2017-10-07 17:40:00

Shamba la mizabibu ni kielelezo cha Ufalme wa Mungu na Kanisa


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXVII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa inaweka mbele ya macho yetu ya imani, shamba la mizabu lililotunzwa na kushughulikiwa sana ili liweze kuzaa matunda kwa wakati wake, lakini kwa bahati mbaya shamba hili likazaa zabibu mwitu! Watumwa waliokuwa wanalishughulikia wakageuka na kuwa kichwa maji, badala ya kutoa faida kwa wakati wake, wakaanza kuwatenda vibaya wajumbe wa Mwenye shamba hadi wakamkamata Mtoto wa mwenye shamba, wakamtupa nje ya shamba na kumfutilia mbali kwa upanga! Tunaambiwa shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli katika Agano la Kale na Kanisa katika Agano Jipya, na kila Mkristo ni sehemu ya ufalme wa Mungu unaojikita katika: toba na wongofu wa ndani; haki, amani, upendo na mshikamano!

Kwa ufupi kabisa, kwa mfano wa shamba la mzabibu, Mama Kanisa ametukumbusha historia nzima ya wokovu inayoonesha upendeleo wa Mwenyezi Mungu kwa taifa la Israeli, alilolichagua kati ya mataifa, ili wawe watu wake, akawalinda kama mboni ya jicho lake! Walipomwasi na kukengeuka, wakaishia utumwani, lakini akawaokoa kwa mkono wenye nguvu kutoka huko. Alitegemea kwamba, watazaa matunda mema kwa wakati wake, lakini bahati mbaya wakazaa zabibu mwitu kwa kukosa uaminifu, haki, amani na upendo! Watumwa wakageuka kuwa wakatili na wauaji na ndivyo walivyowatenda Manabii katika Agano la Kale.

Shamba la mizabibu ni kielelezo cha Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; unaosimikwa katika amani na kweli, staha, haki na upendo kama anavyofafanua kwa kina na mapana Mtume wa Paulo katika somo la pili. Kama ilivyokuwa kwa Wayahudi katika Agano la Kale kwa kumtenda jeuri yule mwana wa Mfalme, ndivyo ilivyokuwa hata katika Agano Jipya. Itakumbukwa kwamba, Yohane Mbatizaji ni Nabii anayeunganisha Agano la Kale na Agano Jipya, aliuwawa kwa kukatwa kichwa kwa sababu alikuwa ni shuhuda wa ukweli! Yesu ambaye ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele naye aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu siku ya tatu kama ilivyoandikwa! Na kwa njia ya ushuhuda wake, ameweza kuanzisha tena Ufalme wa Mungu unaoshuhudiwa na kuendelezwa na Kanisa lake.

Kristo Yesu ndiye Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa ni Jiwe kuu la pembeni. Wale waliokuwa wamepewa shamba la mizabibu yaani Ufalme wa Mungu, sasa wamekabidhiwa Wakristo wanaopaswa kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani yanayoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha imani tendaji! Hapa, Baba Mtakatifu Francisko anatumbusha kwamba, kila jiwe lina thamani ya pekee katika mchakato mzima wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa! Kwani limechaguliwa na kutengenezwa na hatimaye, likapachikwa mahali pake. Hii ndiyo ile neema ambayo waamini wameipata kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, wakaimarishwa kwa Karama za Roho Mtakatifu pamoja na Neno la Mungu! Sasa wanatakiwa kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: maisha ya sala na amani ya Mungu. 

Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa ukweli, haki na utu wema! Mambo msingi yanayofafanuliwa kwa kina na mapana na Mtakatifu Paulo anapowaandikia Wafilipi katika somo la pili. Wakristo wanapaswa kuzaa matunda ya toba na wongofu wa ndani, kielelezo muhimu sana cha ushuhuda katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wakristo wakikosa kinga za maisha ya kiroho mwilini mwao; wakakengeuka na kumwasi Mwenyezi Mungu, watakiona cha mtema kuni!Kumbe, kuna haja ya kuwa waaminifu katika ahadi zao za Ubatizo na kwa kutenda zaidi.

Tumwombe, basi Mwenyezi Mungu katika Juma hili, tuweze kuwa kweli ni mashuhuda amini katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani! Ufalme unaosimikwa katika haki, amani, upendo, umoja na udugu! Roho Mtakatifu atuwezeshe tuwe kweli ni vyombo vya utii na unyenyekevu katika kusikiliza na kutekeleza Amri na Maagizo ya Mungu katika maisha yetu! Huu ni wakati wa kuendeleza zile changamoto tulizozipokea wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.