2017-08-30 17:22:00

Ujasiri wa kuacha yote na kuthubutu kumfuasa Kristo!


Tunasikia katika injili ya leo Yesu akisema ye yote atakaye kunifuata ajikane mwenyewe, achukue msalaba wake na anifuate.  Kwa vile ye yote atakaye kuiokoa nafsi yake ataipoteza, ila aipotezaye nafsi yake kwa ajili yangu, ataiokoa. Ina maana gani kujikana? Na kwa nini kujikania? Mwaliko huu ni mgumu sana kwa watu wengi kama si wote. Mwanafalsafa Friedrich Nietzsche alikataa wazi wazi fundisho hili. Tutafute jibu: mfano wakati wa utawala wa Hitler - unazi – Wayahudi wengi walipelekwa kwenye makambi ya maafa. Wao walidanganywa kuwa wanapelekwa sehemu salama. Wengi wakaingia kwenye treni bila kujua. Kumbe walikuwa wanakiendea kifo. Wenyeji wachache walijua njama hii na ilipotokea kuwa wamesimama katika vituo, wale wenyeji huku wakijificha waliwaeleza ukweli huo. Tokeni, kimbieni. Wachache walifaulu kutoroka lakini wengi hawakufaulu. Waliuawa kama wadudu.

Huu ni mfano mgumu sana, lakini yaelezea hali zetu. Treni zetu za maisha tunazosafiria zinaelekea wapi kama si mautini? Tuko salama katika safari zetu mbalimbali tuzifanyazo?  Hapa hakuna mashaka. Sisi tuna asili ya kifo pia. Inachosema injili leo tunapoaambiwa kujikana, ni kutuita kutoka nje ya hii treni na kupanda ile treni ya uzima. Treni inayoelekea uzima ni imani katika yeye – ye yote aniaminiye, hata kama akifa, ataishi milele. Hapa tunapata jibu moja. Kumwamini yeye aliye Mungu wa kweli. Hapa tunapata jibu la kwanza.

Mtume Paulo anaelewa vizuri pia injili hii ya leo akitualika kuhama toka treni ya kifo na kuingia treni ya maisha. Aanasema, siyo mimi niishiye bali Kristo aishi ndani yangu. Tukiwa ndani ya Kristo, tuna uhakika wa uzima. Na hapa neno la injili ya leo linapata maana – wito wa kujikana. Ile dhana ya kuwa ni kupotea/kupoteza kama wadhaniavyo wengi inabadilika. Hili ndilo chaguo sahihi tuwezalo kulifanya katika maisha yetu. Mengine yote ni ubatili mtupu. Kujikana huko katika injili kunapata maana hapa. Jibu la kuacha yote na kufanya yote na Kristo. Hapa tunapata jibu la pili.

Lakini iwe wazi hapa – Yesu hatuambii kujikana utu wetu. La hasha. Ila kukana vile tulivyochukua bila Kristo. Sisi ni sura yake Mungu. Hii ni lazima ibaki. Tuko vizuri kabisa. Hatuambiwi kujikana sura yake Mungu, ila kile ambacho sisi tumekitengeneza tofauti na mpango wake Mungu, tofauti na sura yake Mungu kama  mielekeo yetu ya kidhambi tangu dhambi ya asili kama kiburi, uchoyo, tamaa mbaya za mwili,  hasira,  ulafi, chuki, uvivu n.k. Mtume Paulo anasema kuwa mizizi hiyo ya dhambi inaharibu sura ya Mungu tuliyoumbwa nayo. Inatupatia sura za kidunia na kuondoa sura ya Mungu ndani yetu.

Kujikatalia kwa hiyo inakuwa siyo kujitakia kifo bali kutafuta uzima, uzuri na furaha. Wengi wanadhani kujikana au kujikatalia  ni kupoteza. Kumbe ni kujifunza lugha ya mapendo ya kweli. Mwanafalsafa Mdenishi – Kierkegaard anatumia lugha ya kibinadamu kuelezea mfano wa kujikana. Anatumia mfano wa vijana wawili wanaopendana, ila wanatoka mataifa mawili tofauti na wanaongea lugha mbili tofauti na wakiwa na mila na desturi tofauti. Ili mapenzi yao yabaki na kudumu, anasema ni lazima mmoja wao ajifunze lugha ya mwenzake, mila na desturi ya mwenzake. Vinginevyo hawataweza kuwasiliana na mapenzi yao hayatadumu. Je hawa wamepoteza au wamepata? Anaendelea kusema – ndivyo ilivyo kati yetu na Mungu. Tunaongea lugha ya mwili, yeye huongea lugha ya roho, tunapongea lugha ya ubinafsi, yeye huongea lugha ya mapendo.

Kujikana huku anakotualika Kristo leo ni kuongea lugha ya Mungu ili tuwasiliane naye, na hivyo pia ni kujifunza huko kwatuwezesha kuongea kati yetu. Hatutaweza kuwasiliana vizuri, kusema ndiyo kwa mwingine, kama sote hatuwezi kusema hapana kwetu wenyewe.  Matatizo mengi na fujo nyingi katika maisha hutokea endapo mmoja hatakuwa tayari kujitoa kwa mwingine – mifano iko mingi – katika familia, jumuiya, n,k.  Mahali po pote penye sadaka ya kweli – kuna mafanikio, maisha bora. Familia ambayo imetoa sadaka, utume ambao umetoa sadaka n.k – una mafanikio na maendeleo mazuri.

Maisha ya shahidi Mt. Maximillian Maria Kolbe yatusaidie kuelewa neno hili la Yesu leo.  Anaokoa maisha kwa kutoa maisha yake. Alikuwa padre, mwana habari  na mpinzani mkubwa sana wa unazi. Hii ilipelekea kufungwa gerezani. Katika gereza lao alitoroka mfungwa mmoja na ikatoka amri kuwa wafungwa kumi wauawe. Wakachaguliwa watu 10 na kati yao alikuwapo kijana mmoja. Padre Kolbe alimfahamu vizuri na akamwonea huruma. Yeye aliamini kuwa unazi utashindwa. Padre Kolbe akajitolea kufa akichukua nafasi ya yule kijana kwa vile alisema huyu bado mdogo, ana familia changa na bado ana muda wa kutengeneza maisha yake. Walihukumiwa kufa kifo cha njaa. Wa mwisho kufa kwa kuchomwa sindano alikuwa padre Kolbe. Katika gereza ambalo ukuta wake umejengwa kwa mawe walikuta alama ya msalaba mkubwa ukutani iliyochorowa kwa vidole vya Padre Koble. Leo hii ni mtakatifu shahidi wa upendo. Hakika huyu ndiye jirani wa kweli. Alitoa maisha yake kwa ajili ya mwingine. Je huyu alipoteza au alipata?

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.