2017-10-02 13:25:00

Papa Francisko: watawa dumisheni maisha ya udugu, upendo na huduma!


Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Shirika la kitawa ni wakati muafaka wa: sala na udugu; ni wakati wa kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu, ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto katika maisha na utume wao katika historia. Huu ni wakati wa kufanya tathmini ya kina kuhusu wito wa mtu binafsi na Jumuiya katika ujumla wake. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 2 Oktoba 2017, wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Dada Wadogo wa Yesu.

Hili ni Shirika lililoanzishwa na Mwenyeheri Charles de Foucauld, aliyeonja neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu: mwenye nguvu, Muumba wa mbingu na dunia, lakini aliyethubutu kujinyenyekesha na kuzaliwa kwake Bikira Maria na bado anataka kujisadaka kwa kila mtu katika unyenyekevu na upendo wa dhati hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Katika kipindi cha miaka themanini tangu kuanzishwa kwa Shirika hili, licha ya matatizo na changamoto za maisha katika historia, Shirika limeendelea kutibu na kuelimisha; kutoa katekesi; kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika kazi, uwepo, urafiki na ukarimu usiokuwa na mipaka!

Hii ndiyo dhamana ambayo watawa wa Shirika hili wanapaswa kuikuza na kuidumisha daima katika hija ya maisha yao, kama kielelezo cha kuwa karibu na Mwenyezi Mungu, anayeendelea kujisadaka katika unyenyekevu ili kumkomboa mwanadamu na hatimaye,  kumkumbatia kwa upendo wake wa dhati! Baba Mtakatifu anawataka watawa hawa kukuza na kudumisha tasaufi ya maisha na utume wao kama kielelezo cha upendo wa Mungu kwa jirani zao. Huu ndio ushuhuda wa kiinjili unaobubujika na kusubiriwa kwa mikono miwili na maskini!

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii kuwatia shime watawa hawa kusonga mbele, kwa kuwa huru na kamwe wasijishikamanishe sana malimwengu, ili waweze kuwa huru katika kuwapenda wale wote wanaokutana katika njia ya maisha na utume wao; tayari kushiriki mateso ya ndugu zao katika Kristo Yesu! Wanalazimika kufunga baadhi ya shughuli zao kutokana na uhaba wa miito, upweke na magumu ya maisha yanayowalazimisha kuvuka Jangwani katika hali ya hatari sana. Pamoja na changamoto zote, hizi, bado watawa wanaweza kukumbatia mambo msingi katika maisha na wito wao!

Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa namna ya pekee kabisa, maisha ya udugu ndani ya Jumuiya, kwa kumfuasa Kristo fukara kati ya maskini, ili kuwashirikiha furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Watawa wadumishe umoja, upendo na mshikamano na jirani zao kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Jumuiya inapaswa kusimikwa katika uhalisia wa maisha, upendo na huduma kwa kujaliana na kusaidiana. Ikumbukwe kwamba, uongozi ni huduma inayowajibisha ndani ya Kanisa na inajikita katika utashi wa pamoja na udugu katika kumsikiliza Mwenyezi Mungu; kwa kujiweka katika shule yake, ili kuishi kadiri ya Roho wake Mtakatifu, ili hatimaye, Ufalme wa Mungu uweze kuwafikia watu wengi zaidi. Katika mazingira kama haya, majadiliano na utii vinapata nafasi ya kukua na kudumishwa kama ilivyokuwa kwa Yesu alivyozidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu. Udugu umwilishwe kati yao na watu wa Mataifa kutoka katika kila: dini,lugha, jamaa na taifa pasi na vikwazo, bali daima wawe ni mashuhuda wa mwanga na furaha ya Injili kwa watu wote, lakini zaidi kwa maskini na wanyonge!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.