2017-10-06 07:09:00

Kuna haja ya kuboresha maisha ya wavuvi na haki zao msingi!


Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo msingi yanayopaswa kukuzwa na kudumishwa katika maeneo ya kazi sanjari na kuzingatia mambo msingi katika maisha ya mwanadamu. Lakini, hii ni changamoto kubwa inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa katika sekta ya uvuvi duniani. Licha ya mchango mkubwa unaotolewa na sekta hii katika uchumi, ustawi na maendeleo ya binadamu, lakini ni kati ya sekta zinazokabiliwa na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu.

Hii ni hoja iliyotolewa hivi karibuni na Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Kilimo na Chakula ya Umoja wa Mataifa, wakati alipokuwa anashiriki katika Kongamano la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi na Uvuvu, lililofunguliwa hapo tarehe 3 Oktoba na kuhitimishwa tarehe 5 Oktoba, 2017 huko mjini Vigo, nchini Hispania. Kongambano hili limeandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, kwa kushirikiana na Shirikikisho la wafanyabiashara wa mazao ya kilimo na uvuvi kutoka Hispania.

Wazo kuu la kongamano hili ni kuona jitihada za Jumuiya ya Kimataifa katika maboresho ya kazi hasa katika sekta ya uvuvi na kilimo, kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshimaya wakulima na wavuvi duniani. Kwa bahati mbaya anasema Monsinyo Fernando Chica Arellano sekta ya uvuvi duniani inakabiliwa na changamoto pevu ya biashara haramu ya binadamu, uharamia pamoja na uvuvi haramu, mambo yanayohatarisha utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Itakumbukwa mada hii, imewahi kujadiliwa na FAO kwenye mkutano wake uliofanyika mwezi Novemba, 2016 mjini Roma, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uvuvi Duniani kwa mwaka 2016 na Kardinali Pietro Parolin, akatoa hotuba elekezi kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa kuitaka kujielekeza zaidi katika mchakato wa maboresho ya kazi, kwa kuhakikisha kwamba, wavuvi wanaheshimiwa na kuthaminiwa katika utume wao sanjari na kuhakikisha kwamba, wanafanya kazi katika mazingira bora zaidi, ikilinganishwa na hali ya wakati huu!

Sekta ya uvuvi, mara nyingi imechambuliwa katika mtazamo wa sheria, malipo na sitahiki za wavuvi; usalama wa maisha ya wavuvi na vyombo vyao vya kazi pamoja na afya yao. Lakini, kuna haja pia ya kuanza kuangalia ubora wa maeneo ya kazi katika sekta ya uvuvi, kwa kutambua na kuthamini utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, sekta ya kilimo na uvuvi inatoa ajira kwa watu zaidi ya milioni 57 sehemu mbali mbali za dunia na kati yao, asilimia 19% ni wanawake.

Idadi hii ya watu wanaoajiriwa kwenye sekta ya kilim ona uvuvi inapaswa kuboreshwa pia na umati mkubwa wa wafanyabiashara wanaojihusisha na mchakato mzima wa utengenezaji, usafirishaji na masoko kwa bidhaa zinazozalishwa katika sekta ya kilimo na uvuvi duniani, ambayo inakadiriwa kuwa ni zaidi ya wafanyakazi milioni 200, kumbe, hawa ni wadau muhimu sana katika kukuza sekta ya uchumi. Katika nchi changa duniani, hata wanawake nao wanashiriki katika kuchangia uzalishaji kwenye sekta ya kilimo na uvuvi.

Monsinyo Fernando Chica Arellano katika hoja zake msingi, anapenda kukazia kwa  namna ya pekee kabisa: ulinzi na usalama kwa utu, heshima na haki msingi za wavuvi sehemu mbali mbali za dunia. Lazima, sheria, kanuni, miongozo na utifaki za Jumuiya ya Kimataifa kutekelezwa na hasa zaidi katika sekta ya uvuvi pamoja na kusimama kidete kupambana fika na biashara haramu ya binadamu inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Wavuvi wanapaswa pia kupata muda wa mapumziko, ili kuongeza tija na ufanisi katika kazi.

Juhudi zote hizi hazina budi kwenda sanjari pia na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Hapa jambo la msingi ni kukuza na kudumisha ekolojia ya mazingira na ekolijia ya binadamu. Kuna itifaki ya sekta ya uvuvi iliyopitishwa na Shirika la Kazi Duniani, ILO, kwa mwaka 2007 kuhusu kazi katika sekta ya uvuvi inayobainisha mambo msingi yanayoapswa kuzungatiwa na wadau mbali mbali katika maboresho ya maisha, kazi na huduma inayotolewa na wavuvi katika sekta ya uvuvi! Kimsingi, utawala wa sheria na haki msingi za binadamu unapaswa kuzingatiwa na kamwe wavuvi wasionewe kwa kufanyishwa kazi kinyume cha utu na heshima yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.