2017-09-18 10:09:00

Papa Francisko: huruma na msamaha ni mafundisho makuu ya Yesu


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XIV ya Mwaka A wa Kanisa inajikita hasa katika dhana ya msamaha, kiini cha mafundisho ya Yesu anayetambua udhaifu wa binadamu katika maisha yake, ingawa ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Binadamu daima ataendelea kutenda dhambi, ndiyo maana Yesu anamjibu Petro mtume, kwamba, anapaswa kusamehe daima na kwamba, msamaha hauna kikomo katika maisha ya mwanadamu. Yesu anafafanua mafundisho yake kwa mfano wa Mfalme mwenye huruma aliyemsamehe mtumwa wake deni kubwa ambalo lingemgharimu maisha yake na yale ya familia yake katika ujumla wake. Akamsamehe yule mtumwa katili, lakini akashindwa kutoa msamaha kwa mtumwa mwenzake!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 17 Septemba 2017 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kiasi kile cha fedha kilikuwa ni kikubwa sana kwa yule mtumwa kuweza kukilipa, lakini kwa bahati mbaya yule mtumwa katili, hakuweza kuonesha wema na huruma kwa mtumwa mwenzake, licha ya kumwomba msamaha wa deni, ile ndogo aliyokuwa anadaiwa! Bila huruma wala upendo, akamtupa gerezani hadi pale atakapolipa deni lake lote!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, pengine watu wa nyakati hizi wanashangazwa na ukatili wa mtumwa yule, lakini hii ndiyo hali halisi ambayo inawakumba hata watu wa nyakati hizi, ambao ni wagumu kuomba na kutoa msamaha wa kweli. Mfalme mwenye huruma anayezungumziwa katika Injili ni mfano wa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, anayethubutu kusamehe kila wakati, lakini pia anawataka waja wake, kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma. Kwa wale wote walionja na kuguswa na ile furaha, amani na uhuru wa ndani baada ya kusamehewa dhambi na makosa yao wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa msamaha na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, Sala kuu ya Baba Yetu, Yesu ameingiza fundisho hili kuu, ili wale wanaothubutu kuomba msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wawe tayari hata wao kuwasamehe jirani zao. Msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni kielelezo cha upendo kwa waja wake, kila mara wanaporejea tena kwa toba na wongofu wa ndani, ili kupata msamaha na maondoleo ya dhambi zao.

Huu ndio upendo wa dhati kabisa, uliomwezesha, Mchungaji mwema kuwaacha kondoo 99 na kwenda kumtafuta kondoo mmoja aliyekuwa ametokomea msituni! Hiki ni kielelezo cha wema, upole na huruma ya Mungu kwa wadhambi wanaotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Baba wa mbinguni ni mwingi wa huruma na mapendo anayewataka waja wake kujivika msamaha, ili kuwakirimia wale wanaoomba msamaha huo kutoka kwao, kamwe wasiwafungie malango ya mioyo yao wale wote wanaokimbilia na kuomba msamaha kutoka kwao. Mwishoni kabisa, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Bikira Maria ili awasaidie kuona umuhimu wa kujisadaka na ukuu wa msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili hata wao, waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa watu wa Mataifa. Mwenyezi Mungu ni mwema, ni mwingi wa huruma na mapendo, si mwepesi wa hasira.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu alitambua uwepo wa waamini na mahujaji kutoka ndani na nje ya Italia. Lakini, kwa namna ya pekee amewataja washiriki wa mbio za Marathoni kwa ajili ya kuombea amani duniani kwa kupitia katika maeneo na nyumba za Ibada za dini mbali mbali zilizoko hapa mjini Roma. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, tukio kama hili la michezo na utamaduni, litaweza kukuza na kuimarisha majadiliano, amani na utulivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.