2017-09-28 11:11:00

Mwenyeheri Padre Tito Zeman alisadaka maisha yake kwa utume wa vijana


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi, tarehe 30 Septemba 2017, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko huko kwenye Kanisa kuu la Familia Takatifu, Jimbo kuu la Bratislava, nchini Slovakia, anamtangaza Padre Tito Zeman kutoka Shirika la Wasalesian wa Don Bosco, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kuwa Mwenyeheri. Aliteswa sana kwenye magereza yaliyokuwa yanadhibitiwa na utawala wa Kikomunisti ambao uliliangalia “Kanisa kwa jicho la kengeza”.

Mwenyeheri Padre Tito Zeman katika maisha na utume wake, aliendelea kushuhudia utambulisho wa Kikatoliki nchini Slovakia kwa kusimamia uhuru wa dhamiri, utu na heshima ya binadamu. Wakati huo, shule na taasisi za elimu ya juu zilizokuwa zinamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini humo, zilitaifishwa; wakleri, watawa na waamini walei, wakahukumiwa na “kushikishwa adabu” kutokana na uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Lakini, Padre Tito Zeman na wenzake wengi wakasimama kidete kupinga uonevu kwa njia ya ushuhuda wa Injili ya upendo na huruma.

Kardinali Angelo Amato anasema, Mwenyeheri Padre Tito Zeman alizaliwa huko Bratislava, nchini Slovekia kunako tarehe 4 Januari 1915, akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya watoto kumi waliozaliwa kwenye familia yake. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kunako mwaka 1940. Mara nyingi alivuka mipaka ya nchi na kuingia Italia ili kuhamasisha miito ya kipadre na kitawa. Siku moja, akakamatwa na kutupwa gerezani na tarehe 8 Januari 1969 akafariki dunia. Kunako mwaka 1991 mchakato wa upatanisho ukamtangaza kuwa hana hatia.

Mwenyeheri Padre Tito Zeman alikamatawa na kutiwa nguvuni kwa vile alikuwa anahamasisha miito ya kipadre na kitawa! Akashutumiwa kwa usaliti, akafungwa na kufanyishwa kazi ngumu na za suluba kwenye machimbo ya madini ambayo mionzi yake iliathiri sana afya ya Padre Tito Zeman. Alifanyishwa kazi katika mazingira magumu na yenye baridi kali na kazi ikawa ni mateso na njia ya Msalaba iliyopelekea kifo cha Padre Tito Zeman katika uchungu na mahangaiko makubwa!

Huyu ni shuhuda wa utume wa vijana wa kizazi kipya, aliyejisadaka bila ya kujibakiza, akakubali kuteseka kwa ajili ya kuwahudumia vijana waliokuwa wanajianda kwa ajili ya Daraja Takatifu na kwamba, mateso na suluba havikumtisha hata kidogo, bali yaliyapokea yote kama mapenzi ya Mungu katika safari ya maisha yake kama mfuasi amini wa Kristo na Kanisa lake! Mwenyeheri padre Tito Zeman sasa anajiunga kwenye jeshi kubwa la mashuhuda wa imani kutoka katika Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco waliotangazwa na Mama Kanisa katika miaka ya hivi karibuni, kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kardinali Angelo Amato anasema huduma ya upendo miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni kati ya changamoto kubwa zinazovaliwa njuga na Wasalesiani wa Don Bosco, sehemu mbali mbali za dunia. Wanataka kuwajengea vijana uwezo wa kusimama kidete kulinda na kutetea imani yao dhidi ya sera na falsafa zinazokwenda kinyume kabisa cha tunu msingi za Kiinjili, utu na heshima ya binadamu.

Mwenyeheri Padre Tito Zeman ni shuhuda wa wokovu wa vijana wa kizazi kipya unaofumbatwa katika gharama ya maisha. Ni Padre aliyependa na kuthamini sana wito na maisha yake ya Kipadre na Kitawa; akatamani kuwaona vijana wanaoweza pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hii ni changamoto kwa waamini katika ulimwengu mamboleo kwamba uhuru na umoja ni chanda na pete katika kumwilisha moto wa Injili ya huduma ya upendo na ufuasi kwa Kristo Yesu licha ya magumu, changamoto: dhuluma na nyanyaso wanazoweza kukumbana nazo katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.