2017-09-06 15:44:00

Umuhimu wa kukosoana kidugu!


Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya XXIII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa inatumbusha wajibu wetu wa kusahihishana makosa hasa kwa wale ambao tumepishana na kuwarudisha kundini. Pia neno hili latupatia njia bora za kutenda hilo, yaani namna ya kufanya hivyo.  Binti mmoja Lydia aliacha Kanisa kwa miaka tisa. Akaabudu miungu ya uongo kwa muda wote huo. Baada ya muda huo akarudi tena kanisani na wakati anaelezea maisha yake akatoa lawama nyingi kwa wale waamini kwamba hakuna hata mmoja aliyemtafuta muda wote ambapo alitoka nje ya kanisa. Akasema, nina hisi kwamba hakuna anayenihitaji hapa. Neno la Mungu siku ya leo inatualika kuangalia hali zetu za kutokujali kwetu hasa kwa wale ambao hawako kati yetu au tunaodhani hatuwahitaji.

Ni kwa nini Injili inatupata changamoto hii? Yaani kusahihishana makosa? Kama wanakanisa, kwa ubatizo wetu sisi ni makuhani, walimu na manabii. Kwa unabii wetu ni wasemaji kwa niaba yake Mungu. Katika somo la kwanza tunaona wazi wajibu wa nabii Ezekieli kwa watu wa Mungu – yule anayesikia neno la Mungu analitangaza. Tunaambia cha kufanya na namna ya kufanya – kama ilivyo katika Mt. 18:15 – kama mmoja akikukosea kae naye, akikusikiliza umempata. Hivyo wale walio vizuri zaidi kiroho basi wawasaidie wale walio dhaifu. Lengo la tendo hili la kikristo ni kumpata ndugu aliyepotoka na kupotea. Lengo si kutafuta ni nani mwenye makosa zaidi au kuanika kosa lake bali ni kumpata ndugu aliyepotea.

Hakika kusahihishana makosa si jambo rahisi kibinadamu ingawa inatakiwa hivyo na inawezekana. Tukumbuke Neno la Mungu katika Lk. 6:41 – mbona unakiona kibanzi kilichomo jichoni mwa nduguyo, lakini boriti iliyomo jichoni mwako huiangalii? Rais Nelson Mandela wa Afrika Kusini alipounda kamati ya usuluhishi na upatanisho ilionekana kama tishio kubwa kwa amani na usalama wa nchi. Mbele ya wengi ilionekana kitu kigumu na hatari lakini mwishoni ilitoa mafanikio makubwa. Ni mahali hapa mtenda maovu na aliyetendewa maovu walipata nafasi ya kukutana uso kwa uso, kukaa pamoja, mmoja akakiri kosa lake dhidi ya mtendewa, kuombana msamaha na msamaha na upatanisho kufikiwa. Tunafahamu kuwa tendo la upatanisho ni jambo gumu sana kwani hata mtenda jema au anayedai haki yake au anayetaka kusahihisha aweza kuonekana tishio mbele ya baadhi ya watu.

Kupatana na adui au kupatanishwa na mkosaji wako ni kitu kigumu sana kwa mwanadamu. Tunaona jinsi watu wanavyohangaika kulipa kisasi kwa waliowakosea. Au jinsi mtu anavyohangaika kutafuta haki ikiwa amekosewa. Lakini kutafuta haki huku hupelekea pia hata kumdhuru mwingine. Hutokea pia hata hilo hitaji la kutafuta haki likaongeza uadui zaidi.

Kadiri ya mafundisho na mapenzi yake Mungu, tiba sahihi ya ugomvi ni upatanisho, pamoja na ugumu wake ulivyo. Mungu ametaka upatanisho nasi na kati yetu wenyewe. Kinachoonekana wazi ni kuwa  ili upatanisho utokee ni lazima Mungu aingilie kati. Mungu mwenyewe ndiye asili ya msamaha. Sisi tunaalikwa kushiriki katika tendo hili. Tunasoma katika 2Kor. 5:17 .. Mtume Paulo anasema mpatanishwe na Mungu. Na anasema kwa vile sisi ni watu wake Bwana, sisi ni viumbe vipya. Tendo halisi la upatanisho hutoka kwa Mungu, kwa njia ya mwanawe na katika sehemu hii ya barua ya mtume Paulo tunasoma kuwa naye anatupa sisi huduma ya upatanisho. Naye Mtakatifu Fransisko wa Assisi husali katika sala zake ‘Ee Bwana unifanya chombo cha amani yako”. Hivyo huu unakuwa ni wajibu na si hiari. Tendo la upatanisho lina asili yake ndani ya Mungu na sisi watoto wake tunapaswa kuwa watu wa upatanisho. Mtume Paulo anasisitiza haja ya mwanadamu kuupokea huu upatanisho. Wakati mwingine inakuwa vigumu kujua ni nini hasa cha kufanya – kuongea au kukaa kimya. Hapa ndipo inaingia sheria ya dhahabu kama ilivyo katika somo la pili la leo – msiwe na deni kwa mtu ye yote, isipokuwa deni la kupendana. Kwani mwenye kumpenda mwenzake ameitimiza sheria.

Ndicho tunachoona katika masomo yetu ya leo – kusahihishana na kusameheana kindugu. Tunatafakarishwa na tabia ya dini ya kibiblia yenye sifa kuu tano – uchaguzi, agano, jumuiya, upendo, msamaha. Kimsingi Mungu ametuchagua kwa upendo na uhuru wake kuwa watu wake. Huu upendeleo unadhihirishwa kwa njia ya agano na jumuiya ya watu – taifa. Hili agano linafunga mahusiano, makubaliano yanayofanywa na pande mbili. Matokeo yake ni kuunda jumuiya ya watu – Kumb. 7:6 – kwa kuwa u taifa lililotakaswa kwa Bwana Mungu wako; ndiwe uliyechaguliwa na Bwana Mungu wako uwe taifa lake yeye, kupita mataifa yote yaliyoko duniani. Hili taifa linakuwa mali yake Mungu – 1Pt. 2:10 – zamani mlikuwa si taifa, lakini sasa mmekuwa taifa la Mungu, zamani hamkujaliwa huruma, lakini sasa mmehurumiwa.

Hii ndiyo jumuiya ambayo inawajibika kwa Mungu na Mungu anatenda ndani yake. Wokovu wetu unatokana na mpangilio huu. Huu upendo unaoelezwa kwa njia ya kusahihishana makosa ni ule upendo unaotambua majukumu au wajibu binafsi kwa mwingine kwa sababu ya lile agano. Ni pendo la agano. Binadamu ni dhaifu na mdhambi. Ni kwa sababu hii mtu anaalikwa kukimbilia hilo pendo. Ndilo hilo pendo linalotusukuma tunapokosea kuombana msamaha. Tendo hili takatifu likifanyika basi huruma takatifu kwa watu wake inapatikana. Na Mungu anapenda hili lifanyike kati ya watu wake – Yoh. 20:22-23 - baada ya maneno hayo, akawapulizia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu, wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa, wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa. Kwa upande mwingine wa lile agano kuna uhusiano kati ya mtu na jumuiya. Mungu amefanya agano na jumuiya na hivyo sote tunabanwa na agano hilo.

Hii inaonekana katika somo la kwanza ambapo nabii anakumbushwa kuwaambia watu wake dhambi yao kwani asipofanya hivyo wote wataangamia. Na hilo liko wazi katika injili. Sisi ni jumuiya ya waamini, iliyokombolewa kwa upendo wake Mungu na kufungwa na agano. Na anasema wazi, kama kanisa au jumuiya inawezekana kufunga au kufungua, kusamehe au kulaani. Hapa ndipo sote tunawajibishwa. Tendo la upatanisho si hiari tena kwa sababu sisi tumefungwa na pendo lake Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.