2017-09-20 07:26:00

Padre Stefanizzi: Miaka 100 ya maisha; Miaka 50 ya hapa kazi tu!


Padre Antonio Stefanizzi, Myesuit, aliyewahi kuwa Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican, tarehe 18 Septemba 2017 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa yaani tarehe 18 Septemba 1917 huko Lece, Kusini mwa Italia. Baba Mtakatifu Francisko ametumia nafasi hii kumtakia heri na baraka pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyemkirimia karama mbali mbali katika maisha na utume wake, akafanikiwa kuzimwilisha katika mawasiliano ya jamii. Padre Stefanizzi mtaalam wa hesabu na fisikia, kwa muda wa miaka 50 amejisadaka kwa ajili ya huduma ya mawasiliano mjini Vatican.

Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican akiwa ameambatana na Monsinyo Lucio Adrian Ruiz, Katibu wa Sekretarieti wamemtembelea Padre Antonio Stefanizzi ili kumpelekea salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, kwa kuwawezesha viongozi wa Kanisa kufikisha ujumbe kwa watu wengi zaidi kwa njia ya mawasiliano ya jamii. Kwa upande wake, Padre Antonio Stefanizzi anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kutekeleza utume wake; amewatia moyo viongozi wakuu wa Sekretarieti ya mawasiliano kusonga mbele katika utekelezaji wa mageuzi katika vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatica, daima kwa kusoma alama za nyakati.

Alitumia karama na mapaji yake kwa ajili ya kusaidia kuhariri nyaraka za Papa Pio XII zilizokuwa zinarushwa hewani kwa njia ya Radio Vatican. Ilikuwa ni Mei Mosi, 1955 Papa Pio XII alipotangaza rasmi kwamba, Mtakatifu Yosefu, tangu siku hiyo ni msimamizi wa wafanyakazi duniani, ujumbe ambao ulitangazwa moja kwa moja na Radio Vatican.

Padre Federico Lombardi, aliyewahi kuwa Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican na Msemaji mkuu wa Vatican anakiri kwamba, miaka 100 si haba. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre 7 Julai 1946. Akaendelea kufundisha na kujinoa sehemu mbali mbali katika masomo ya sayansi. Kati ya Mwaka 1951- 1953 akapewa dhamana ya kufundisha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, hadi tarehe 29 Machi 1953 alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican.

Tangu wakati huo, akashiriki katika sera na mikakati mbali mbali iliyoiwezesha Radio Vatican kurusha matangazo yake kwa ufanisi mkubwa kwa kutumia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya wakati huo! Itakumbukwa kwamba, Vatican ni kati ya nchi kumi na moja waasisi wa Satellite, kunako mwaka 1964. Kunako mwaka 1992 Vatican  akafanikiwa kurusha matangazo ya Radio Vatican kwa njia ya Satellite. Tangu wakati huo, ujumbe wa Baba Mtakatifu, salam na baraka za Noeli na Mwaka Mpya maarufu kama Urb et Orb zimekuwa zikirushwa na Radio Vatican sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya Radio Vatican, Kituo cha Televisheni ya Taifa la Italia, RAI na baadaye huduma hii ikaendelezwa na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV. Huduma hii kwa mara ya kwanza ilitolewa kunako tarehe 24 Desemba 1974 wakati Mwenyeheri Paulo VI alipozindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu.

Kunako mwaka 1989 alishiriki kikamilifu katika mchakato wa kuanzisha Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV. Kunako mwaka 1997 Padre Antonio Stefanizzi akang’atuka kutoka madarakani na kuwaachia vijana kuchapa kazi, baada ya kuweka msingi thabiti wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano kwa ajili ya Kanisa la Kristo. Padre Antonio Stefanizzi na baadhi ya Wayesuit walikuwa wanaishi katika nyumba ambayo baadaye ilibomolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II ili kujenga Monasteri ya “Mater Ecclesia” ambayo kunako mwaka 2013 iligeuzwa kuwa ni Makazi mapya ya Papa mstaafu Benedikto XVI.

Padre Antonio Stefanizzi anasema, dhamana na utume wake katika umri wa miaka 100 ni kuendelea kusali kwa ajili ya kuliombea Kanisa, Shirika lake pamoja na kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na Fumbo la Kifo, tayari kukutana na Kristo Yesu, Hakimu mwenye huruma na haki. Katika maisha yake, amejitahidi kumtumikia Kristo Yesu kwa njia ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni matumaini yake kwamba, ameitekeleza dhamana hii kwa uaminifu mkubwa, kadiri ya uwezo n anafasi aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.