2017-10-09 09:21:00

Jubilei ya Miaka 100 ya Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki


Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 9 – 12 Oktoba 2017 linafanya mkutano wake wa mwaka hapa mjini Roma, kama sehemu pia ya kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Baraza hili la Kipapa lilipaonzishwa. Ni mkutano unaopambwa pia kwa Jubilei ya Miaka 25 tangu kuchapishwa kwa Gombo la Sheria za Makanisa ya Mashariki. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutumia nafasi hii kuweza kukutana na kuzungumza kwa faragha na Mapatriaki pamoja na Maaskofu wakuu kutoka Makanisa ya Mashariki.

Hawa ni viongozi wa Kanisa wanaotekeleza dhamana na utume wao katika maeneo tete ya vita, ghasia na nyanyaso za kidini! Huko watu wa Mungu wanateseka sana kutoka na umaskini na hali ngumu ya maisha kwani wengi wao wamelazimika kuzikimbia au kuzihama nchi zao na kujikuta wakiishi “diaspora” au ugenini. Wengi wao wanatoka huko Mashariki ya Kati, yaani: Siria, Iraq, Uturuki, Lebanon, Yordani, Misri, Ethiopia na Eritrea bila kusahau Ukraine na Armenia. Mama Kanisa anatekeleza dhamana na utume wake katika mazingira magumu na hatarishi na hata wakati mwingine, kwa kukosa vitendea kazi katika shughuli za kichungaji, ili kulinda na kudumisha amana na utajiri wa kitaalimungu, kiliturujia, maisha ya kiroho na kinidhamu kati ya watu wa Mungu walioko kwenye Makanisa ya Mashariki.

Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki katika mkutano wake, linapembua kwa kina na mapana: changamoto zote hizi kwa kutambua na kuthamini utambulisho wa umoja na utofauti unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki. Ni nafasi ya kuibua vigezo muhimu kwa ajili ya uteuzi wa viongozi wa Makanisa ya Mashariki; Uratibu na usimamiaji wa mali za Kanisa kwa ajili ya shughuli za uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni fursa ya kukutana na kufahamiana na viongozi wapya walioteuliwa hivi karibuni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu kwenye Makanisa ya Mashariki; Majadiliano ya kiekumene na Tume ya Liturujia iliyorejeshwa tena madarakani na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015.

Ratiba elekezi ya maadhimisho yote haya inaoneshwa kwamba, Jumatatu, tarehe 9 Oktoba 2017, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Mapatriaki pamoja na Maaskofu wakuu kutoka Makanisa ya Mashariki. Umekuwa ni muda wa kusikilizana kwa dhati; kushirikishana: magumu, fursa na matumaini ya Makanisa mahalia na Khalifa wa Mtakatifu Petro, utaratibu mpya unaotumiwa na Baba Mtakatifu Francisko hata wakati wa hija za kitume “Ad Limina Visita” zinazofanywa na Maaskofu mahalia hapa mjini Vatican.

Tarehe 11 Oktoba 2017, wajumbe wa mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki watashiriki kwenye Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 12 Oktoba 2017 utakuwa ni uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki. Baba Mtakatifu atatumia nafasi hii kutembelea Taasisi ya Kipapa ya Makanisa ya Mashariki. Akiwa kwenye Taasisi hii, atabariki mti uliopandwa kwa ajili ya kumbu kumbu ya Miaka 100 na kukagua shughuli za ukarabati mkubwa uliofanywa kwenye majengo ya taasisi hii, atazungumza na wafadhili na kukabidhi barua ya uzinduzi wa maadhimisho haya. Baadaye, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Baadaye Baba Mtakatifu atarejea mjini Vatican kuendelea na shughuli nyingine wakati huo huo, Barua ya Baba Mtakatifu itasomwa rasmi kwenye Taasisi ya Kipapa ya Makanisa ya Mashariki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.