2017-10-07 16:43:00

Kongamano la Kimataifa: Malezi na mang'amuzi katika maisha ya kipadre


Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, hapo tarehe 8 Desemba 2016 lilichapisha Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Malezi na majiundo ya kipadre yanapaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa. Hizi ndizo sababu msingi ambazo zimepelekea kuchapishwa kwa Mwongozo wa Malezi ya Kipadre yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya kipadre, ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ni mwongozo ambao umetungwa kwa kuzingatia maswali muhimu katika maisha ya wakleri: matatizo, changamoto, fursa na matumaini ya  wakleri katika maisha yao Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee. Msingi wa mwongozo huu ni majiundo ya kitume kwa mapadre katika utekelezaji wa utume wao. Mwongozo huu ni mchango kutoka katika uzoefu na mang’amuzi kutoka kwenye Makanisa mahalia, Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na ushauri uliotolewa na mabingwa katika malezi na majiundo ya kikasisi.

Itakumbukwa kwamba, Mwongozo wa kwanza wa Malezi ya Kipadre ulitolewa kunako mwaka 1970, ukafanyiwa marekebisho makubwa wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1985. Tangu wakati huo, kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya kitamaduni na kijamii pamoja na maboresho ya mafundisho ya Mababa wa Kanisa kuhusu: maisha, utume na utambulisho wa Padre. Huu ni ufafanuzi ambao umetolewa Alhamisi, tarehe 5 Oktoba, 2017 na Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri wakati akitoa hotuba elekezi kwenye Kongamano la Kimataifa juu ya “Mwongozo wa Malezi ya Kipadre”. Kongamano hili limekuwa likifanyika huko Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma na kuhitimishwa tarehe 7 Oktoba 2017.

Mwongozo wa Malezi ya Kipadre umeboreshwa kwa kufafanua zaidi tasaufi ya maisha, wito na utume wa kipadre, mintarafu dhana ya kimisionari inayokaziwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwataka mapadre kutoka sakristia na kuwaendea watu wa Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Ili kufanikisha lengo hili, kulikuwa kuna haja ya kuwa na mwongozo makini wa malezi ma majiundo ya kipadre! Huu ni mwongozo unaofumbata malezi na majiundo mazima ya kipadre kwa kukazia: maisha ya kijumuiya na kimisionari sanjari na utume kadiri ya Kristo mchungaji mwema.

Mwongozo unasisitizia umuhimu wa mang’amuzi ya maisha ya kiroho na katika shughuli za kichungaji. Kumbe, majiundo ya kipadre hayana budi kujikita katika: umoja na kuwa endelevu kwa kumwambata mtu mzima: kiroho na kimwili; kiakili na kichungaji; kijumuiya na kimisionari kwa kutambua kwamba, wito unazaliwa na kulelewa katika Kanisa kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu. Majiundo yana mwelekeo wa kimisionari kwa sababu, majandokasisi wanafundwa ili kushiriki katika azama ya uinjilishaji unaomgusa mtu: kiroho na kimwili. Maisha ya seminari, yanapaswa kukuza na kudumisha dhana ya maisha ya kijumuiya, lakini kila mtu akiangaliwa kwa jicho la pekee katika malezi.

Uteuzi wa majandokasisi wanaotarajiwa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre unapaswa kufanywa kwa umakini na katika hali ya ukomavu: kiroho na kimwili, baada ya kufanya mang’amuzi ya maisha ya kiroho yanayoboreshwa kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti pamoja na Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Hapa, Mama Kanisa anataka kumwandaa mfuasi wa Yesu atakejisadaka bila ya kujibakiza katika maisha na utume wake, daima akijitahidi kufuata nyayo za Kristo Yesu, mchungaji mwema. Hija hii ya kitume inamwelekeza jandokasisi katika Daraja Takatifu ya Upadre, ili kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa: kwa kuwatafuta wale waliopotea ili kuwaganga na kuwaponya kwa mafuta ya huruma ya Mungu. Mtume na mchungaji ni mambo msingi katika hija ya majiundo ya kipadre anasema, Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.