2017-10-03 14:43:00

Maendeleo ya teknolojia na uwajibikaji katika maisha ya binadamu!


Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha, kuanzia tarehe 5 Oktoba hadi 7 Oktoba, 2017 inaadhimisha mkutano wake wa XXIII, lakini huu ni mkutano wake wa kwanza tangu, Baba Mtakatifu Francisko alipofanya mabadiliko makubwa katika taasisi hii. Kauli mbiu inayoongoza mkutano huu ni “Kusindikiza maisha wajibu katika wakati huu wa maendeleo ya teknolojia”. Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha, Monsinyo Renzo Pegoraro, Mkuu wa Taasisi hii pamoja na Dr. Bernardette Tobin, Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Kimaadili cha Plunkett, kilichoko kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Australia. Hawa ni kati ya “vigogo” wa taasisi hii waliopata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 2 Oktoba 2017.

Mabadiliko yaliyoletwa na Baba Mtakatifu Francisko tangu mwaka 2016 yamepelekea uteuzi wa wasomi kutoka katika nchi 37 duniani; wajumbe wanne wanaoshiriki kwa heshima; wajumbe 45 walioteuliwa na Baba Mtakatifu pamoja na wajumbe wengine 87 wanaoshiriki kwa njia ya mitandao ya mawasiliano ya kijamii. Katika katiba mpya, wameingizwa pia vijana 13 wanaofanya tafiti zao, ili kutekeleza kikamilifu matamanio ya Baba Mtakatifu Francisko katika kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo mintarafu maendeleo ya sayansi na teknolojia kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Changamoto kubwa kwa wakati huu ni kutoa kipaumbele cha kwanza katika uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo unaozinyemelea nchi nyingi Barani Ulaya; kwa kulinda na kudumisha uhai wa binadamu katika hatua zake mbali mbali, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, taasisi hii inakuwa ni jukwaa la majadiliano imani katika ukweli na uwazi kuhusu Injili ya uhai kwa kuzingatia: Imani, Mapokeo na Dini za watu mbali mbali.

Wajumbe wa taasisi hii kwa mwaka huu wanajikita zaidi katika mchakato wa kusindikiza Injili ya uhai katika hatua zake zote; umuhimu wa teknolojia katika maisha ya binadamu; madhara yake yanayoweza kupelekea kutoweka kwa tunu msingi za maisha ya binadamu. Baadaye, Mwezi Novemba 2017 kutafuatia kongamano la Shirikisho la Madaktari Duniani kuhusu nyakati za mwisho za maisha ya binadamu. Huduma ya kutuliza maumivu kwa wagonjwa walioko kufani, Kongamano ambalo litaadhimishwa nchini Russia kwa kushirikiana na Patriaki wa Moscow na Russia nzima.

Kutakupwepo pia na mfululizo wa semina mbali mbali kuhusu Injili ya uhai na Roboti bila kusahau makongamano ya kimataifa yatakayoandaliwa kwa nia hizi. Lengo ni kukabiliana na changamoto zote hizi za kisayansi kwa kujikita katika: utu na heshima ya binadamu; ukweli na weledi kutoka katika medani mbali mbali za uzoefu na mang’amuzi ya kibinadamu! Makumbusho ya Vatican, kuanzia tarehe 6 Oktoba 2017 hadi tarehe 5 Januari 2018 kutakuwepo na onesho la sanaa mbali mbali katika mchakato wa kusindikiza maisha wakati huu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake, Monsinyo Renzo Pegararo, anasema, kipaumbele cha kwanza ni Injili ya uhai katika hatua zake zote; yaani tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ni mkutano unaopembua mambo nyeti katika maisha ya binadamu: tangu kuzaliwa, mahusiano, tamaduni, kifo na mahusiano kati ya teknolojia, haki na rasilimali za uchumi zilizopo mintarafu kanuni maadili zinazowasukuma watu kuwajibika katika kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anabainisha umuhimu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia na madhara yake katika maisha ya binadamu. Maendeleo ya sayansi na teknolojia hayana budi kumsaidia mwanadamu katika mchakato wa maendeleo endelevu: kwa kuwajibika, kwa kuzingatia tunu msingi sanjari na kuongozwa na dhamiri nyofu. Kumbe, mkutano huu ni jukwaa linalopania kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kwa habari zaidi unaweza kutembelea katika mtandao wa taasisi hii kwa anuani ifuatayo:

www.academyforlife.va

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.