2017-09-05 12:26:00

Mada zinazoongoza hija ya kitume ya Papa Francisko nchini Colombia!


Askofu mkuu Oscar Urbina Ortega, Rais wa Baraza al Maaskofu Katoliki Colombia katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Colombia, Ijumaa tarehe 8 Septemba 2017 ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kuwatangaza wenyeheri Askofu Jesùs Emilio Jaramillo Monsalve wa Jimbo Katoliki la Arauca aliyeuwawa kikatili kunako tarehe 2 Oktoba 1989 pamoja na Padre Maria Ramirez Ramos, aliyeuwawa kikatili tarehe 10 Aprili 1948. Hii itakuwa ni siku ya Upatanisho wa Kitaifa takribani baada ya miaka 50 ya vita ya wenyewe kwa wenyewe: Mwaliko wa kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Juma la Amani Colombia, lililoanza kutimua vumbi tarehe 3 na litahitimishwa tarehe 10 Septemba, 2017. Askofu mkuu Oscar Urbina Ortega anakaza kusema, upatanisho ndiyo mada muhimu sana inayofanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu nchini Colombia kwa wakati huu, changamoto kwa familia ya Mungu nchini Colombia kupiga hatua ya kwanza katika mchakato wa haki, amani na upatanisho, ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, kila mwanchi akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake!

Baba Mtakatifu Francisko akiwa mjini Bogotà, anaalikwa kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai na familia, ili kuwasaidia wananchi wa Colombia kugundua tena ndani mwao zawadi ya maisha pamoja na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ili kutangaza Injili ya familia inayosimikwa katika amani. Baba Mtakatifu akiwa Villavincencio, tema ya siku ni upatanisho na Mungu, jirani pamoja na kazi ya uumbaji, ili kweli familia ya Mungu nchini Colombia iweze kuwa ni chombo na wajenzi wa haki, amani na upatanisho. Mjini Medellìn, Baba Mtakatifu, atawaalika waamini kujikita katika mchakato wa uinjilishaji, kwa kujikita katika ufuasi, umisionari na utume; kwa kutambua kwamba, uinjilishaji mpya unajikita katika ushuhuda wa maisha.  Akiwa Cartagena atakazia haki msingi za binadamu dhidi ya utumwa mamboleo unaonyanyasa na kudhulumu: utu na heshima ya binadamu, kama alivyofanya Mtakatifu Petro Claver katika mapambano dhidi ya biashara ya utumwa.

Askofu mkuu Oscar Urbina Ortega, Rais wa Baraza al Maaskofu Katoliki Colombia anakaza kusema, Mama Kanisa ataendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya haki, amani na upatanisho kati ya watu, dhamana inayopaswa kuvaliwa njuga na familia nzima ya Mungu nchini Colombia. Huu ni mchakato unaowawezesha hata wale waliokuwa upande wa upinzaji kujisikia kuwa ni sehemu ya familia ya Mungu nchini Colombia, tayari kushiriki katika ujenzi wa demokrasia ya kweli; ustawi na maendeleo ya wengi. Uwepo wa Baba Mtakatifu unapenda kuhamasisha umuhimu wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana; umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kukumbatia mchakato wa upatanisho na maridhiano kati ya watu unaofumbatwa katika msamaha wa kweli unaobubujika kutoka katika undani wa maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.