2017-10-05 07:04:00

Nyanyaso dhidi ya watoto ni uhalifu na kashfa mbele ya Mungu


Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko mjini Roma, kuanzia tarehe 3 – 5 Oktoba 2017 kinaendesha Kongamano la Kimataifa kuhusu ulinzi wa watoto wadogo kwenye ulimwengu wa digitali kwa kwa kuongozwa na kauli mbiu “Utu wa watoto wadogo katika ulimwengu wa digitali”. Ni kongamano ambalo linawashirikisha viongozi wakuu wa Kanisa, Serikali ya Italia; wasomi, wanasiasa, mapadre na watawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Wote hawa wanashirikishana mbinu za kupambana na nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya watoto wadogo kwa njia ya mitandao ya kijamii.

Padre Hans Zollner, Rais wa Kituo cha Kulinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ametoa hotuba elekezi kwa kukazia umuhimu wa kulinda: utu, heshima, ustawi na maendeleo ya watoto wadogo: kiroho na kimwili! Wajumbe wa kongamano hili wanakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 6 Oktoba, 2017 pamoja na kuwasilisha Tamko lao baada ya Kongamano hili. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia alikaza kusema kwamba, tangu sasa Kanisa halitakuwa na msamaha kwa viongozi watakaokamtwa kwenye kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican katika hotuba yake amekazia utu, heshima ya watoto wadogo kuwa ni mambo matakatifu yanayopaswa kulindwa na kuendelezwa na wote. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zimeibuka kwa kasi kubwa kiasi cha kupaka matope maisha na utume wa Kanisa; mateso na mahangaiko makubwa katika maisha, malezi na makuzi ya wahanga wa nyanyaso za kijinsia. Sasa, Kanisa linataka kujikita katika mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo kwa kuwahakikishia ulinzi na usalama wa maisha, malezi na makuzi yao. Hadi sasa kumekuwepo na mafanikio makubwa anasema Kardinali Parolin, hali inayopaswa kuendelezwa katika ukweli na uwazi, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za watoto wadogo.

Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, kuna watoto wanaozaliwa katika ulimwengu wa digitali unaogusa masuala; uchumi, maendeleo na mahusiano ya watu! Kwa bahati mbaya sana, huu ni ulimwengu ambamo pia utu, heshima na haki msingi za watoto wadogo zinavurugwa sana, kiasi cha kutishia malezi na makuzi ya watoto wadogo. Huu ni mfumo unaowatumbukiza watoto wadogo katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mifumo ya utumwa mamboleo na madhara yake; dhuluma na nyanyaso za kijinsia. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete, kulinda na kutetea haki msingi za watoto wadogo. Semina hii iwe ni jukwaa la majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuibua mbinu mkakati wa kuwalinda watoto wadogo; kudhibiti mitandao ya kijamii na huduma itakayodumisha haki, utu na heshima ya watoto wadogo, kwa kuwawajibisha wadau mbali mbali katika sekta ya mawasiliano ya kijamii. Katika nchi zinazoendelea ambazo uchumi wake unasusa sua, bado hata huko kuna watoto wanaozaliwa katika ulimwengu wa digitali; hata huko watoto wanapaswa kulindwa! Hii inatokana na ukweli kwamba, hata katika nchi ambazo zimeendelea bado kuna umaskini mkubwa wa maadili, utu wema na maisha ya kiroho.

Kardinali Parolin anakaza kusema, wajibu wa kwanza wa kuwalinda, kuwalea na kuwafunda watoto wadogo ni ya familia na shule ambamo watapewa elimu makini na kusimamia utu na heshima yao dhidi ya bahari ya mawasiliano yanayokuja kwa njia ya mitandao ya kijamii. Kanisa linapenda kulinda, utu na heshima ya watoto, ili waweze kukua na kukomaa na hatimaye, kufikia utimilifu wa ndoto na maisha yao, kwani hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kuwanyanyasa watoto wadogo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, lakini pia ni kashfa dhidi ya Mwenyezi Mungu. Utu na heshima ya binadamu ni mambo matakatifu sana katika maisha ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.