2017-09-06 11:01:00

Papa Francisko "ang'oa majembe" kuelekea Colombia!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuondoka kuelekea nchini Colombia kwa ajili ya hija yake ya kitume inayoongozwa na kauli mbiu “Demos el primer paso” yaani “Tupige hatua ya kwanza”, Jumanne, tarehe 5 Septemba 2017 majira ya jioni, alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma, ili kujikabidhi kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi! Taarifa hii imethibitishwa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala zao wakati huu wa hija yake ya kitume nchini Colombia kuanzia tarehe 6-11 Septemba 2017. Anasema, hii ni hija ya amani na upatanisho kwa familia ya Mungu nchini Colombia. Hii ni hija ya 20 ya Kitume inayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko nje ya Italia na ni safari ya tano Amerika ya Kusini.

Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa tatu kutembelea Colombia, baada ya Mtakatifu Yohane Paulo II kutembea nchi hii kunako mwaka 1986 na Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1968. Hii ni safari ya masaa 12 angani! Anatarajiwa kuwasili saa 10:30 kwa saa Colombia sawa na saa 5:30 Usiku kwa saa za Ulaya. Kwa Afrika Mashariki itakuwa ni Saa 6:30 Usiku wa manane! Rais Juan Manuel Santos Calderon anasema, Colombia iko tayari kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko. Msukumo wa pekee ni haki, amani na upatanisho miongoni mwa familia ya Mungu nchini Colombia.

Katika mkesha wa ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia, Serikali pamoja na Kikosi cha Mapinduzi ya Kijeshi “FARC” zilitiliana sahihi mkataba wa amani ya kudumu. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Vatican kuhusu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia anasema, inafumbatwa katika mchakato wa amani, upatanisho na msamaha, ili kuweza kupokea huruma na upendo wa Mungu, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya kwa maisha ya wananchi wa Colombia.

Askofu mkuu Octavio Ruiz Arenas, Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Villavicencio, ambaye kwa sasa ni kati ya maafisa waandamizi wa Vatican anasema, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuhimiza mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kweli unaobubujika kutoka katika nyoyo za watu, ili kutorudia tena makosa yaliyojitokeza huko Amerika ya Kusini, ambapo wapiganaji wa msituni waliachwa “soremba” bila kuingizwa katika mafungamano ya kijamii na matokeo yake, wakajiunga na makundi ya wahalifu Amerika ya Kusini! Matokeo yake ni kushamiri kwa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Mtakatifu Yohane Paulo II na Mwenyeheri Paulo VI walizungumzia changamoto hizi kwa nyakati mbali mbali, lakini ushauri wao, haukuweza kufua dafu! Ni matumaini ya wapenda amani kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia itaweza kuzaa matunda ya haki, amani, upatanisho, msamaha, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Ratiba elekezi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia inaonesha kwamba, Alhamisi tarehe 7 Septemba 2017, akiwa mjini Bogotà anakutana na viongozi wa Serikali, atatembelea Kanisa kuu la Jimbo kuu la Bogotà. Anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia; Kamati kuu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM na baadaye, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Simon Bolivar. Baba Mtakatifu Francisko akiwa mjini Bogotà, anapenda kuwaalika waamini kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai na familia, ili kugundua tena ndani mwao zawadi ya maisha pamoja na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ili hatimaye, waweze kutangaza Injili ya familia inayosimikwa katika amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.