuombea amani nchini Kenya, iliyofanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Kitaifa huko Subukia. Rais Uhuru Kenyatta, akiongozwa na busara kama mkuu wan chi, awe kiongozi wa kwanza kuchukua hatua ya kuganga madonda ya utengano na mpasuko wa kitaifa, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa; mambo msingi katika mchakato mzima wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais nchini Kenya, kumepelekea hali ya wasi wasi wa: amani, ulinzi na usalama; umoja na mshikamano wa kitaifa. Katika mazingira kama haya kuna haja ya wanasiasa kujikita katika mchakato wa majadiliano, umoja na mshikamano wa kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, limeshukuru na kumpongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuitikia mwaliko wao na hatimaye, kushiriki katika Sala ya Kitaifa kwa ajili ya kuombea: usalama, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Sala hii imeongozwa na kauli mbiu “Amani kwenye familia, amani nchini Kenya na matumaini kwa vijana”.

Kwa upande wake, Rais Uhuru Kenyatta ameishukuru familia ya Mungu nchini Kenya kwa kuungana pamoja katika sala kwa ajili ya kuombea: haki, amani, usalama na maridhiano kati ya wananchi wa Kenya. Amekumbusha kwamba, amani ni zawadi ya kwanza kabisa ambayo Kristo Yesu aliwakirimia wafuasi wake baada ya mateso, kifo na ufufuko wake.  Amewakumbusha waamini kwamba, Kristo Yesu ndiye amani yao, aliyewafanya wote kuwa wamoja, akibomoa kiambaza cha kati kilichokuwa kinawatenganisha.

Baraza la Maaskofu Katoliki linakaza kusema, kuna haja kwa familia ya Mungu nchini humo kujizatiti zaidi katika ujenzi wa: amani, umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kudumisha upendo kwa Mungu na jirani; daima kila mtu akijitahidi kuwa ni kikolezo cha mabadiliko katika jamii. Familia ya Mungu nchini Kenya kwa kusali na kuombea amani na mshikamano, inataka kuwa kweli ni mjenzi na chombo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu! Maaskofu wanawataka wananchi wa Kenya kuendelea kudumisha amani na utulivu, hasa wakati huu, wanapojiandaa kwa ajili ya marudio ya uchaguzi mkuu hapo tarehe 26 Oktoba 2017. Mahali ambapo kuna haki, amani na maridhiano, hapo, kuna maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limeiweka familia ya Mungu nchini humo chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa amani, hasa wakati huu ambapo homa ya marudio ya uchaguzi inaendelea kupanda na kushuka kila kukicha. Ni matumaini ya Maaskofu kwamba, uchaguzi mkuu ujao utakuwa: huru, wa haki na unaoaminika, ili kuwawezesha wananchi wa Kenya kupata kiongozi waliomchagua kihalali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.