2017-08-31 18:09:00

Papa Francisko ametuma ujumbe kwa tukio la Sikukuu ya Mt. Rosa wa Lima


Jumatano 30 Agosti Kanisa  Katoliki lilikuwa linamkumbuka Mtakatifu Rosa wa Lima, mahali ambapo Ibada ya Misa Takatifu ilifunga nchini Peru Jubilei ya mwaka wa 400 tangu kifo cha Mtakatifu Rosa wa Lima, Matakatifu huyo anayependwa sana na wazalendo nchini Peru.
Aliyeongoza misa katika Kanisa Kuu la Lima alikuwa ni mwakilishi wa Papa Kardinali Raúl Eduardo Vela Chiriboga Askofu Mkuu mstaafu wa Quinto. Kardinali Aduardo Vela alisoma ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya tukio hilo la Jubilei, ambapo Baba Mtakatifu  anawatakaa waamini wote kuendeleza ibada maalumu kwa Mtakatifu Rosa wa Lima ili kwa maombezi yake  kwa Mungu  wapate neema nyingi majimbo yote ya Lima, nchi ya Peru na ulimwengu mzima.

Katika Barua hiyo, Baba Mtakatifu Francisko anamwelezea Mtakatifu Rosa wa Lima kwenye  sura ya Wimbo uliyo bora kwamba ni mwanamke aliye kulia katika ua lenye miiba.Hiyo ni kutokana na kwamba alijitesa mwenyewe kufanya malipizi, katika kuonesha upendo upeo wa kuweza kupata maisha ya milele katika Kristo. Baba Mtakatifu anaendelea kueleza; akiwa mdogo Mtakatifu Rosa alikuwa rafiki wa Bwana  na kujitoa mwenyewe sadaka akijiimarisha katika karama. Tangu wakati huo kwa maombezi ya Bikira Maria na kuiga mfano wa Mtakatifu Caterina wa Siena, alijitoa sadaka maisha yake kwa Mungu, kwa kuvaa nguo ya utawa wa tatu wa wa kidomenikani .Na mwisho Baba Mtakatifu Francisko anakumbuka upendo wa Mtakatifu Rosa kwa ajili ya uumbaji, ambapo kwa namna ya pekee anawaalika kila kiumbe kumsifu Mungu.

Rosa wa Lima kwa jina la ubatizo alikuwa ni  Isabel Flores y de Oliva  alizaliwa tarehe 20 Aprili 1586.Akiwa ni mtoto wa kumi kati ya watoto kumi na tatu. Anatokea katika familia ya wenye uwezo kutoka nchi ya Uhispania waliohamia Lima, Peru.Tangu udogo wake alihisi wito na hasa kwa ajili ya kumpenda sana Mtakatifu Caterina wa Siena aliyekuwa kama mfano wake wa kuigwa. Na akiwa  mlei wa miaka 20 alijiunga na utawa wa tatu wa Mt. Domeniko. Alipata umaarufu kwa juhudi zake katika maisha ya kiroho na kwa huduma zake  za huruma kwa maskini wa mji wake huo. Alikufa tarehe 24 Agosti 1617, ni Mwamerika wa kwanza kutangazwa Mtakatifu katika Kanisa Katoliki. Kwanza alitangazwa mwenye heri na Papa Klementi IX tarehe 10 Mei 1667, pia akatangazwa mtakatifu tarehe 12 Aprili 1671 na Papa Klementi X. Ni msimamizi wa nchi ya Peru na katika ulimwengu mpya pamoja na nchi ya Ufilippini.

Sr Angela Rwezaula

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
 
 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.