2017-10-06 08:11:00

Imani inamwilishwa katika matendo!


Ipo aina fulani ya imani huko Marekani inayosema kuwa tunachotakiwa kufanya ni kuungama kwamba Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi na kuweka matumaini yetu yote kwake. Cho chote tufanyacho  zaidi ya kushika aina hii ya imani hakina maana yo yote kwa ajili ya wokovu. Hata dhambi zetu haziathiri ukweli na upendo wa Mungu katika Kristo. Imani hii inaweza kuenea au ikawepo miongni mwetu na pengine ikakubalika bila kung’amua mara moja au pole pole madhara yake. Kusema kweli kinachosemwa hapa au uelewa huu au fundisho hili juu ya nafasi ya imani kuhusu wokovu ni kweli kabisa. Imani hii yaeleza wazi kuwa Mungu ni upendo – 1 Yoh: 4:16 – nasi tumejua mapendo anayotuelekeza Mungu, tukayaamini. Mungu ni upendo, na mwenye kuishi katika upendo, anaishi ndani ya Mungu na Mungu anaishi ndani yake. Kwamba Mungu ni upendo, hivyo ni lazima apende, hatuwezi kumbadilisha.

Mungu alitupenda hata kabla ya sisi kumpenda, na ametupenda si kwa sababu ya kitu fulani tulicho nacho, lakini katika uhuru wake. Musa anawaambia Waisraeli kuwa upendeleo wao si kwa sababu ni taifa kubwa bali Mungu amewapendelea. Kum. 7:7-8 -  Bwana amewapendelea ninyi na kuwateua si kwa sababu mu wengi kuliko mataifa mengine, maana mu wachache kuliko wengine. Lakini ni kwa kuwa amewapenda ninyi ili atimize kiapo alichowaapia baba zenu, ndiyo sababu Bwana aliwatoa kwa mkono wenye nguvu, na kuwakomboa katika nyumba ya utumwa na katika uwezo wa Farao, mfalme wa Misri. Na 1 Yoh: 4;10 – huu ndio upendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwana wake awe malipizi ya dhambi zetu

Mtume Paulo akiongea kuhusu wokovu katika  – Gal. 2:16 –anasema hivi:  lakini kwa kuwa tumetambua ya kuwa mwanadamu hafanywi mwadilifu kwa matendo ya sheria ila kwa kumwamini Yesu Kristo, nasi tumemwammini Yesu Kristo tupate kuthibitishwa kwa kumwamini Kristo, si kwa matendo ya sheria. Hapa yaonekana Paulo akitaja imani tu kama inatosha kupata wokovu. Hivyo imani tajwa hapo juu inapata nguvu. Tutaona hapo mbele ufafanuzi wa ufahamu huu na Paulo mwenyewe. Ni kweli hatuwezi kuununua wokovu, ni zawadi ya Mungu kwetu.

SEHEMU B.

Hayo yote yaliyosemwa hapo juu twayapokea na  ni kweli. Kweli Mungu ni upendo na kweli ametuonesha yeye kwanza upendo wake. Ni kwa kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi katika imani ya kweli tunapokuwa au kufanywa wenye haki mbele ya Mungu. Kinyume chake ni kupinga Neno la Mungu. Shida iliyopo katika fundisho hilo au ufahamu huu hapo juu au huo mfumo wa maisha wa aina hiyo ya ukristo si katika kile kinachosemwa ila shida ipo katika kile ambacho hawajakisema. Ifahamike kuwa pamoja na kwamba Mungu anatupenda upeo, hilo pendo ni lazima lipokelewe na kujibiwa na mwanadamu. Kama hakuna jibu wazi katika maisha yetu, basi tunamtania Mungu. Shida hiyo inaoenekana katika somo la 1 na 3.

Mwinjili Yohane huyo ambaye hapo juu tumeona akisema Mungu ni upendo na wale wanaosisitiza mtindo wa maisha tajwa hapo juu wameishia hapo anaendelea kusema – 1Yoh: 4:11 – wapendwa, kama Mungu ametupenda hivyo, imetupasa nasi kupendana. Bahati mbaya hawa wenye imani tajwa hapo juu hawakufikia sehemu hii. Ni kwa namna hii Waisraeli katika somo la kwanza na waliokabidhiwa shamba katika Injili walishindwa kumheshimu hata mrithi wakamuua. Kwa maneno mengine ni lazima turuhusu pendo la Mungu lifanye kazi katika maisha yetu.

Mtume Paulo – anayesema tutafanywa wenye haki kwa imani katika Yesu katika Gal 2:16 anafafanua mafundisho yake katika Rum. 2:6 – akisema atamlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake na katika Rum. 2:13 – anasema – si wenye kuisikia sheria walio waadilifu kwa Mungu, bali wenye kuitimiza sheria ndio watakaofanywa waadilifu. Maelezo haya ni muhimu kuelewa masomo yetu ya leo Jumapili ya 27 A ya kawaida ya mwaka: i. katika Somo la I – Nabii Isaya anaongea juu ya pendo lililokataliwa. Kilichofuata ni adhabu ya Mungu. ii. Katika somo la II – mtume Paulo kwa Wafilipi – anatoa mwaliko kuishi kadiri ya fundisho sahihi na katika Injili – wimbo wa Nabii Isaya toka somo la I unapewa mahadhi ya Kikristo. Wale waliokabidhiwa shamba – kwa sababu ya kukosa uaminifu watanyang’anywa.

Ni lazima kuamini pendo la Mungu kwetu. Yeye alitupenda kwanza. Ni lazima kuungama kuwa Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi. Lakini ni lazima pia kukumbuka kuwa katika Yoh: 15:16 anasema – si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi, kusudi mwende kuzaa matunda, na matunda yenu yadumu, ili Baba awapeni yote mwombayo kwa jina langu. Kwa maana nyingine akija apate matunda katika shamba lake.

Sisi tunajisikiaje tunaposoma, kusikia na kutafakari masomo yetu ya leo? Sisi tunajisikia kuwa taifa teule kama Waisraeli? Tumepewa dhamana ya kutunza shamba. Tumekuwa waaminifu? Je hilo shamba lina matunda? Je sisi tunajisikia kukabidhiwa shamba la mizabibu na kuwa na wajibu wa kulitunza – yaani ufalme wa Mungu na mahitaji yake? Ni kwa kiasi gani tumekuwa waaminifu katika imani, matumaini na mapendo? Katika kuishi maisha ya Kisaakramenti? Katika kuushuhudia ufalme? Matendo yetu ya kila siku yanaakisi imani yetu au tumetenganisha imani na matendo? Je ufalme wa Mungu ambao ndilo shamba lenyewe lililokabidhiwa kwetu liko salama au liko salama kiasi gani? Je Bwana wa mavuno akija atapata matunda? Mungu alimkabidhi mwanadamu ulimwengu ili aendeleze – je ni kwa kiasi gani tunashiriki katika ujenzi wa ufalme wa Mungu tukianzia katika familia zetu, jumuiya ndogo ndogo, kigango, parokia na taifa zima la Mungu?

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.