2017-09-26 10:27:00

Vatican: Jumuiya ya Kimataifa ijielekeze katika amani na maisha bora


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya mwanadamu wa nyakati hizi, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa; yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Wala hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisilogusa mioyo yao. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza katika ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu kwa kulinda maisha yao na kuhakikisha kwamba, Umoja wa Mataifa unatekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kama inavyobainishwa katika Katiba ya Umoja wa Mataifa.

Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na ulinzi wa: uhai, utu na heshima yao kama binadamu bila kusahau uhuru wa kuabudu na kidini. Hizi ni nguzo msingi za: amani, usalama na maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Chakula na lishe bora; maji safi na salama; kazi bora na salama sanjari na fursa ya kazi na mazingira bora ya kuishi ni sehemu ya haki msingi za binadamu zinazopaswa kuendelezwa na kudumishwa na Jumuiya ya Kimataifa. Athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira ni mambo yanayoachangia sana kuhatarisha usalama, utu na heshima ya binadamu, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Itifaki ya makubaliano ya Paris ya Mwaka 2015 juu ya utunzaji bora wa mazingira na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo mwaka 2017 ni alama za matumaini.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, tarehe 25 Septemba 2017, kwenye mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika majadiliano yanayolenga: kuimarisha amani, maboresho ya maisha ya binadamu na maendeleo endelevu duniani kwa kujikita katika: utu wa binadamu, usawa na mazingira bora! Huu ni mchakato unaowahusisha na kuwakumbatia watu wote. Ili kuweza kufikia mafanikio haya kuna haja ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa; kwa ukweli na uwaminifu, ili kukabiliana na changamoto za maisha. Watu wanapaswa kujengewa uwezo, ili waweze kuwa ni wadau katika mchakato wa maendeleo yao: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Gallagher anakaza kusema, Makanisa yameendelea kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuragibisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowawajibisha wote. Ikumbukwe kwamba: utu na heshima ya binadamu vina mahusiano ya karibu sana na utunzaji bora wa mazingira. Uchafuzi wa mazingira ni chanzo kikuu cha umaskini, vita, ghasia sanjari na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika sera makini zinazopania kuzuia uharibifu na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote; kwa kuheshimu na kudumisha haki msingi za binadamu; kwa kujenga na kuendeleza utamaduni wa amani duniani. Mauaji ya kimbari, ukabila, udini, ubaguzi na mifumo mbali mbali ya nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu ni mambo ambayo hayakubaliki na Jumuiya ya Kimataifa.

Utawala wa sheria na sheria za kimataifa ni mambo yanayohitaji utekelezaji ili kudumisha amani na usalama kati ya watu wa Mataifa. Vita na ghasia huko Mashariki ya Kati, DRC na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati; kinzani na migogoro kati ya Israeli na Palestina. Kuna biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; rushwa na ufisadi; biashara haramu ya silaha na vitendo vya kigaidi ni mambo ambayo yanakwamisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, ulinzi na usalama. Amani ya kudumu ndiyo msingi thabiti wa maendeleo ya binadamu yanayofumbatwa katika haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu.

Vita inawapora watu haki zao msingi kiasi cha kuwageuza kuwa wakimbizi na wahamiaji; inasababisha umaskini mkubwa wa hali na kipato na inachangaia uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote! Ni matumaini ya Vatican kwamba, Mkataba wa Kimataifa juu ya Usalama wa Wakimbizi utaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuratibu changamoto hii kwa ufanisi mkubwa kwa njia ya ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja, huku: utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji zikipewa kipaumbele cha kwanza.

Juhudi hizi hazina budi kwenda sambamba na mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu sanjari na mifumo yote ya utumwa mamboleo; rushwa na ufisadi; kwani yote haya anasema Baba Mtakatifu ni ”madonda makubwa ya binadamu katika ulimwengu mamboleo” yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waathirika wa majanga haya wanapaswa kuponywa na kusaidiwa ili waweze kuandika ukurasa wa matumaini mapya katika maisha yao!

Biashara haramu ya silaha duniani imekuwa ikipigwa vita vya maneno, lakini viwanda vinaendelea kutengeneza na kuuza, kiasi cha kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kwa dhati Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku matumizi ya silaha za kinyuklia. Lakini, bado kuna vitisho vya utengenezaji, majaribio na matumizi ya silaha za kinyuklia, kama inavyoshuhudiwa huko Korea ya Kaskazini. Utashi wa kisiasa na utekelezaji wa maazimio ya Jumuiya ya Kimataifa ni jambo ambalo linapaswa kupewa uzito wa pekee kwa viongozi kuaminiana, kuheshimiana na kuthaminiana. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher anahitimisha hotuba hii tete kwa kusema umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa amani na kuachana kabisa na utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.