2017-10-02 10:21:00

Maaskofu na hatima ya vijana Barani Ulaya!


Bara la Ulaya linapaswa kujisikia kuwa kama Mama na mwalimu, anayeweza kufundisha, kuongoza, kukemea na kukanya kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha. Hii ni changamoto endelevu kwa familia ya Mungu Barani Ulaya kupenda na kuthamini dhana ya Jumuiya ya inayowabika barabara. Huu ni mchango ulitolewa na Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya katika mkutano wake wa mwaka, uliokuwa unapembua pamoja na mambo mengine maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana sanjari na hatima ya Bara la Ulaya kwa siku za usoni! Mkutano huu uliokuwa unafanyika huko Minsk, Belarus, umehitimishwa, Jumapili, tarehe 1 Oktoba 2017.

Bara la Ulaya linapaswa kujisikia kuwa ni ukweli unaofumbatwa hata katika maisha ya kiroho licha ya tofauti zake za kiuchumi, kisiasa na kijiografia. Mama Kanisa kwa upande wake anapenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi, maendeleo na haki msingi za binadamu dhidi ya utamaduni wa ubinafsi na mifumo ya ubaguzi!

Maaskofu wamepembua kwa kina na mapana historia ya Bara la Ulaya, kwa miaka iliyopita, hali ya sasa na mwelekeo kwa siku za usoni, kwa kujikita katika mizizi ya Ukristo inayofumbatwa katika kazi na sala; umuhimu wa falsafa; utamadunisho wa Maandiko Matakatifu katika lugha asilia na umuhimu wa wamini kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kama alivyofanya Mtakatifu Edith Stein, chachu ya muungano kati ya Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Huyu ni mtakatifu aliyewafunuliwa watu wengi wa Bara la Ulaya: utukufu wa Fumbo la Msalaba, linalofumbata hekima, huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa binadamu!

Bara la Ulaya haina budi kuendeleza maboresho katika sekta ya elimu na utamaduni itakayowajengea vijana uwezo wa kupambana na changamoto za maisha ya kila siku, badala ya kubweteka na kuanza kuwaonyooshea watu wengine kidole, kana kwamba, wao ni wapita njia tu! Maaskofu wametafakari mawazo, maoni na mapendekezo yaliyotolewa na familia ya Mungu Barani Ulaya, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayofanyika mjini Vatican, mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” ni nafasi ya pekee kwa Maaskofu kuwasikiliza vijana kwa makini ili hatimaye, Kanisa liweze kuibua mbinu mkakati wa utume kwa vijana wa kizazi kipya Barani Ulaya!

Kardinali Vincent Gerard Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales anasema, Maaskofu wanakabiliwa na changamoto kubwa mbele yao mintarafu utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya! Huu ni mwaliko kwa Mama Kanisa kutoka na kuwaendea vijana huko “vijiweni” tayari kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwaelekeza mambo wanayopaswa kuzingatia katika maisha, kama sehemu ya wajibu wao kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Vijana wanakabiliwa na matatizo na changamoto kubwa za maisha: kuanzia katika mahusiano ya kifamilia na kijamii, ambayo yameendelea kuwa tenge tangu mwaka 1968, hali ambayo imewafanya vijana wengi tangu wakati huo kupambana na mifumo ya kijamii kutokana na kukosa matumaini kwa siku za usoni; mwelekeo potofu wa maisha na hali ya kuchanganyikiwa inayowakumba vijana wengi kiasi hata cha kukosa utu na maadili mema.

Mama Kanisa kwa wakati huu anao wajibu wa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza vijana kwa makini, bila kujidai kwamba, anaweza kuyapatia kisogo matatizo na changamoto zinazowakumba vijana wa kizazi kipya katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Matatizo na changamoto za vijana ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa. Kushiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana maana yake ni kujizatiti katika mchakato mzima wa kupanga sera na mikakati ya utume wa vijana; kuwajengea vijana uwezo ili kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa sera na mikakati hii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kutambua kwamba, wao ni wahusika wakuu! Vijana hawana budi kuwa na ndoto ya matumaini kwa sasa na kwa siku za usoni!

Askofu mkuu Eamon Martin, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland, anasema, familia ya Mungu nchini Ireland inaendelea na maandalizi ya kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Dublin, mwezi Agosti, 2018. Wajumbe kati ya 20000 hadi 40000 wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huu ambao unapania pamoja na mambo mengine, kujenga na kudumisha Injili ya familia! Kwa Kanisa nchini Ireland, hii ni fursa makini ya kutafakari kwa kina na mapana utume wa familia: umuhimu, changamoto na fursa zilizopo mintarafu mwanga wa wa Injili na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”.

Kanisa linataka kuweka bayana maana, uzuri na utakatifu wa Sakramenti ya Ndoa kadiri ya: Imani na Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki, muhimu si tu kwa waamini, bali hata kwa jamii nzima ya binadamu! Kwa mara ya kwanza kabisa, Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” utapembuliwa kwa kina na mapana! Itakumbukwa kwamba, kwa siku za hivi karibuni, kumewepo na upinzani na upotoshwaji wa makusudi unaofanywa na baadhi ya waamini kutaka kumpaka matope Baba Mtakatifu Francisko. Ni wakati wa kufafanua dukuduku hizi na hatimaye, kuliwezesha Kanisa kusonga mbele katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia kwa watu wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.