2017-09-11 12:33:00

Papa Francisko: Lindeni utu wa binadamu na haki zake msingi!


Mji wa Cartegena kwa muda wa miaka 200 iliyopita ulisimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu na kwa takribani miaka 32 mji huu umekuwa ni kitovu cha haki msingi za binadamu ambazo zimesimamiwa kidete na Wamisionari Wayesuit akina Pedro Claver  y Corbero na wenzake. Huu ndio mji ambao Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hija yake ya kifchungaji nchini Colombia kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na  kauli mbiu “Utu wa binadamu na haki msingi za binadamu”.

Ibada hii imeadhimishwa kwenye Madhabahu ya Mtakatifu Petro Claver, mahali pa tafakari na upembuzi yakinifu kuhusu haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake anasema, Liturujia ya Neno la Mungu inakazia kuhusu: msamaha, kukosoana, jumuiya na sala. Injili inakazia umuhimu wa maisha ya kijumuya yanayomfanya mchungaji mwema kuacha kondoo 99 na kwenda kumtafuta kondoo mmoja aliyetokomea msituni, kielelezo cha ukarimu na msamaha wa Mungu kwa waja wake, kwani madhara ya dhambi yana athari zake katika maisha ya kijumuiya, kumbe kuna haja ya kuwa na ujasiri katika kusahihishana na kurekebishana katika safari ya maisha!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika hija yake ya kitume, amebahatika kusikiliza shuhuda za watu mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa kutafuta amani na upatanisho wa kitaifa, ili kujenga na kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Lengo ni kuondokana na tabia ya kutaka kulipizana kisasi. Mama Kanisa anapenda kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani inayofumbatwa katika majadiliano, ustawi na mafao ya wengi. Kanisa halihitaji mipango inayofanywa na watu wachache kwa ajili ya wachache; au wasomi wachache wanaodai kuzungumza kwa niaba ya wengine wote. Swala hili linahusu kukubali kuishi kwa pamoja ili kudumisha mafungamano ya kijamii na kitamaduni.

Majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya pande mbili ndiyo njia inayooneshwa na Kristo Yesu katika mchakato wa upyaisho wa Colombia; kwa kuwajengea watu ujasiri wa kukutana na kuzungumza; kufafanua, ili kuelewana na hatimaye kusameheana. Madonda ya historia, vita, chuki na utengano yanagangwa na kuponywa kwa njia ya haki, ukweli na malipizi ya madhara yaliyotendwa, ili kuhakikisha kwamba, matukio kama haya hayajirudii tena kwa siku za usoni. Kwa Wakristo, hii ni changamoto ya kufanya mabadiliko makubwa katika maisha kwa kukataa katu katu utamaduni wa kifo, ili kuambata Injili ya uhai na utamaduni wa watu kukutana unaofumbatwa katika elimu makini juu ya umuhimu wa amani, upendo na maisha.

Baba Mtakatifu anawataka wananchi wa Colombia kuwa ni mashuhuda, vyombo na wajenzi wa amani kwa kufanya mageuzi katika mfumo wa maisha unaoisambaratisha jamii kwa njia ya vita, ghasia na mafachuko ya kijamii ambayo wakati mwingine yanaonekana kuwa kama ni jambo la kawaida. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro Claver aliyethubutu kuwarejeshea tena watumwa: utu, heshima na matumaini yao, kuna haja pia kwa waamini kumwilisha ndani mwao tunu msingi za Kiinjili na kujenga utamaduni wa kukutana wote bila ubaguzi au kuwadhania kuwa ni maadui. Huduma kwa maskini ni chachu ya mabadiliko katika maisha kama alivyofanya Mtakatifu Maria Bernada Butler kwa ajili ya maskini wa mji wa Cartagena. Utamaduni wa watu kukutana unawawezesha kutambua na kudumisha haki zao msingi; udugu, utakatifu wa maisha ya binadamu wote na kwamba, Nyumba ya wote haina budi kujikita pia katika utunzaji bora wa mazingira.

Kristo Yesu katika Injili anawachangamotisha wafuasi wake kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kujenga na kudumisha Jumuiya dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu ana laani kwa nguvu zake wale wote wanaoendekeza biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya yanayoendelea kupandikiza mbegu ya kifo na uharibifu; mambo yanayofifisha matumaini ya watu kwa siku za usoni. Uchafuzi na uharibifu wa mazingira; utakatishaji wa fedha haramu; uchu wa mali na madaraka ni mambo ambayo ni hatari sana kwa uchumi, utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mifumo yote ya utumwa mamboleo; biashara haramu ya binadamu na viungo vyake ni hatari sana kwa maisha ya binadamu. Umefika wakati kwa familia ya Mungu nchini Colombia, kusimama kidete kutangaza na kushuhudia haki katika upendo, kwa kuvunjilia mbali mambo yote yanayotishia usalama wa maisha ya binadamu. Papa amewakumbuka wale wote waliosimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, changamoto kwa sasa ni kusimama kidete kutetea haki msingi za binadamu. Wananchi wote wa Colombia wana hamasishwa kuunganisha sauti zao ili kudumisha haki na ukweli, kwa kupiga hatua ya kwanza katika amani na upatanisho.

Baba Mtakatifu anasema, mchakato huu unawezekana ikiwa kama wananchi watakuwa na ujasiri wa kujikutanisha na Kristo Yesu; kwa kusamehe na kukubali kupokea msamaha; kwa kupenda na kupendwa; kwa kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujikita katika ujenzi wa jamii inayomsikwa katika usawa, haki na utunzaji bora wa mazingira. Wananchi waondokane na utamaduni wa kifo kwa kuwa na ujasiri wa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu mbali mbali na ujasiri wa kukosoana katika upendo na udugu, ili hatimaye, kujenga amani ya kweli inayomwilishwa katika matendo, kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwani hakuna lisilowezekana mbele yake na kwamba, daima yuko pamoja na watu wake hadi utimilifu wa nyakati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.