2017-10-06 07:33:00

Jeuri ya binadamu ina kikomo; huruma ya Mungu haina mipaka!


Mwenyezi Mungu ametuumba na kutukabidhi wajibu akisema: “zaeni, mkaongezeke, makijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi” (Mw 1:28). Huu ni uwekezaji mkubwa na wa aina yake ambao Mungu anaufanya kwa wanadamu. Mungu anamkirimia kila mmoja kipawa chake maalum ili kwa utendaji wake kadiri ya mapenzi yake Mungu ulimwengu uweze kupambika. Hapa tunaona chimbuko la kwanza la wito kwa wanadamu wote. Nafasi tunayopewa na Mungu ni kwa makusudi ya kuutiisha ulimwengu, yaani kuzaa matunda mema yanayoendana na kusudi la Mungu ndani mwetu. Tuepuke kuichezea shilingi shimoni. Tuitambue thamani yetu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Neno la Mungu leo hii hususani Somo la Kwanza na Injili liufafanua huo uwekezaji mkubwa wa Mungu. Mungu anaonesha uwekezaji wake huo kwa namna mbili. Kwanza kwa mtu binafsi na pili kwa ajili ya kuwahudumia wengine. Ni kana kwamba anaanza kumuunda mtu vyema na kufanya juhudi yote ili akamilike na mwishoni amtume kwenda kumwakilisha au kuufunua uso wake kwa watu wengine. Nabii Isaya anaonesha kwanza matumaini ya Mungu kwani anachagua mahali penye rutuba na penye uhakika wa kutoa matunda. Mahali palipopandwa mzabibu ni “kilimani penye kuzaa sana” na ndani yake ndipo anapanda mzabibu na kuupatia huduma zote muhimu kama vile ulinzi, maji ya kutosha na samadi na ana matumaini ya kutoa matunda mema.

Somo la Injili kwa upande mwingine linatuwekea picha ya mmoja aliyeliandaa shamba zuri la mizabibu na kulipatia huduma zote muhimu kama hapo juu na kwa hakika mzabibu ukastawi vizuri kisha akakodisha watu kulitunza akitarajia kupata matunda mazuri. Matokeo ya kazi hizi njema ni ya kukatisha tamaa. Mpandaji katika somo la kwanza alitegemea zabibu lakini mti wake “ukazaa zabibu-mwitu”. Mwenye shamba katika somo la Injili alitegemea kupewa matunda yake lakini waliokodishwa waliishia kuwadhuru watumishi wake aliowatuma na hata alipomtuma Mwana wake wakamuua. Ni matokeo yenye kukatisha tamaa. Mmoja anaweza kujiona kwamba amepoteza muda na nguvu zake kiasi cha kupokea majibu hasi kama hayo.

Tukiitafakari nafasi ya kwanza tunamuona mwanadamu aliyekengeuka na kuiacha njia ya haki. Mungu ametuumba akikusudia sisi kumjua, kupenda na kumtumikia na mwisho kuungana naye mbinguni. Matunda mema ya wito wetu yatawezeshwa na utii wetu katika makusudi haya manne ya Mungu kwa wanadamu. Wito wa mwanadamu ni kuufikia ukamilifu kama alivyo Mungu wetu (Rej Mt 5:48). Mungu anawekeza kwa kila mmoja kupitia matendo mema ya binadamu wenzetu. Kwanza kupitia wazazi wetu ambao wanatupenda na kutuongoza katika njia njema. Pia kupitia ndugu na majirani zetu. Maneno na maelekezo yao ni mahsusi kutufanya tuweze kuzaa zabibu bora. Maneno na makuzi yao yakipitia sikio moja na kutokea sikio jingine tunageuka zabibu mwitu. Tusisahau kuwa “asiyesikia la mkuu huvunjia guu”. Tuonyeshe shukrani kwa utii wetu katika maelekezo mbalimbali kuelekea ukamilifu. Tuweke pembeni kiburi chetu na majigambo yetu.

Kwa nafasi ya pili tutafakari juu ya miito mbalimbali ambayo tunakabidhiwa na Mungu. Mithili ya watunzaji wa mfano katika Injili mwanadamu anaingia katika ukosefu wa uaminifu na matokeo yake ni kunyang’anywa wajibu wake. Kila mmoja anatumwa kuhangaikia wokovu wake na wa watu wengine. Lakini mfano wa watumishi hawa, ambao ni matokeo mabaya ya mfano wa kwanza kwani badala ya kuwa zabibu njema wamekuwa zabibu mwitu, tunageuka kuwa wadhulumu wa kazi za Mungu. Unapewa wito utoe matunda ila unageuza ni juhudi zako na watumishi wanaotumwa kuchukua matunda unawabalasa. Hili linathibitishwa na wanadamu katika jamii ya leo ambao wamejitwalia madaraka ya kila kitu na kupora mali za Mungu. Matokeo yake ni mabaya kwani wote hawawajibiki kadiri ya miito yao na hivyo huingia uzembe, unyonyaji na rushwa katika nafasi mbalimbali.

Mfano wa mwana wa mwenye shamba la mizabibu ni mfano wa Kristo ambaye alipokuja kuhitimisha ufunuo wa Neno la Mungu na hivyo kuusimika ukweli alipingwa na wakamtoa nje ya mji na kumuua. Hivi ndivyo Neno la Mungu linavyoendelea kusubishwa leo hii. Jamii ya kisekulari inalitoa Neno la Mungu nje ya mambo yake, jamii hii inendelea kumsulubisha Kristo na haioni kuwa inawajibika katika kutoa matunda yaliyo mema. Mambo ya kijamii leo hii ni aghalabu kuangaziwa na Neno la Mungu na mbaya zaidi juhudi zinapofanywa kulipenyeza Neno hilo majibu yake ni kuambiwa “bene curere sed extra viam”, yaani maneno yenu ni mazuri lakini si mahali pake. Mungu aliyeumba mbingu na Dunia ananyang’anywa kazi ya uumbaji wake na kiumbe chake alichokiumba yeye mwenyewe.

Mungu katutendea kwa ukarimu lakini sisi tunajibu kwa ukorofu na kumuasi. Uasi wetu hautanyamaziwa na Mungu. Tunapoacha kuitumia vema nafasi tunayopewa na Mungu ama atatuacha na kuharibiwa na wanyama wakali. Mwenyezi Mungu anatuambia “nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake”. Mmoja naweza kuhoji ipo wapi hapa huruma ya Mungu. Kama kweli anampenda mwanadamu kwa nini anamwacha aangamie? Lakini lazima kuitambua hadhi ambayo mwanadamu amepewa na Mungu. Mwanadamu ameumbwa huru na hivyo pamoja na Mungu kufanya juhudi ili kuzaa matunda mema mwanadamu amechagua njia ya maangamizi. Mungu wetu ni mwenye huruma lakini pia hutenda kwa haki.

Watunzaji wa shamba ya mzabibu Neno la Mungu linatuambia kwamba “Mungu atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake”. Uzembe katika kuitikia wito yaani katika kuhudumia mahali fulani hakumfanyi Mungu kulala usingizi. Upendo wake ni wa milele na hivyo atatafuta namna nyingine ya kuwahudumia watu wake. Haki ya Mungu inadhihirika katika hili na pia tunatahadharishwa na kukumbushwa kwamba nafasi tunazopewa katika jamii ni mahsusi kwa ajili ya kuweka mchango wako kwa manufaa ya jamii nzima. Tunapoanza kupindishapindisha tunahatarisha kuiharibu jamii na hivyo Mungu hatosita kutuondoa katika nafasi zetu ili kuwaweka wale “watakaomlipa matunda kwa wakati wake”.

Lakini hii haimaanishi kuwa hawa waovu wamefungiwa mlango milele. Wimbo wa Zaburi unamkumbusha Mungu wema wake na hivyo kuomba tena awarudie watu wake na Paulo anakazia kuwa tumwendee Mungu kwa toba na kubaki na amani ya Mungu katika matendo mema. Kumbe bado kuna fursa la kurudi katika mstari kwani Mungu huruma yake kuu ni ya milele. Tujiulize leo, je! Mungu amewekeza nini katika nafasi yangu niliyonayo? Je, anatarajia matunda gani kutoka kwangu? Je, ninamlipa kwa wakati au najilipa mwenyewe na kumpora Mungu mali yake?  Tutambue kwamba kupindisha wito wako mahsusi aliokuutia Mungu hakukupatii furaha bali mahangaiko na pia tuepuke kuichezea shilingi shimoni.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.