2017-08-30 17:03:00

Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kushikamana kulinda mazingira


Dini mbali mbali duniani zinapaswa kusaidia mchakato wa kutafuta na kudumisha haki na maani; utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Lengo ni kujenga jamii inayosimikwa katika Injili ya upendo, udugu na mshikamano ili kupambana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Ni wajibu wa dini mbali mbali kuwekeza katika elimu makini na endelevu; malezi na majiundo kwa watoto na vijana wa kizazi kipya. Jamii ielimishwe juu ya umuhimu wa kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwani uharibifu wa mazingira una madhara makubwa yasiyochagua wala kubagua maskini na matajiri.

Huu ni mchango ulitolewa na Askofu Miguel Angel Ayuso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, huko, nchini Chile, Jumatatu, tarehe 29 Agosti 2017 katika mkutano wa utunzaji bora wa mazingira ulioandaliwa na Serikali ya Chile kwa kushirikiana na Taasisi ya Majadiliano ya Kidini kutoka Buenos Aires, nchini Argentina kwa kuongozwa na kauli mbiu “Amerika katika majadiliano. Nyumba yetu ya pamoja”. Ikumbukwe kwamba, majadiliano ya kidini ni sehemu muhimu sana katika maisha ya binadamu na wala hili si jambo la anasa!

Majadiliano ya kidini ni chombo muhimu sana kwa ajili ya kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni chachu madhubuti ya kutibu na kuganga madonda ya: chuki, uhasama, utengano na mipasuko ya kidini na kijamii; hali inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku, kutoka kwa waamini wa dini mbali mbali duniani. Dini zinapojikita katika mchakao wa majadiliano ya kidini pamoja na kutambua umuhimu wa kujizatiti katika kulinda na kudumisha mafao ya wengi, hapo, dini zinaweza kutekeleza dhamana kubwa katika maisha ya watu.

Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Haya ni majadiliano yanayofumbatwa katika msingi wa kazi ya uumbaji unaowaunganisha wote kama sehemu muhimu sana ya sera za kimataifa. Inasikitisha kuona kwamba, tema juu ya utunzaji bora wa mazingira wakati mwingine haipewi kipaumbele cha kutosha au kuna wakati inabezwa na kuonekana kana kwamba, ni jambo la mtu au kikundi cha watu binafsi.

Lakini, Jumuiya ya Kimataifa inasahau kwa haraka madhara makubwa yanayoendelea kusababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, binadamu wote wanaunda familia kubwa ya watu wa Mungu inayopaswa kuwajibika barabara katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anakazia majadiliano ya kidini na kiekumene yanayopania kujenga na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, dini iwe ni kichocheo cha maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Pale ambapo vitendo vya binadamu haviheshimu utunzaji bora wa mazingira, madhara yake ni makubwa katika maisha ya watu na mali zao. Matokeo yake ni ubaguzi na nyanyaso zinazounda utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine! Huu ndio msingi wa uchumi unao “wabagua na kuwachambua watu kama karanga”.

Utengano na ubaguzi una madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu. Huu ndio mwanzo wa ukosefu wa haki jamii; kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi; njaa na ukame. Askofu Miguel Angel Ayuso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, anasema, tema ya wakimbizi na wahamiaji imekita mizizi katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuivalia njuga na wala si kubaki imejifungia katika kimya kikuu kwa kutojali wala kuguswa na hatima ya maisha ya wakimbizi na wahamiaji duniani.

Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ni tete na nyeti sana; lakini, ikiwa kama waamini wa dini mbali mbali watashirikishwa kwa dhati, wanaweza kujenga mfumo wa uchumi endelevu unaojikita katika mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili; ili kukuza na kudumisha haki jamii, amani na maridhiano kati ya watu sanjari na kuheshimu ekolojia endelevu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.