2017-10-06 15:49:00

Monsinyo Vigano: Mawasiliano ya Baba Mtakatifu ni ya moja kwa moja


Lugha mpya ni njia muhimu ya kutafakari ambayo haipunguzi  katu lugha ambazo Kanisa kwa muda mrefu imekuwa ikitumia na ambayo inatoa fursa ya kuendeleza mazungumzo ambayo Bwana alitumia wakati ule kuelimisha watu ili waweze kujibu zawadi kubwa ya Mungu anayoitoa mwenyewe na kwa watu wote. Ni Maneno ya  Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano  Vatican, Monsinyo Dario Vigano akihutubia mapema wiki hii katika Toleo la 30 ya wiki ya Mafunzo ya Kitelojia yenye mada inayohusu lugha mpya za kuwasiliana huko Pistoia Italia.

Monsinyo Vigano katika hotuba yake, amejikita zaidi kuelezea lugha mpya na hasa akitafakari juu ya mawasiliano ya Baba Mtakatifu katika Kanisa na kwa jamii. Njia za kuwasiliana kwa Baba Mtakatifu katika Kanisa na jamii daima zinathibitisha hali halisi ya tunavyoishi, kwa maana yeye anasisitiza umuhimu wa kusikiliza, kusikiliza sauti za vyombo vya habari kwa makini, kuchambua mwelekeo wake na kuwa na subira katika  kutoa huduma kwa ajili ya Injili.
Tabia ya Baba Mtakatifu imejionesha hata wakati wa kutoa sauti za ukarimu  na kuwasiliana, ambayo Monsinyo Viganao anabainisha kuwa inakwenda kinyume na  yule apigaye kelele  na kumfanya msikilizaji a hasiwe kufuata kwa makini kile kinachotolewa au kuzungumza. Kwa njia hiyo, anatufundisha Baba jinsi gani ya kuwasiliana kwa ukarimu, upole , sauti za chini na kusikiliza kwa makini.

Akitoa mfano halisi na  rahisi ya mawasiliano ya Baba Mtakatifu anasema, Yeye  ana uwezo wa kuelewana na kila mmoja katika mitandao ya kijamii, kwa mfano kwa vijana, kutumia selfie, kuwapigia simu watu wengi, na hiyo ndiyo tabia ya Baba Mtakatifu katika mawasiliano yake.
Katika kuthibitisha zaidi anasisitiza akisema,Mawasiliano ya Baba Mtakatifu yanakwenda sambamba na nyakati za sasa, mahali ambapo kuna hata mabadiliko ya mawasiliano  Vatican. Kwa mtazamo wa Mtakatifu Ignatio wa Loyola, anaendelea Vigano, Baba Mtakatifu ana uwezo wa kumfikia kila mmoja, kujikita katika mawasiliano, siyo tu katika kusema na kutenda, bali hata kusikiliza kwa makini na kutambua jinsi gani ya kuweza kusaidia inapobidi kwa hali halisi. Hiyo ndiyo kutambua kwa macho na moyo wa upendo wa Mungu.

Uhusiano wa Baba Mtakatifu ni ule unaojikita katika jadi anasisitiza,  kwa maana ya mazungumzo ya moja kwa moja na vijana, kwa wale wote wenye kuwa na  sababu, kama vile wenye imani haba au wasio jihusisha kamwe na imani. Aidha anasema, Baba Mtakatifu anayo karama na zawadi ya ukaribu na jirani, hiyo imeweza kujionesha na kushuhudiwa wazi na wengi katika matendo yake ya kila siku, ni katika  maneno na mifano mingi inayojieleza kwenye maisha yake ya kawaida ya kila siku.

Monsinyo Vigano  anabainisha  pia juu ya muhimu na mtindo wake wa kuwasiliana, kama vile kuinamia watu, kuwapokea, ucheshi, hizo ni mifano rahisi lakini, pamoja na ishara mbalimbali rahisi za kila siku katika kutumia lugha rahisi ya moja kwa moja, hata kile kitendo cha kubeba mkoba wake bila kusaidiwa na mwingine, ndiyo njia ya lugha mawasiliano ya Baba Mtakatifu.
Mwisho Monsinyo Vigano anasisitiza juu ya  ulazima wa mwamini  kuishi kama anayefanya mazoezi ya shahuku ya mambo ya Mungu. Ni kwa njia hiyo tu sote  tutakuwa ni jumuiya iliyofanikiwa  yaani ni Kanisa ambalo linajihusisha kuwasilisha kwa furaha Injili na uwepo wa Injili hiyo katikati ya watu bila ya ubaguzi.

 Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.