2017-10-06 06:32:00

Papa Francisko: Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai!


Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha, kuanzia tarehe 5 Oktoba hadi 7 Oktoba, 2017 inaadhimisha mkutano wake wa XXIII, kwa kuongozwa na  auli mbiu inayoongoza mkutano huu ni “Kusindikiza maisha wajibu katika wakati huu wa maendeleo ya teknolojia”.  Huu ni wajibu msingi wa Mama Kanisa unaojikita katika kuangalia fursa na changamoto zinazojitokeza katika maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya tiba ya mwanadamu; kanuni maadili na matatizo yanyoweza kujitokeza. Mama Kanisa anapenda kukazia kuhusu umuhimu wa maisha ya binadamu na hatima yake mintarafu imani ya Kikristo inayoongozwa na Neno la Mungu.

Huu ni wakati wa Jumuiya ya Kimataifa kujikosoa, changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi na Kanisa kwa kuangalia mapungufu yake katika utekelezaji wa kanuni maadili, ili kuendelea kujikita katika mchakato wa kusindikiza maisha ya mwanadamu katika hatua zake mbali mbali kwa kujikita katika ushuhuda wa imani inayofumbatwa katika huruma ya Mungu! Kwa muhtasari, haya ndiyo mawazo makuu yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha, Alhamisi, tarehe 5 Oktoba 2017.

Baba Mtakatifu anasema, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya tiba ya mwanadamu ambayo kwa sasa inatishia Injili ya uhai; kwa kusababisha kinzani katika kanuni maadili, kijamii na kisheria, kiasi hata cha kutishia utu na heshima ya binadamu mintarafu nadharia na vitendo vya sayansi. Kanisa kwa upandwe wake linapenda kujikita katika asili, umuhimu na hatima ya maisha ya binadamu ili kufafanua mambo yanayotishia uhai wa binadamu; ubora wa maisha pamoja na kuangalia fursa zinazotolewa na sayansi pamoja na teknolojia katika matamanio halali ya maboresho ya maisha ya binadamu bila kutumbukizwa katika mtego wa wajanja wachache kutaka faida kubwa kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia duniani, lakini bado kuna umaskini mkubwa wa hali na kipato duniani, changamoto kwa watunga sera na maendeleo ya binadamu kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya uhai na furaha ya kweli dhidi ya utamaduni wa kifo! Hii ni dhamana inayowataka kuwajibika, kupenda kwa dhati na kuwaheshimu watu katika hatua zao mbali mbali za maisha! Changamoto hii inatekelezwa na Mama Kanisa kwa kujikita katika mwanga wa Neno la Mungu unaofumbata kazi ya Uumbaji na Ukombozi, kielelezo makini cha baraka na upendo wa Mungu kwa binadamu wote ambao Mwenyezi Mungu ameamua kufunga nao Agano katika kazi ya uumbaji na historia katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, agano kati ya Mungu na mwanadamu linamwajibisha binadamu kurithisha zawadi ya maisha kwa njia ya ndoa, familia na jamii katika ujumla wake. Hapa kuna haja ya ushirikiano wa karibu sana kati ya Serikali na Kanisa ili kusaidia kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kuheshimu kazi ya uumbaji na historia ya mwanadamu. Kutokana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha ya ndoa na familia, Kanisa halina budi kujikosoa kwa kuchelewa kuchukua hatua madhubuti kwa kutokazia sana kanuni maadili kwa kuzingatia utamaduni unaowatambulisha na kuwatofautisha watu kadiri ya jinsia zao; kwa kutambua na kuthamini utu wao kama binadamu walioumbwa kwa jinsia tofauti lakini, wanakamilishana katika safari ya maisha yao.

Tofauti hizi msingi ndiyo siri ambayo inamshirikisha mwanadamu katika kazi ya uumbaji na urithishaji wa maisha. Uchakachuaji wa kibaiolojia na kisaikolohia mintarafu tofauti za kijinsia kwa njia ya maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kisingizio cha uhuru wa mtu binafsi ni hatari sana! Kumbe, hapa, Kanisa linataka kukazia kazi ya uumbaji katika maisha ya binadamu ni jambo muhimu sana na wala si tishio la ustaarabu na ustawi wa wengi! Watu wajizatiti kikamilifu kukataa na kupinga mawazo yanayokazia usawa wa kijinsia nje ya mpango wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mama Kanisa anataka kujizatiti kusindikiza maisha katika hatua zake mbali mbali na kwamba, hii si dhamana ya sayansi ya tiba na ustawi wa jamii; kwani kuna mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza; kwa kulindwa na kuheshimiwa na mtu binafsi na jamii katika ujumla wake na wala si bidhaa inayoweza kuuzwa au kununuliwa sokoni. Inasikitisha kuona kwamba, Jamii inajenga na kusimika miji inayotishia usalama, maisha na ustawi wa watoto pamoja na wazee. Maisha ya binadamu yanapaswa kulindwa na kudumishwa.

Mwishoni Baba Mtakatifu anakaza kusema, ushuhuda wa imani inayofumbatwa katika huruma ya Mungu ni kielelezo cha haki na upendo kwa zawadi ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Huu ndio utume wa Taasisi ya Kipapa kwa Ajili ya Maisha kuwaandaa mashuhuda, wasomi watakaosimama kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai. Baba Mtakatifu kwa niaba ya Kanisa zina, anapenda kuwashukuru wajumbe wa Tume hii ya Kipapa kwa wajibu wake wa kutetea maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni utume unaojikita katika mang’amuzi, akili na upendo kwa ajili utume kwa maisha ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.