2017-09-11 14:07:00

Papa Francisko: Salam na matashi mema kwa wakuu wa nchi na serikali


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 11 Septemba 2017 amehitimisha hija yake ya kitume nchini Colombia iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Demos el primer paso” yaani “Tupige hatua ya kwanza”, ambayo ilikuwa inafuata nyayo za watangulizi wake Mwenyeheri Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II katika mchakato wa kukuza amani na upatanisho miongoni mwa familia ya Mungu nchini Colombia. Akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia salam na matashi mema Rais wa Colombia, Nchi ya Netherland, Marekani, Ureno, Hispania, Ufaransa na Italia.

Kwa namna ya pekee, anamshukuru sana Rais Juan Manuel Santos na Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka alizomkirimia wakati wote wa hija yake ya kitume nchini Colombia. Anapenda kuwahakikishia wananchi wote wa Colombia sala zake na kwamba, anawashukuru kwa ukarimu waliomwonesha. Ataendelea kuwasindikiza katika sala ili kweli Colombia iweze kupata amani, ustawi na maendeleo. Alipowasili kwenye anga la Italia, Baba Mtakatifu amemwambia Rais Sergio Mattarella kwamba, sasa anarejea kutoka Colombia ambako amepata nafasi ya kukutana na watu wa familia ya Mungu nchini Colombia. Ameshangazwa sana na ushuhuda wa imani  na ukomavu wao wa maisha ya kiroho na kijamii. Anapenda kumhakikishia Rais Sergio na familia ya Mungu nchini Italia sala na matashi mema; Amani, utulivu na maendeleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.