2017-09-18 09:55:00

Papa Francisko anaihamasisha Colombia kujikita katika amani!


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, amehitimisha hija yake ya kitume nchini Colombia ambayo imekuwa na mafanikio makubwa katika maisha na utume wa Kanisa nchini Colombia. Sasa ni wakati wa kumwilisha yale yaliyopandikizwa katika akili na sakafu ya nyoyo za watu wa familia ya Mungu nchini Colombia ili kwa pamoja waweze kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani na upatanisho wa kitaifa, kila mwananchi akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake kadiri ya nafasi na dhamana yake ndani ya jamii.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko imekuwa ni chachu ya upatanisho wa kitaifa katika ukweli na amani. Imewahamasisha waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia inayosimikwa katika Injili ya uhai na amani dhidi ya utamaduni wa kifo. Waamini wamekumbushwa kwamba, mchakato wa uinjilishaji mpya unajikita katika ufuasi na utume unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni wajibu wa familia ya Mungu nchini Colombia kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu dhidi ya utumwa mamboleo unaonyanyasa na kudhulumu utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia linasema, Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha wananchi wote wa Colombia kuvunjilia mbali mambo yote yanayosababisha vita, ghasia na mipasuko ya kijamii, ili kuanza mchakato wa uvunaji wa matunda ya haki, amani na upatanisho, ili kwa pamoja waweze kufanya hija inayopania kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, utulivu na udugu. Hija ya Baba Mtakatifu nchini Colombia imekuwa ni kipindi cha neema na baraka na kwamba, sasa ni wakati wa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji ili kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia kwamba, ujumbe na mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko utaweza kupenya na hatimaye, kuleta mabadiliko makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu nchini Colombia. Hiki kitakuwa ni kielelezo makini cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu katika miji ile yote ambayo imebahatika kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Colombia. Jumapili, tarehe 17 Septemba 2017 familia ya Mungu nchini Colombia imeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufanikisha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia na kumwomba, awajalie ari na mwamko wa kupiga hatua mbele katika utekelezaji wa mchakato wa amani na upatanisho nchini mwao.

Askofu mkuu Oscar Urbina Ortega, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia anasema, Baba Mtakatifu amewaachia changamoto kubwa katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa; mambo yanayofumbatwa katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni wakati wa kujikita katika majadilino katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuweka kando ubinafsi, uchu wa mali na madaraka pamoja na tabia ya baadhi ya watu kujitafuta wenyewe. Ni muda wa kusimamia kanuni maadili na utu wema kwa kukataa kishawishi cha kuwatumbukiza tena wananchi wa Colombia katika vita, ghasia na mipasuko ya kijamii “isiyokuwa na kichwa wala miguu”. Ushuhuda wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko uwe ni chachu ya mabadiliko katika maisha ya wananchi wa Colombia.

Askofu mkuu Ettore Ballestrero, Balozi wa Vatican nchini Colombia anakaza kusema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia imekuwa ni chemchemi ya furaha, amani na matumaini yanayosimikwa katika dhamana ya uwajibikaji mkubwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Colombia. Ujumbe wa Baba Mtakatifu ni chachu ya ujenzi wa msingi wa haki, amani, upendo, umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko amekiri na “kuwavulia kofia” wananchi wa Colombia kwa wema, ukarimu na matumaini! Colombia imeonesha na kushuhudia utajiri wake unaofumbatwa katika rasilimali watu, tamaduni na mapokeo; imeonesha ukomavu na uwajibikaji kiasi hata cha kuwa ni bandari ya ukarimu na utulivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.