2017-09-05 14:09:00

Raila Odinga aweka pingamizi la uchaguzi mkuu tarehe 17 Oktoba 2017


Wafula Chebukati Mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi na Mipaka ya Kenya, IEBC amesema marudio ya uchaguzi mkuu nchini Kenya yatafanyika tarehe 17 Oktoba 2017 kwa kuwashirikisha Rais Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza William Samoei Ruto na Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga pamoja na mgombea mwenza Stephen Kalonzo Musyoka. Hakutakuwa na uteuzi mpya wa wagombea wa urais katika uchaguzi huo upya. Tume inawataka wadau pamoja na wananchi wote wa Kenya kuonesha uvumivu na uelewa; ili kuwezesha uchaguzi mkuu wa marudio kuwa huru, wa haki na unaoaminika na wadau wote!

Wakati huo huo, Bwana Raila Odinga, Jumanne, tarehe 5 Septemba 2017 amesema chama chake hakitashiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika hapo tarehe 17 Oktoba 2017 ikiwa kama hautapewa uhakika wa kisheria na kikatiba. Chama cha upinzani kwa sasa kinakusudia kufungua kesi kadhaa ili kupinga matokeo ya wabunge na wawakilishi wa Serikali za mitaa. Bwana Odinga anataka pia maafisa sita wa Tume huru ya uchaguzi na Mipaka ya Kenya, IEBC kufukuzwa kazi na hatimaye, kuchunguzwa kwa makosa ya jinai. Taarifa zinaonesha kwamba, kiasi cha kura milioni 1.4 zilikuwa na itilafu. Tukio Mahakama kuu kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu limepongezwa na Bwana Odinga kuwa ni la kishujaa na la kihistoria, Barani Afrika, ingawa wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanahofia mpasuko mkubwa wa kijamii! Mahakama kuu umejijengea heshima kwa kusimamia misingi ya ukweli na uwazi.

Katika kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, Mahakama Kuu iliitupia lawama Tume huru ya uchaguzi na Mipaka ya Kenya, IEBC. Majaji wa tume hiyo hawakuandaa uchanguzi huo kwa viwango vilivyowekwa kwenye katiba na sheria za uchaguzi, na kwamba kulitokea kasoro nyingi sana katika mchakato wa kutangaza matokeo. Chebukati amesema tume hiyo inafanyia tathmini mifumo na taratibu zake kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa marudio

Majaji wa mahakama ya juu waliahidi kutoa hukumu kamili kabla ya tarehe 22 Agosti 2017 Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na IEBC kuhusu uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, Rais Uhuru Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku naye Bwana Raila Odinga akipata kura 6,762,224. Wapinzani walipinga matokeo hayo wakisema, mitambo ya tume hiyo ya uchaguzi ilidukuliwa na wajanja ili kumnufaisha Rais Uhuru Kenyatta. Baada ya kutangazwa kwa matokeo, machafuko ya kisiasa yalijitokeza kwenye baadhi ya maeneo na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha, jambo ambalo lilikemewa vikali sana na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.

Ni matumaini ya wapenda amani ndani na nje ya Kenya kwamba, marudio ya uchaguzi mkuu yatafanyika kwa amani na utulivu ili kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya kitaifa! Ni jambo lisilokubalika kwamba, kila wakati kunapotokea uchaguzi mkuu nchini Kenya lazima damu ya watu wasiokuwa na hatia imwagike!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.