2017-09-16 09:23:00

Msamaha na upatanisho katika kweli na haki ni chemchemi ya furaha!


Msamaha, upatanisho katika kweli ni haki ndicho kiini cha Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXIV ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, tema ambayo inabubujika kutoka katika Sala kuu ya Baba Yetu: Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe waliotukosea. Jumapili ya XXIII ilitupatia mambo msingi ya kutuongoza katika mchakato wa kusahihishana kidugu katika ukweli na mapendo. Msamaha ni kipimo cha kanuni maadili mintarafu Injili ya Kristo Yesu, tofauti kabisa na tabia ya kulipizana kisasi kwa sera za “jino kwa jino; jicho kwa jicho”, kiasi hata cha kufikia wakati watu kuanza kunoa mapanga! Hii ni hatari kubwa sana kwa ulimwengu mamboleo, kwani kukosa na kukoseana ni ubinadamu, kusamehe na kupatana ni mchakato wa utakatifu wa maisha.

Kristo Yesu anaonesha dira na mwelekeo mpya katika maisha kwa kusema kwamba, msamaha hauna kikomo, kwani hii ni fadhila inayopaswa kumwandama mwanadamu katika maisha yake yote! Hii ndiyo tabia ya Mwenyezi Mungu kusamehe daima pasi hata na kuchoka kwa wale wote wanaomwendea kwa moyo wa toba na majuto ya kweli. Huu ndio ujumbe mzito aliotuachia Kristo Yesu alipokuwa pale Msalabani, alipowaombea msamaha watesi wake, kwa kusema, hawajui walitendalo!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, aliwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kati ya watu wa Mataifa, kwani huruma na msamaha ni kiini  cha imani na Injili ya Kristo, chemchemi ya furaha na faraja ya Mungu kwa waja wake. Huruma na msamaha ni utambulisho wa watoto wa Mungu na sehemu muhimu sana ya ushuhuda wa upendo. Msamaha una nguvu inayoleta uponyaji wa ndani katika maisha ya mwamini. Msamaha humweka mtu huru na kuanza mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati katika ukweli. Hii ni chemchemi ya matumaini ya maisha mapya!

Lakini kwa bahati mbaya, nguvu ya msamaha inahifadhiwa katika vyombo vya udongo, inahifadhiwa katika mikono dhaifu ya binadamu, ambaye daima hasira, gadhabu, kisasi na ukatili vinamandama kiasi hata cha kukosa furaha, amani na utulivu wa ndani. Huu ni mwaliko wa kujikita katika Heri za Mlimani, na hasa zaidi ile inayosema, “Heri wenye huruma maana hao watahurumiwa, kwani huruma na msamaha wa Mungu ndicho kiini cha mahangaiko na upendo wake kwa binadamu. Msamaha unapaswa kuwafikia na kuwagusa watu wote pasi na ubaguzi. Katika Injili ya leo, Yesu anamwonesha Bwana aliyemfutia mtumwa wake deni kubwa ambayo hasingeliweza kuilipa, lakini kwa bahati mbaya, yule “mtumwa katili” hakuwa hata na chembe ya huruma kwa jirani yake!

Yesu anahitimisha sehemu hii ya Injili kwa kusema “Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake” (Re. Mt. 18:35). Mwenyezi Mungu yuko tayari kusamehe, lakini mwanadamu yuko tayari kulipiza kisasi. Changamoto kubwa ni kusamehe kaba Baba Yetu wa mbinguni, mkazo unaotolewa na Kristo Yesu. Msamaha ni kioo cha upendo kwa jirani, kwani mwamini anapatia neema ya kuweza kuvaa miwani mipya ya kuweza kumwona jirani yake kama ndugu na wala si kama adui. Msamaha unaratibu machungu ya moyo, ndiyo maana msamaha kwa lugha ya Kilatini unaitwa “Misericordia” kwa kuundwa na maneno makuu mawili “Miserior” yaani “Huruma” na “Cordis” yaani “moyo”. Ukiunganisha maneno yote mawili unapata  neno “Moyo wenye huruma”. Kumbe, huruma inapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu. Na tunaambiwa kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo na wala si mwepesi wa hasira, kwani anatambua udhaifu na unyonge wa binadamu.

Paulo Mtume, anawaandikia Wakolosai akiwataka kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu na kuchukuliana; na kusameheana kama wao pia walivyosamehewa na Mwenyezi Mungu; wajivike upendo ambao ni kifungo cha ukamilifu. Kuna haja ya kuendelea kukazia huruma, upendo na msamaha katika maisha ya mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake, kwani hali na mazingira ya sasa kwa sehemu kubwa yanaunda mazingira ya kutaka kulipizana kisasi. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia ilijikita katika mchakato wa amani na upatanisho unaofumbatwa katika ukweli na haki; chemchemi ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Colombia walitwangana wao kwa wao kwa muda wa miaka 54. Hata leo hii Barani Afrika hatuwezi kusahau vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Angola, Msumbiji na Afrika ya Kusini. Bado kuna madonda na makovu makubwa ya uchaguzi mkuu uliopita nchini Kenya, hali inayohitaji mchakato wa msamaha, upatanisho na ujenzi wa umoja wa kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hivi karibuni katika tamko lake lina laani vurugu, mauaji na uvunjifu wa amani. Wanaiombea Tanzania iweze kuwa na amani na utulivu, tunu ambazo ni matunda ya haki, uhuru na kuheshimiana. Msamaha na upatanisho ni sawa na chanda na pete; tunu zinazowawezesha watu kusimamia haki msingi za binadamu; kukosoana katika ukweli na uwazi; udugu na amani.

Hata Yesu katika maisha na utume wake alipambana sana, lakini alikuwa tayari kusamehe. Tuwe wepesi wa kukimbilia na kuambata msamaha unaofumbatwa katika huruma na mapendo; katika haki na kweli, kwa kutambua kwamba, Kanisa Barani Afrika ni chombo cha haki, amani na upatanisho wa kweli! Tukimbilie katika Mahakama ya huruma ya Mungu inayomwondolea mwamini dhambi zake na hivyo kuwa ni chemchemi ya huruma inayotakasa; huruma inayofariji, huruma inayosamehe na kupyaisha tena maisha ya mwamini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.