2017-09-22 17:38:00

Jitahidini kuutafuta Ufalme wa Mungu na wala si fedha! Mtafedheheka!


Mfano wa vibarua wa saa moja katika injili ya leo daima umezua minongono kuhusu bwana (asiyetoa haki sawa) mwenye shamba anayelipa ujira sawa kwa vibarua katika shamba lake pamoja na kwamba kila mmoja aliajiriwa kwa wakati na muda tofauti. Kama malalamiko haya yakikubalika kibinadamu basi kibiblia tutapingana na sehemu ya maandiko katika Rum. 2:6 – yasemayo; atamlipa kila mtu kadiri ya matendo yake. Ieleweke wazi kuwa ujira wa kweli hapa kwa wote kadiri ya Yesu ni ufalme wa mbinguni ambao Yesu ameuleta hapa duniani, yaani uwezekano wa wote kushiriki katika ufalme wa mbinguni. Tunaona wazi kuwa sehemu hii ya injili ya leo inaanza hivi; kwa maana ufalme wa mbingu umefanana na mwenye shamba….. na kwa hiyo basi lengo hapa ni kuupata huo ufalme na si dinari.

Mhubiri maarufu Padre Munachi anaelezea andiko hili akitumia mfano wa familia ya wakulima ambao baba na watoto wakubwa wa kiume huamka mapema kuwahi shambani. Mama hubaki nyumbani akiandaa chai na kusafisha nyumba. Shughuli hizo zikikamilika basi mama na wale watoto wadogo huwafuata wakubwa shambani wakiwapelekea chakula na maji. Kwa kawaida watoto wakifika shamba huendelea na michezo ya kitoto mpaka kwisha muda wa kazi. Muda wa kazi ukiisha kwa pamoja hurudi nyumbani. Mavuno yakitoka wote hushiriki sawa bila kubaguana kadiri ya utendaji. Hapa hakuna anayedai ujira zaidi ya mwingine.

Tukirudi katika injili yetu ya leo inaonekana wazi kuwa wapo watu wa aina mbalimbali kama wasio na kazi, wasiosikiliza habari mpya na maelekezo yanayotolewa katika kupokea majukumu n.k.  Hata hivyo haina maana kuwa wataachwa mbali au watakuwa daraja la pili katika ufalme wa mbinguni. Angalisho la Yesu kwamba wa kwanza watakuwa wa mwisho na wa mwisho wa kwanza litupe changamoto pia. Kinachotakiwa hapa ni kujua vizuri maana ya mfano huu wa Yesu. Hatuna budi kujua vizuri mapenzi ya Mungu juu ya ufalme wake hapa ulimwenguni. Tunatakiwa tuelekeze uelewa wetu kadiri ya fundisho husika na si kadiri tunavyotaka kuelewa sisi wenyewe kama wale vibarua wa saa ya asubuhi. Katika mfano twaona kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kuita ye yote na kwa wakati wo wote kadiri atakavyo. Sisi tumepewa nafasi katika ufalme wa mbinguni na kwa hali hiyo basi mahangaiko yetu yawe katika wito huo na si katika kitu kingine cho chote, si katika malipo. Baba Mtakatifu Yohani Paulo II katika waraka “Christifidelis Laici – no. 1-2 –“ Wito wa Utume wa Walei katika Kanisa na Ulimwengu – anasema walei wanafanya ule ufalme unaowakilishwa na wafanyakazi katika shamba la mizabibu – nendeni shambani.

Katika somo la injili tunaona makundi matatu ya watenda kazi katika shamba lile lile ila kwa muda tofauti. Wale wa mapema asubuhi walipewa mkataba wa kazi na malipo na kiasi kinatajwa, dinari moja. Waliokuja baadaye walifanya kazi wakiamini katika neno la mwenye shamba – Mt. 20:4 …. iliyo haki yenu nitawalipa na wale walioajiriwa saa za jioni hawakuambiwa cho chote kuhusu malipo – 20:6-7 ….waliambiwa waende shambani kufanya kazi. Hakuna mkataba wo wote hapa. Ni swala la uaminifu tu. Sehemu hii ya Injili yatuonesha kuwa Mungu si tu mwenye haki bali pia ni mwema, mkarimu na mpole. Ufalme wa Mungu unajengwa kama familia yenye kushirikiana na si yenye ushindani. Tunachagizwa kuelewa vizuri masharti ya kuupata huo ufalme wa Mungu.

Pia tunaambiwa kuwa tusihoji ukubwa wa upendo wa Mungu bali tufurahie neema yake. Hakuna mwenye haki ya kujivuna zaidi. Tunachoona kutoka kwake Mungu ni huruma, msamaha, ukarimu na upendo. Sisi tunaalikwa kutangaza kwa nguvu zetu zote hiyo injili ya Kristo kama anavyotuasa mtume Paulo katika somo la pili. Habari hii ya huruma na upendo wa Mungu ipo wazi katika somo la kwanza na zaidi sana mwanadamu anatakiwa kuacha dhambi. Nabii Isaya anaandika wakati watu au taifa la Israeli wakiwa wamerudi toka utumwani, wamekata tamaa, wakidhani kuwa Mungu amewaacha, ila nabii anawaambia kuwa Mungu bado yuko nao na yuko karibu nao. Sisi nasi hatuna budi kutambua kuwa Mungu na ufalme wake upo kati yetu na ni wajibu wetu kutenda au kujibu mapenzi hayo kwa kushiriki kwa uaminifu katika ujenzi wa huo ufalme.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.