2017-09-10 14:22:00

Papa Francisko: Kanisa ni mali ya Kristo linapaswa kujipyaisha daima


Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Colombia, Jumamosi tarehe 9 Septemba, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa ndege wa Yohane Paulo II, huku akiongozwa na mada “Maisha ya Kikristo kama ufuasi wa Kristo”. Kutokana na mvua kubwa kunyeesha, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na msafara wake, walilazimika kutumia magari na hivyo ibada kuchelewa kuanza kwa takribani dakika 45. Kabla ya Ibada ya Misa, Baba Mtakatifu Francisko aliomba msamaha kwa umati mkubwa wa waamini uliokuwa unamsubiria kwa shahuku kubwa, huku ukitandikwa na mvua kubwa! Baba Mtakatifu amewashukuru kwa uvumilivu, udumifu na ujasiri wao na kwamba, kabla ya kuanza Ibada ya Misa Takatifu, wote waombe toba na maondoleo ya dhambi kwani binadamu wote ni wadhambi wanahitaji msamaha, huruma na upendo wa Mungu Baba Mwenyezi!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amepembua kwa kina na mapana dhana ya ufuasi wa Kristo tangu siku ile ya kwanza Yesu alipowaona na kuwachagua mitume wake wa kwanza na hivyo kuanza mchakato wa kujipyaisha, kwa kumtii na kumfuasa Kristo Yesu ili kuweza kukutana wagonjwa, watu waliotengwa na jamii pamoja na wadhambi, huku wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma kwa Mungu pamoja na jirani zao. Mitume wa Yesu walipaswa kuonesha uhuru kamili; utimilifu wa Sheria daima wakijitahidi kumfuasa Kristo Yesu kwa kuzingatia mambo msingi; kwa kujipyaisha kila wakati ili kushiriki katika maisha na utume wa Kristo Yesu! Mambo makuu matatu yanapaswa kuzingatiwa na wafuasi wa Yesu! Mosi ni kujikita katika mambo msingi! Pili ni Kujipyaisha na Tatu: ni kujishikamanisha na Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kujikita katika mambo msingi ni sehemu ya mchakato wa utekelezaji na utimilifu wa Sheria, jambo msingi katika maisha linalorutubisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto inayomtaka mwamini kutubu na kuongoka kama sehemu ya mchakato wa maisha mapya yanayothubutu kuambata upendo wa Mungu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, haitoshi kwa Mkristo kuwa na cheti cha Ubatizo, bali Mkristo daima anapaswa kutembea kumwelekea Yesu, ili kuonja uwepo wake wa daima na unaotenda kazi na hatimaye, kumwezesha mwamini kusikiliza kwa makini Neno la Mungu! Haitoshi hata kidogo kung’ang’ania ufafanuzi wa Mafundisho tanzu ya Kanisa, ikiwa kama mwamini ndani mwake ni mkavu kama kigae! Sheria zipo kwa ajili ya binadamu na Kristo Yesu ni Bwana wa Sabato.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, upyaisho wa maisha ya Kikristo ni sehemu muhimu sana ya ufuasi wa Kristo Yesu, jambo ambalo kamwe lisiwapatie waamini hofu! Kanisa linapaswa daima kuwa katika mchakato wa kujipyaisha katika maisha na utume wake kwa kujikita katika imani thabiti na matumaini ya Injili inayotangazwa na kushuhudiwa. Upyaisho wa maisha ya Kikristo unahitaji sadaka na ujasiri, kwa kutambua na kukiri udhaifu na mapungufu yanayoweza kujitokeza kama binadamu. Sheria, Kanuni na Taratibu ziwasaidie waamini kumfuasa vyema Kristo katika maisha yao ya kila siku. Waamini wawe tayari kuona na kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu kati ya watu wanaowazunguka! Waamini wawe na ujasiri wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wanaoomba msaada! Wawe na ushujaa wa kusimama kidete kuzima kiu ya haki na amani duniani. Nchini Colombia, anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna hali na mazingira yanayowataka wafuasi wa Yesu kuiga mtindo wa maisha ya Kristo mwenyewe kwa kumwilisha upendo katika mchakato wa amani na upatanisho dhidi ya vita, ghasia na mipasuko ya kijami.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuambatana na Yesu katika maisha ni jambo msingi linalopaswa kukua kila siku, ili kuwawezesha wafuasi wa Kristo kuwa na ujasiri wa kuzima njaa ya uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Watu wana njaa ya kutambuliwa utu na heshima yao kama binadamu, kwani katika historia, wamedhalilishwa na kunyanyaswa sana! Huu ni mchakato unaopaswa kutumiwa na Mama Kanisa ili kuwawezesha watu kama hawa kukutana tena na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Kanisa la Kristo linapaswa kuacha malango yake wazi, ili watu waweze kuonja na kuguswa na huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Kanisa haliwezi kuendelea kuwa ni Kanisa linalowanyooshea watu vidole! Kanisa si mali ya mtu binafsi, bali ni la Kristo mwenyewe! Yeye ndiye Bwana wa mavuno na msingi wa Hekalu. Kanisa halina budi kuwapatia waamini wote fursa ya kupyaisha na kurutubisha maisha yao kwa Yesu! Viongozi wa Kanisa watambue kwamba, wao ni wahudumu tu wa Mafumbo ya Kanisa na kamwe wasiwe ni kikwazo kwa watu wanaotaka kukutana na Mungu katika maisha yao. Yesu mwenyewe anawataka mitume wake kuonesha wema na ukarimu kwa kuwapatia upendo wa Mungu sanjari na kuwamegea ule Mkate ulioshuka kutoka mbinguni unaowawezesha kuwa Ekaristi inayotolewa kwa ajili ya ustawi na mafao ya jirani zao.

Mtakatifu Petro Claver alilitambua fumbo hili, akajisadaka kwa ajili ya kuwahudumia Waafrika waliokuwa utumwani nchini Colombia. Alitambua wito na dhamana yake, kiasi kwamba, akajisadaka kuwa ni mtumwa ili kuwasaidia wale ambao walikuwa wanateseka, waliotengwa na kunyanyaswa wakati wake! Kanisa nchini Colombia halina budi kujikita katika majiundo makini ya wafuasi wa Kristo kama walivyokazia Mababa wa Aparecida katika mkutano wao uliofanyika Medellin kunako mwaka 1968. Mitume wawe na uwezo wa kuona, kuamua na kutenda. Hawa wanapaswa kuwa ni wamisionari mitume wanaoweza kuangalia barabara pasi na ”makengeza”, wenye uwezo wa kuchambua mambo mintarafu jicho na Moyo Mtakatifu wa Yesu na hatimate kutenda kwa kutubutu, kwa ujasiri na uwajibikaji!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, yuko nchini Colombia ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo mintarafu Injili ya Kristo inayowawezesha kuwa huru na thabiti ndani ya Kristo. Wajitahidi kukumbatia kwa nguvu zao zote ufuasi wao kwa Kristo kwa kumtambua, kwa kumwachia nafasi ili aweze kuwaunda na kuwafunda kadiri ya mahitaji yake. Wajitahidi kumtafuta Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti na huduma katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Mwishoni, wamwombe Bikira Maria wa ”Candelaria” yaani „Bikira Maria wa mwanga angavu” aweze kuwasindikiza katika hija yao kama wafuasi wa Kristo kwa kumweka Kristo Yesu kuwa ni kiini cha maisha yao na kwamba, wao ni wamisionari wanaobeba ndani mwao mwanga na furaha ya Injili kwa watu wote wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.