2017-09-14 10:07:00

Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe jirani zetu!


Sehemu ya Sala ya Bwana inatupatia wajibu wa msamaha kwa wenzetu. Hapo huwa tunamwomba Mungu tukisema “utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea”. Hitaji letu la uponyaji kutoka kwa Mungu linawekewa sharti na sisi wenyewe tunaoomba msamaha. Kristo anatufundisha njia hiyo njema kwani anatambua kwamba msamaha unapaswa kuiponya nafsi yangu na ya jirani yangu. Wazo hili la Dominika hii ni muendelezo wa Dominika iliyopita ambapo tulipata furasa ya kutafakari jinsi ya kupatana kidugu.

Amri za Mungu zipo kumi na kila moja ina umuhimu wake katika mahusiano yetu na Mungu. Ni vigumu sana kujidai kwamba kamwe hatuhanguki katika kuivunja amri moja kwa namna moja au nyingine. Lakini katika mazingira haya Mungu wetu ni mwema na tunapomkimbilia mithili ya mtumwa anayeomba msamaha Yeye ambaye wimbo wa Zaburi umemtaja kama “mwema na mwingi wa huruma” hutusamehe. Je, sisi kwa upande wetu tunatenda vipi pale tunapojiwa na waliotukosea? Kwa nini tunayageuka maneno ya sala yetu kwamba tusamehewe kwani nasi tunawasamehe wenzetu?

Sharti la msamaha kutoka kwa Mungu kwamba nasi tuwasamehe wenzetu ni kubwa lakini ni la lazima. Kristo anatuambia tunapaswa kusamehe daima na si kwa kuhesabu kwani Mungu naye haesabu maovu yetu. Mzaburi analia mbele ya Mungu akisema: “Bwana kama wewe ungehesabu maovu yetu nani angesimama?” Sasa sisi tunabaki kuhesabu maovu ya wenzatu na kuwa wazito kutoa msamaha ili hali tunahitaji msamaha wa Mungu. Lakini sisi wanadamu mara nyingi tunashindwa kusamehe kadiri tunavyohitaji nasi kusamehewa. Tunasahau kwamba “mkuki mtamu ni mtamu kwa nguruwe lakini kwa mwanadamu ni mchungu”.

Tukiitafakari kwa kina sababu ya Mungu kutusamehe tutaiona mantiki yake ya kutaka nasi kuwasamehe wenzetu. Yeye aliye mkamilifu hakunuia mwanadamu kuingia katika uharibifu. Sisi tumeingia katika dhambi sababu za hila za shetani kusudi atuondoe katika uhusiano na Mungu. Lakini Mungu wetu daima ni mwema na mwingi wa huruma. Daima anatutafuta na kutuondoa katika shimo la dhambi na kuturudisha kwake. Tendo hili la upendo wa Mungu halibagui. Yeye hutaka kuturudisha wote na hivyo anaposamehe huyu hamtengi au kumwacha yule. Msamaha wangu kwa wengine huwafungulia kwa Mungu, humrudisha ndugu yangu na sote tunaendelea kuishi katika hali ya umoja wa kindugu.

Kitendo cha wewe kushindwa kumsamehe mwenzako kinaathiri msamaha wa Mungu kwa mwenzako kwani unapomkosea mwenzako unamkosea na Mungu pia. Sasa yeye aliyekukosea anapotamani msamaha wa Mungu atakwamishwa na kugoma kwako kumsamehe na hapo ndipo tutakapoona kikwazo hata Mungu kushindwa kukusamehe na wewe. Msamaha tunaoupata kutoka kwa Mungu unaturudisha kundini na kutufanya sote kuwa ndugu. Ni vigumu kudhihirisha huu undugu unaojipambanua katika umoja kama nasi tunashindwa kupatana. Msamaha wa Mungu unatumiminia upendo wake ambao unadai kupenya na kusambazwa kwa wengine.

Yoshua bin Sira anashangaa ni jinsi gani mtu ambaye anatunza hasira, vinyongo na visasi kwa mwingine anaweza kwenda kuomba msamaha kwa Mungu. Anaiasa hadhira yake kwa kuwaelekeza kusameheana kwani kwa njia hiyo kutawafanya sala zao kusikilizwa na kuondolewa dhambi zao. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inatutaka tujitafakari kama kweli tunajua maana ya tendo la msamaha; tunakumbushwa kwamba msamaha unarudisha upendo ambao hufukuzwa na dhambi. Lakini upendo wa kimungu haubagui na pia unadhihirika katika mahusiano yetu sisi kwa sisi katika upendo.

Mtume Yohane anasema: “Yeye asemaye kwamba yupo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa… Mtu akisema, nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona”(1Yoh 2:9; 4:20). Upendo na chuki havichangamani. Hatuwezi kuutafuta upendo wa Mungu wakati tumejaa chuki mioyoni mwetu. Mungu anakusamehe na kutaka kukutuma nawe uwe mjumbe wa msamaha. Huruma ya Mungu kwetu inatupatia wajibu wa kuwa mitume wa huruma ili jumuiya yote ya wanadamu imulikwe na upendo wake.

Katika hali yetu ya kibinadamu huwa tunatawaliwa na uchovu au kupima kiwango cha msamaha. Mara nyingine huwa tunaweka hata masharti kwamba “nitakusamehe kama utatimiza hiki au kile”.  Kristo anatufundisha katika Injili kusamehe bila kipimo. Hii ni mantiki ya upendo wa kimungu ambao unasamehe yote bila kujali ukubwa wa kosa. Mtumwa anayeshindwa kusamehe ni mfano kwetu. Anashindwa kusamehe kiasi kidogo cha deni kwa mwenzake ukilinganisha na kiasi alichosamehewa yeye. Kilio chake kuomba msamaha kilitawaliwa na ubinafsi wa kutaka hali njema kwake tu bila kujali hali ya jirani yake. Kwa hakika hii ndiyo hali inayojitokeza katika jamii yetu leo hii iliyojaa chuki, visasi, uhasama na ukandamizaji.

Talanta elfu kumi ni kipimo ambacho kinaweza kulinganishwa na takribani kilo 35 za vito vya thamani. Ni deni kubwa ambalo ni vigumu kwa mtu wa kawaida kulilipa. Uzito huo haukuweza kufidiwa kirahisi kiasi cha kuifanya familia nzima kuwekwa kizuizini. Kipimo hicho kinaonesha ukubwa au uzito wa dhambi zetu mbele ya Mungu. Lakini kwa upendo mkubwa wa Mungu anamtuma Mwanae wa pekee na anakuwa kifidio cha deni hilo (Rej 1Yoh 4:10). Dhambi yote inafutwa na kufanywa huru. Lakini sisi wanadamu tumekosa uaminifu katika upendo huu. Pamoja na kusamehewa kwa kiasi kikubwa na Mungu, Yeye anayetusamehe bila kujali ukubwa wa kosa sisi huwa tunapima na kushindwa kusamehe hata gramu moja ya deni letu. Tunawasweka wenzetu katika gereza la chuki, visasi, laana, ukandamizaji na uhalifu wa aina mbalimbali wa kidunia.

“Ndiyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake”. Tuhitimishe tafakari yetu kwa kutazama tendo hilo la kusamehe kwa moyo. Hii inatuelekeza si katika kusamehe juu juu tu au kufunika kombe ili mwanaharamu apite, bali ni kuingia ndani katika kati nafsi yako na kuondoa hasira yote, chuki yote na visasi.  Wakristo tunafanywa kuwa wafuasi wa Kristo na hivyo kuishi kwetu au kufa kwetu ni Kristo. Na Mtume Paulo anaendelea kutuambia kwamba: “Basi kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, michukuliana na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kulaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe Ninyi, vivyo na ninyi. (Kol 3: 12 – 13).

Kama tunataka kupata kipimo cha msamaha kwa wenzetu basi kipimo chake ni Mungu. Kwani Neno la Mungu linatuambia kwamba: “iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma” (Lk 6:36). Huruma yake inayoufunua upendo wake ni ya milele kwani yeye ni “mwema na mwingi wa huruma”. Hivyo si kusamehe mara saba tu, yaani kusamehe hadi kikomo fulani bali ni saba mara sabini ikimaanisha bila kikomo.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.