2017-09-11 13:46:00

Wosia wa Papa Francisko kwa familia ya Mungu nchini Colombia


Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Mtakatifu Petro Claver, Jimbo kuu la Cartagena, Jumapili, tarehe 10 Septemba, 2017, amewashukuru watu wa Mungu, viongozi wa Kanisa na Serikali, lakini kwa namna ya pekee, Rais Juan Manuel Santos aliyempatia mwaliko wa kutembelea Colombia. Amewashukuru viongozi na watu wote wenye mapenzi mema waliokuwa wanafuatilia tukio hili kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii.

Baba Mtakatifu amewashukuru wale wote waliojisadaka usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, hija hii ya kitume nchini Colombia inafanikiwa. Zimekuwa ni siku ambazo zimesheheni matukio mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa, mambo ambayo yamemwezesha kukutana na kusalimiana na umati wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Colombia. Watu na matukio yote haya anasema Baba Mtakatifu yameigusa sakafu ya moyo wake na kwamba, wao wamemtendea mambo makuu katika maisha na utume wake!

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, wosia anaopenda kuwaachia kabla ya kufunga vilago vya hija yake ya kitume nchini Colombia alioianza hapo tarehe 6 hadi tarehe 11 Septemba 2017 kila mtu ajitahidi kupiga hatua ya kwanza katika amani na upatanisho; ili wote waweze kutembea kwa pamoja katika mchakato wa kutafuta, ili kudumisha amani na maridhiano kati ya watu na hatimaye, kujenga umoja na udugu. Ilikuwa ni tarehe 8 Septemba 1654 Mtakatifu Petro Claver alipofariki dunia, baada ya kutekeleza huduma ya upendo kwa watumwa kwa kipindi cha miaka 40, daima ajikisadaka kwa ajili ya maskini. Mfano wake mahiri uwawezeshe wananchi wa Colombia kuwaendea kwa moyo radhi na wa upendo ndugu zao, kwani Colombia inawahitaji watu wake wote, ili waweze kukumbatiana katika amani na uhuru wa kweli unaovunjilia mbali ghasia, ili waweze kuwa kweli ni watumwa wa amani ya kudumu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.