2017-09-21 16:57:00

Nishati ya atomic isaidie kupambana na umaskini na kuboresha maisha!


Padre Bruno Marie Duffè, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu, akichangia hoja kwenye mkutano mkuu wa 61 wa Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomic, IAEA, amewapongeza wakala hawa kwa mchango wao katika mchakato wa kudhibiti utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha ya kinyuklia katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu kwa njia ya ushirikiano wa kimataifa. Nishati ya atomic inapaswa kutumiwa kwa ajili ya maendeleo na wala si kuwa ni chanzo cha majanga kwa watu na mali zao.

Padre Duffè anasema kuna uhusiano wa karibu sana kati ya udhibiti wa utengenezaji, matumizi, usambazaji na ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia na upigaji rufuku wa silaha hizi, kwa ajili ya mchakato wa kujenga na kudumisha amani na utulivu duniani. Vatican inaendelea kufuatilia kwa umakini mkubwa malumbano ya kijeshi na majaribio ya makombora ya masafa marefu yanayorushwa na Korea ya Kaskazini na kwamba, Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomic anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake. Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono Mkataba wa Kimataifa unaopiga Rufuku Silaha za Kinyuklia, kama sehemu ya hatua muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia.

Padre Duffè anakazia umuhimu wa kuwajengea uwezo mkubwa zaidi Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomic ili uweze kutekeleza wajibu wake barabra kwa kuwezesha matumimizi rafiki ya nishati ya atomic kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu. Mchango wa IAEA katika miradi ya ushirikiano wa kimataifa umesaidia sana katika maboresho ya afya na tiba ya binadamu, kilimo, lishe, usalama wa chakula, afya ya wanyama; udhibiti wa wadudu waharibifu; maji safi na salama ya kunywa; ulinzi na utunzaji bora wa mazingira; mambo ambayo pia yamesaidia katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini duniani kwa kukoleza maendeleo endelevu ya binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, matumizi ya nishati ya atomic yana athari zake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani. Ni upotevu mkubwa wa rasilimali fedha na nguvu kazi ambayo ingeweza kutumika kwa ajili ya kuchangia maendeleo makubwa zaidi ya binadamu hasa katika maboresho ya elimu, afya na mapambano dhidi ya umaskini duniani. Padre Duffè anapenda kukazia umuhimu wa ulinzi na usalama; kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani pamoja na ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya ulinzi na usalama. Kanuni maadili katika uwajibikaji wa kimataifa, mshikamano na ushirikiano ni mambo yanayopaswa kudumishwa badala ya kujikita katika sera na falsafa za kutenga baadhi ya mataifa kwa ajili ya mafao binafsi na hofu zilizokuwa na mashiko wala mvuto. Ulinzi na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa ni mchakato unaowategemea watu wote. Ujumbe wa Vatican unapenda kuwahimiza wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kukazia mchakato wa upigaji rufuku: utengenezaji, ulimbikizaji, usambazaji na matumizi ya silaha za kinyuklia. Juhudi za makusudi zinapaswa kuelekezwa katika matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu ya binadamu, hususan kwenye nchi change zaidi duniani, ili kukuza na kudumisha amani ya kudumu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.